CHAKISI; Bakora mwafaka dhidi ya matokeo butu ya Kiswahili Shuleni Isibania
Na CHRIS ADUNGO
CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Isibania (CHAKISI) kilianzishwa rasmi na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni humo, Bw Nicodemus Matara mnamo 2015.
Tangu wakati huo, chama kimepata mashiko na kuwafanya wengi kukichapukia Kiswahili kwa ufasaha.
Kwa hakika chama hiki kimethibitisha kuwa bakora bora dhidi ya matokeo mabaya yaliyochangiwa na mtazamo hasi kuwa Kiswahili ni somo gumu miongoni mwa wanafunzi kutoka gatuzi la Migori.
CHAKISI kimekuwa mlezi wa matokeo bora miongoni mwa wanachama katika Kiswahili, somo ambalo kwa sasa linachangamkiwa pakubwa hata na wanafunzi ambao si wanachama.
Kwa sasa, wanachama wa CHAKISI ambao ni wanafunzi wa Kidato cha Nne wanatarajia kufanya vizuri katika mtihani wa KCSE Kiswahili mwaka 2019.
Chama kipo chini ya ulezi wa Bi Adelide Agosa ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni Isibania. Bi Agosa anashirikiana na walimu Jacktone Kisa, Machuma Simba, Jacob Mwita Rose Robi, Noah Merengo na Eric Juma kuendeleza gurudumu la Kiswahili katika kuboresha na kuimarisha Kiswahili shuleni Isibania.
Walimu hawa wamekuwa mhimili mkubwa katika kuchangia maendeleo ya chama kwa kuwatia shime wanachama pamoja na kuendeleza ufundishaji wa Kiswahili hadi kufikia upeo wake.
Lugha ashirafu
Ufunzaji huo tayari umetambuliwa na kupongezwa na Mwalimu Mkuu, Bw Thomas Boke ambaye yuko mstari wa mbele kuendeleza lugha hii ashirafu kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Naibu wake, Bw Thomas Obola.
Chama kinajivunia zaidi ya wanachama 90 ambao wamejisajili rasmi. Hawa hujitolea kwa hali na mali kuendeleza shughuli zote za chama ndani na nje ya Shule ya Upili ya Isibania Boys.
Wanachama hupania kukutana kila siku ya Jumatano kuanzia saa kumi kamili za jioni katika mojawapo ya madarasa shuleni. Wakutanapo, wanachama hufaidi pakubwa kutokana na mijadala mipevu ya Kiswahili kuhusu masuala ibuka na teknolojia, maswali tatanishi waliyokumbuna nayo madarasani kwa wiki nzima, kutuza aliyejibu kwa usahihi swali la wiki, uwasilishaji wa mashairi na kuandaa mikakati ya kuimarisha maendeleo ya chama na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Mbali na kukuza vipawa vya utunzi wa kazi za kibunifu na sanaa ya ulumbi miongoni mwa wanafunzi kwa lengo la kuwatayarisha kuwa viongozi wenye uwezo wa kuwasiliana ipasavyo kwa Kiswahili safi, CHAKISI vilevile kinazidi kuwa chemchemi inayowapa wanafunzi fursa yaa kuendesha midahalo wazi na kuangazia masuala mbalimbali yanayofungamana na maendeleo ya jamii.
Wanachama wanajitahidi pia kutumia misamiati mwafaka ya Kiswahili katika kuelezea dhana zenye utata miongoni mwa watumiaji wa lugha hiyo.
Ikumbukwe kwamba Uzungumzaji na Usikilizaji ni kati ya stadi ambazo wanafunzi huzihitaji sana ili kuendesha mijadala yao kwa ufasaha na mantiki.
Vinara wa chama kwa sasa wana mipango ya kupata uanachama wa kila mwanafunzi shuleni hasa ikizingatiwa kwamba Kiswahili ni somo la lazima na la kutahiniwa katika KCSE.
Kwa miaka michache ambayo chama kimekuwapo, wanafunzi wameonyesha ari kubwa ya kukichapukia Kiswahili vilivyo.