'Corona ilinisukuma kugeuza shule yangu vyumba vya kilimobiashara'
NA MWANGI MUIRURI
BAADA ya kufundisha wanafunzi wa shule za msingi nchini kwa miaka 21, James Kung’u aliamua kugura kutoka ajira ya serikali mwaka wa 1998 akilenga kuzindua shule yake binafsi.
Alikuwa na matumaini makuu kwamba akizindua uwekezaji katika safu ambayo alikuwa na tajiriba ya miaka mingi haungemwaibisha kwa pato na akiwa na yale marupurupu ya kustaafu ya kima cha Sh362,000 na akiba ya Sh1 milioni, akapata motisha kujitosa kwa biashara ya elimu.
Katika taaluma yake ya ualimu, Bw Kung’u alikuwa amejinunulia ekari saba za shamba katika mji wa Ngurubani kando mwa barabara kuu ya kutoka Makutano hadi Embu, Kaunti ya Kirinyaga.
Hapa ndipo alijenga vyumba vya kwanza akitumia mabati na mbao na kisha akazindua shule yake ya msingi inayofahamika kama Roka (Reliable Organisation of Knowledge Acquisition) akiwa na wanafunzi 17 wa kufungua kazi.
Kwa sasa, shule hiyo ya jinsia zote mbili na pia ikiwa ya mseto ambapo iko na mrengo wa mabweni na wale wa kusoma wakirejea manyumbani mwao imegeuka kuwa na majengo ya kifahari na ambapo magari ya shule kwa sasa ni 10 yakiwemo mabasi mawili, madogo manne na malori mawili na madogo (pickups) mawili.
Hakuwa amenoa alipoafikia uamuzi wa kuwekeza katika safu ambayo alikuwa na ujuzi kwa kuwa shule hii ilipaa akisema kuwa Mungu aliibariki kwa kuafikia matokeo mema ya mtihani katika kipindi cha miaka 23 ambayo imekuwa ikitoa huduma.
Anasema kuwa alikuwa na wanafunzi 530 kufikia Machi 2020 “lakini huo ndio mwezi ibilisi mwenyewe alitembelea uwekezaji wangu.”
Anasema kuwa ibilisi huyo alikuwa amefika nchini Kenya kwa ziara zake za ukatili na akapitia kwake shuleni.
“Ibilisi huyo ni janga la Covid-19 ambalo mwezi huo wa Machi lilimsukuma Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kufungwa kwa taasisi zote za kielimu, shule yangu ikiwemo ndani ya amri hiyo,” asema.
Kabla ya janga hili kumfikia, anasema kuwa shule yake ilikiuwa ikimpa faida ya mamilioni kwa mwaka na ndiyo sababu taharuki ilimwingia kujipata akiagizwa afunge milango ya uwekezaji huu.
“Maisha yalinigeuka kuwa ya kuhangaika kimawazo. Nilikuwa na mkopo wa Sh2.4 Milioni na ambao mdhamini alikuwa wanafunzi hawa ambao sikuwa na budi ila tu kuwaambia waondoke shuleni. Nilipowaona wakiondoka, na nikahakikisha kuwa wa mwisho alikuwa ameondoka, ule upungufu wa ujasiri rohoni ulinihepa na ni vile tu mimi ni Mwaafrika wa kiburi halisi ambaye huamini wanaume hawafai kulia…nilitaka sana kulia, tena kwa sauti!” asema.
Uchungu zaidi ulimwingia rohoni kuona wafanyakazi wake 31 ambao walikuwa wamesaidia kuafikia makubwa ya shule yake wakiondoka kutoka manyumba ya shule hiyo mwezi wa Mei.
“Niliwalipa kwa miezi miwili zaidi tukingoja kurejelea kwa ratiba ya masomo. Lakini Mwezi wa Mei ikawa dhahiri kuwa huyu Ibilisi wa Covid-19 alikuwa mgeni asiye na adabu kabisa na hakuwa na haraka ya kujitoa hapa nchini,” asema.
Anasema kuwa mshahara wa wafanyakazi hao ulikuwa Sh290, 000 kwa mwezi na hangeweza kuendelea kulipa bila pato kutoka kwa ulipaji karo ya wanafunzi.
Anasema kuwa wazazi walitoa watoto wao shuleni wakiwa na malimbikizi ya kuchelewa ulipaji karo ya kima cha Sh6Milioni.
“Kwa ujumla, uwekezaji wangu ambao nilikuwa nimeujenga hadi kuafikia utajiri wa Sh800 milioni ukijumuisha thamani ya shamba, majengo, biashara na uwekezaji mwingine kama wa manyumba ya kukodisha ndani ya shamba hili langu la ekari saba, ukawa katika hatari ya kuyeyuka kama hewa yambisi!” asema.
Katika taharuki ambayo ilimkamba, Bw Kung’u ambaye ni wa sita katika familia ya watoto 12 ambapo babake mzazi kwa sasa ako na miaka 106, aliazimia kuuza biashara hiyo yake.
“Lakini nani angeinunua kukiwa na janga hili la Covid-19 na ambalo hakukuwa na uhakika wa tarehe ya ufunguzi? Lakini mimi wa mahangaiko haya ya sasa nikakumbuka jinsi nilivyohangaika nikiwa mtoto mchanga katika lindi la umasikini…ambapo hata nilipokuwa shuleni ilibidi niwe nikifanya vibarua ndio nipate karo…mimi hapa ambaye hata kwa wakati mmoja nilihudumu kama yaya na shambaboi ndio niopate chakula na karo,” asema.
Asema aliamua kuwa katika maisha yake yote hadi sasa hakuwa amekumbatia injili ya kupoteza matumaini na ndipo mawazo yake yalithibitika na akaanza kufikiria kuhusu jinsi ya kujinusuru kifedha.
Anasema kuwa alikuwa na mkopo mwingine wa benki wa Sh8 milioni na ombi lingine la mkopo wa Sh23 Milioni alionuia kuwekeza katika ujenzi wa manyumba zaidi ya upangaji.
“Kitu cha kwanza nilifanya baada ya kupata ulainifu wangu wa kimawazo kilikuwa kukimbia katika benki iliyokuwa ikinikopesha na nikaomba likizo ya ulipaji mikopo yangu. Nikapewa likizo ya miaka miwili. Kisha nkikasimamisha ule mkopo wa Sh23 Milioni ndio nipungukiwe na mzigo wa kifedha,” asema.
Lakini ndani ya ubongo wake alikuwa na ufahamu wa masuala mawili nyeti; “Kusimamishiwa ulipaji madeni yangu kwa muda sio kusamehewa na pia ni lazima maisha yangu yangeendelea mbele.”
Katika hali hizo mbili, aligundua kuwa ni lazima angebakia katika pato ili alipie mikopo yake na pia afadhili maisha yake ya kila siku.
Aliamua kuwa mkulima lakini shamba la kutekelezea kilimobiashara liko wapi ilihali ekari zote saba zilikuwa zimejaa mijengo?
“Madarasa yakageuka kuwa ya kufugia kuku na ambapo kwa sasa niko na kuku 2, 000 wa kutaga na 1, 500 wa nyama! Uwanja wa shule nikaugeuza kuwa kuwa shamba la mboga na matunda huku uwanja wa mikutano ukigeuka kuwa wa kilimo cha mahindi na Miciiri! Dimwbi la shule la watoto kuogelea la dhamani ya Sh15 Milioni nikaligeuza kuwa hifadhi ya maji ya unyunyiziaji!” afichua.
Leo hii anasema kuwa ingawa pato lake la kilimo haliwezi likalinganishwa kamwe na lile la shule, ako na raha kuwa analipia mikopo yake kwa urahisi na pia maisha yake yameendelea kunoga kwa raha ya pesa. Anasema hakungoja ile likizo ya miaka miwili ndio aanze kiulipioa mikopo yake bali aliamua kujitoa kitanzi hicho cha kifedha shingoni mapema.
“Kwa siku moja sasa kwa kuwa ndio nimeanza kupenya sokoni ninaweza kupata Sh70, 000. Pato hilo litapanda jinsi kilimobiashara changu kinogavyo…Nikiwa na umri wa miaka 69 kwa sasa, sina stresi za kimaisha na nimegundua kuwa uwekezaji wowote ule hauna uhakika wa kudumu kama yunavyoshuhudia Covid-19 ikibomoa hata biashara za jadi,” asema.
Pia, anasema kuwa amekuja kueleewa kuwa pato lolote lile ni sawa bora linakupa raha na utulivu.
“Nimekuja kueleewa hakuna pesa kubwa na pesa ndogo. Zote ni sawa, cha maana kikiwa ni jinsi pato hilo linakupa raha,” asema.