Makala

CHADEMA chapinga tume aliyounda Rais Samia kuchunguza fujo za uchaguzi

Na CHARLES WASONGA November 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)kimepinga tume iliyoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchungeza chanzo cha ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kwenye taarifa aliyoitoa Novemba 19, 2025 Naibu Mwenyekiti wa chama hicho John Heche alisema hawatambui tume hiyo na majukumu yake.

Kulingana na chama hicho, Rais Samia hana ukubalifu wa kisiasa, kisheria na kiutu kuunda asasi yoyote ya kuchunguza maovu kinachodai yalichochewa na utawala wake.

“Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kingependa kuwaarifu raia wa Tanzania na jamii ya kimataifa kwamba hatutambui Tume ya Uchunguzi iliyoteuliwa na Samia Suluhu Hassan, aliyejilazimisha mamlakani bila idhini ya raia. Tume hiyo inaongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman na kimetwikwa wajibu wa kuchunguzi maovu yaliyodaiwa kutokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29,” Heche akasema.

Naibu huyo wa mwenyekiti alisema uteuzi wa tume hiyo unakiuka viwango vya kidemokrasia, akirejelea ripoti za waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) zilihoja uhalali wa uchaguzi huo.

“Msimamo wetu unatokana na hali kwamba Rais Samia hana mamlaka wala ukubalifu wa kisheria kufanya hivyo. Alijilazimisha kuwa rais kupitia mchakato usio huru, haki na uliokosa uwazi wala kufuata misingi ya kidemokrasia,” akasema.

Kando na Jaji Othman, tume hiyo inashirikisha wanachama wengine saba wenye tajriba katika nyanja ya sheria, diplomasia, usalama na uongozi.

Wao ni pamoja na; Profesa Ibrahim Juma, Balozi Ombeni Sefue, Balozi Radhia Msuya, Luteni Jenerali  Paul Meela, Inspekta Jenerali Mstaafu  Said Ally Mwema, balozi David Kapya na Dkt  Stergomena Tax.

Muda wa kuendesha shughuli zake na kuwasilisha ripoti yake haijawekwa.

Bw Heche alisema tume hiyo haitaendesha kazi zake kwa njia huru kwa sababu chini ya Sheria ya Tume za Kuendesha Chunguzi ya 2002, itafanyakaz kazi chini ya maagizo na uelekezi wa Rais.

“Rais yuko na mamlaka ya kuamua ikiwa ripoti ya tume hiyo itachapishwa au kudumazwa, ikiwa itatolewa kwa umma au itafichwa. Hii ina maana kuwa tume hiyo haiwezi kuwa huru haswa katika hali ambapo serikali ndiyo mshukiwa mkuu wa uhalifu unaochunguzwa,” akasema.

Bw Heche aliongeza kuwa uanachama wa tume hiyo unashirikisha maafisa wa serikali au wanachama wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wamekuwa watendaji katika machafuko hayo, wengine wakidaiwa kuhusishwa katika vitendo vya ukiukaji haki.

Chadema sasa kinapendekeza maovu hayo yachunguzwe na asasi ya kimataifa ambayo haitatishwa wala kuingiliwa na Serikali ya Tanzania.

“Tunasisitiza kuundwe Tume Huru ya Kimataifa, yenye uwezo, utaalamu, mamlaka na ukubalifu, kuendesha uchaguzi huru kuhusu vitendo vya mauaji, uhalifu dhidi ya binadamu na ukiukaji wa haki vilivyotendeka chini ya usimamizi wa utawala wa Samia Suluhu Hassan,” chama hicho kikaeleza.