Chama kinaweza kuimarisha au kuvunja ndoa yako
KATIKA jamii nyingi za leo, hasa miongoni mwa wanawake, chama au merry-go-round kimekuwa sehemu muhimu ya maisha. Wanawake hukutana mara moja au mbili kwa mwezi, kuchanga pesa kwa ajili ya miradi, mikopo midogo au kusaidiana wakati wa janga.
Hata hivyo, ingawa vyama hivi vimeleta maendeleo kwa wengi, pia vimegeuka chanzo cha migogoro katika ndoa nyingi.
Baadhi ya wanaume hulalamika kuwa wake zao wamezama katika masuala ya chama kiasi cha kusahau majukumu ya kifamilia.
Kuna wanaojihusisha na mikutano hadi usiku au safari za “shughuli ya chama” bila kueleza kwa uwazi kinachoendelea.
Wengine hutumia fedha za nyumbani kuwekeza katika chama bila kumshirikisha mwenzake jambo linaloleta kutoaminiana na migogoro ya kifedha.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wanawake wanasema chama ni njia ya kujikomboa kifedha na kisaikolojia.
“Kabla ya kujiunga na chama, nilimtegemea mume wangu kwa kila kitu.
Sasa ninaweza kuchangia kodi, chakula na hata akiba yangu mwenyewe,” anasema Bi. Jane Achieng’, mwanachama wa kikundi cha Akina Mama Umoja.
Hata hivyo, anakiri kuwa ilibidi aweke mipaka ili ndoa yake isivurugike.
Grace Nyawira, mataalamu wa masuala ya ndoa anasema tatizo si chama chenyewe, bali ukosefu wa mawasiliano kati ya wanandoa.
“Chama kinakuwa tatizo pale mmoja anapofanya maamuzi ya kifedha kisiri au kutumia muda mwingi na wanachama wenzake kuliko familia.
Kuna haja wanandoa waweke mipaka na wawe wazi,” anasema Bi Grace.
Kuna pia visa ambapo chama kinakuwa uwanja wa ushawishi mbaya.
Baadhi ya wanachama huanza kulinganisha maisha yao na ya wengine, wakitaka magari, mavazi au likizo wanazoziona kwa wenzao. Matokeo yake ni msukumo wa kutumia zaidi ya kipato na hatimaye migogoro ya kifamilia.
Hata hivyo, chama kinaweza kuwa nguvu chanya endapo kitaendeshwa kwa nidhamu. Wanandoa wanaweza kushirikiana kuanzisha chama cha pamoja au kuweka utaratibu wa kushirikishana habari za kifedha.
Kwa mfano, mke anaweza kumwonyesha mume wake faida na changamoto za chama, ili wawiane katika malengo ya kifamilia
Kwa jumla, chama si adui wa ndoa.
Ni chombo cha maendeleo kinachoweza kusaidia familia ikiwa kuna uaminifu, mipango na mawasiliano ya wazi. Lakini kikitumika vibaya, kinaweza kuwa chanzo cha mgawanyiko, kutoaminiana na hata kuvunjika kwa ndoa.