CONSOLATA KAMAU: Produsa, mwelekezi wa filamu, mwandishi na msanii
Na JOHN KIMWERE
NI miongoni mwa wasanii wachache wa kike ambao wameamua kujituma kwa udi na uvumba kuvumisha tasnia ya filamu nchini. Ni taaluma aliyoanza kushiriki tangu akiwa mwanafunzi wa darasa la tatu. Muda huo alianza kushiriki kwenye kipindi kilichoitwa Rambo Bamboo buy kilichokuwa kinapeperushwa kupitia runinga ya KBC.
Ukweli wa mambo ni kuwa wahenga hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa walivyolonga kwamba ‘Vitu vya biashara havigombani.’
Katika mpango mzima ni mwigizaji anayejivunia kushiriki filamu nyingi tu tangia mwaka 2011 alipoanza kushiriki kipindi cha Vionja mahakamani. Msanii huyu ameshiriki filamu ambazo zimefaulu kuonyesha kupitia runinga kadhaa ikiwamo KTN Burudani na Capuchin TV.
Consolata Bahati Kamau (37) maarufu kama Inspekta Zena amevalia kofia nyingi tu katika tasnia ya uigizaji. Mwigizaji huyu ni produsa, mwelekezi wa filamu, mwandishi, msanii wa mapambo, mfanyibiashara, msanii wa nyimbo za injili pia anaamiliki brandi ya kuzalisha filamu bila kusahau studio ya kurekodi muziki. Pia ameanzisha runinga ya mtandaoni inayojulikana kama Zenawood TV.
”Bila kujipigia debe ninajivunia kushiriki filamu nyingi maana ni talanta iliyogundua tangu utotoni mwangu,” alisema na kuongeza kwamba analenga kufikia kiwango cha filamu za haiba ya juu kama Nollywood.
Hata hivyo anasema alivutiwa kuendeleza talanta yake katika masuala ya maigizo alipotazama filamu iitwayo ‘Trouble maker’ ya mwigizaji mahiri wa filamu za Kinigeria (Nollywood) Patience Ozokwor maarufu Mama G.
Kando na kushiriki kipindi cha Vioja mahakamani pia ameshiriki filamu zingine ikiwamo ‘Hila,’ ‘Angels Diary,’ zote za KCB bila kuweka katika kaburi la sahau kipindi cha ‘chini ya mnazi’ kilichopeperushwa kupitia runinga ya Ken TV.
BRANDI
Chini ya brandi yake aliyoanzisha mwaka 2014 inayojulikana kama Bahati Zenawood Production msanii huyu amezalisha filamu kadhaa kama ‘Mke sumu,’ ‘Misukosuko,’ zote zilionyeshwa kupitia runinga ya Capuchin TV. Pia amekuwa akiandaa kipindi cha nyimbo za kiafrika cha Afrika Mobimba ambacho kimekuwa kikipeperushwa kupitia runinga hiyo.
Pia ndiye aliyezalisha filamu iitwayo ‘House of commotion’ (KTN Burudani). ”Vile vile nimezalisha filamu kama ‘Masaibu’ ambayo hupeperushwa kupitia runinga yangu,” alisema na kuongeza kwamba pia ipo filamu kwa jina ‘Afande zena,’ ambayo haijaonyeshwa popote.
Dada huyu anasema ndani ya miaka mitano ijayo ana imani tosha atakuwa amepiga hatua kubwa katika kampuni yake hasa kuzalisha filamu nyingi zitakaokuwa zikipeperushwa kwenye runinga. Anadokeza kwamba wasanii wengi tu watakuwa wamefaidi kupitia kampuni yake. Studio yake ya muziki inayojulikana kama Green Studio inayopatikana eneo la Uthiru.
MUZIKI
Kama msanii wa injili anajivunia kutoa albamu mbili ‘Chakacha ya Yesu,’ na ‘Napiga vita,’ zenye nyimbo sita kila moja. Muziki wake unapatikana kupitia mtandao wa kijamii wa Youtube.
Anatoa mwito kwa serikali iune mkono kikamilifu tasnia ya filamu nchini ili kuokoa vijana wengi wenye talanta hasa kuwaepusha dhidi ya kujiunga na makundi ya uhalifu mitaani.