• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
CAROLINE OUMA: Mwigizaji na msanii wa nyimbo za injili

CAROLINE OUMA: Mwigizaji na msanii wa nyimbo za injili

Na JOHN KIMWERE

Ni miongoni mwa wanadada ambao wameamua kujituma kwa udi na uvumba kuvumisha tasnia ya filamu nchini. Ni taaluma aliyoiwazia tangu akiwa mdogo. Ingawa hajapata mashiko dada huyu aliyezaliwa mwaka 1982 anaamini anauwezo tosha kufikia hadhi ya kimataifa katika uigizaji.

Caroline Akinyi Ouma ambaye katika usanii anafahamika kama Caroline Warah kando na uigizaji ni mghani wa nyimbo za injili, msusi pia anamiliki kanisa liitwalo Jesus Prophetic Ministries linalopatikana katika mtaa wa Umoja 2 Kaunti ya Nairobi.

ANIKWA

”Binafsi nilivutiwa na uigizaji mwaka 1998 nikiwa shule nilipotazama kipindi cha Papa Shirandula ambacho hupeperushwa kupitia runinga ya Citizen ya humu nchini,” alisema na kuongeza kuwa alivutiwa zaidi na uigizaji wake Wilbroda.

Hata hivyo anasema la mno ni talanta iliyo ndani ya roho yake. Katika mpango mzima msanii huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa lakini ni moja tu ‘Anikwa’ iliyofanikiwa kupata mpenyo na kupeperushwa kupitia Switch TV.

Pia ameshiriki filamu iitwayo ‘Mpango wa Kando’ inayotazamiwa kuachiwa baadaye mwaka huu iliyotengenezwa na Vuma productions.

Anasema amepania kupambana mwanzo mwisho anakotaka kufikia upeo wa kimataifa kama mwigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood), Florence Ozonkwo.

NYIMBO ZAKE

Kama mwimbaji wa fataki za injili dada huyu anajivunia kutunga na kurekodi albamu mbili: ‘Anania na Safira,’ na ‘Nakupenda.’ Albamu ya Anania na Safira inasheheni nyimbo kama: ‘Anania na Safira,’ ‘Apako nyingi,’ ‘Nitakuimbia,’ ‘Majaribu,’ ‘ Upendo wa Yesu,’ ‘Ombi langu,’ ‘Pigana naye,’ na ‘Usinipite.’ Nayo albamu ya pili, Nakupenda inajumuisha ‘Onge moro,’ ‘Nakupenda.’ Nyimbo zake zinapatikana kupitia mtandao wa Youtube:Caroline Warah.

”Kwa waigazaji wa humu nchini ningependa kufanya kazi na Rufena mama yake Sylus ambaye huigiza kwenye kipindi cha Maria ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV,” alisema na kuongeza kuwa ingawa hajafanikiwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya uigizaji kwake ni ajira kama nyingine.

Kimataifa anasema angependa sana kufanya kazi na waigizaji mahiri kama Mercy Johnson na Ini Edo wazawa wa Nigeria. Mercy Johnson ameigiza filamu kama ‘The Local Drycleaner’ na ‘Top secret.’ Naye Ini Edo ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘Love of my life,’ na ‘Miss me,’ kati ya zingine.

CHANGAMOTO

Dada huyu anasema hakuna sekta isiona pandashuka zake. ‘Binafsi mwaka jana nilikutana na kisa ambapo watu wengi walionekana kunishangaa baada ya kushiriki kipindi cha Anikwa,” anasema na kuongeza kwamba ukweli wa mambo msanii akishiriki uigizaji sio uhalisia wa maisha yake. Kadhalika anasema amegundua kwamba kama haujapata umaarufu uigizaji sio ajira ya kutengemea kujikimu kimaisha.

Anadokeza kuwa nyakati nyingi msanii ukawia bila kufanya kazi yoyote ilhali anahitaji hela za mahitaji ambapo hali hiyo huchangia mhusika kuwazia kujiunga na shughuli zingine za kusaka riziki.

MAWAIDHA

Mwigizaji huyu anataka wenzie wanaoibukia kuwa wabunifu endapo wanapania kupenya katika sekta hii. ”Waigizaji wapya kwenye gemu wafahamu hakuna mteremko pia lazima wamakinike kama sivyo ni rahisi kuangukia meno ya maprodyuza ambao hupenda kuwashusha hadhi ya wasanii wa kike,” alieleza. Kadhalika alisema ukuaji wa teknologia unatoa njia muafaka kuitumia kusambaza kazi za sanaa yao ili kutambulika na wengi kote.

You can share this post!

BI TAIFA AGOSTI 29, 2020

SANDRA TENAI: Alenga kuwa mwigizaji na mwanahabari mtajika