DAU LA MAISHA: Ajizatiti kupunguza mapuuza ya vijana
Na PAULINE ONGAJI
KUNA msemo mmoja ambao asili yake haijulikani, kwamba, ukitaka kuficha kitu kisipatikane na Mwafrika, basi kibanze kwenye kitabu.
Dhana ya msemo huu ni kwamba kwa kawaida Waafrika hawapendi kusoma.
Ukweli wake bila shaka haujabainika, lakini dhana hii potovu ni mojawapo ya sababu zilizompa Esther Mwanyume, 23, mshawasha wa kutaka kukuza mazoea ya kusoma vitabu hasa miongoni mwa vijana.
Bi Mwanyume anafanya hivi kama mbinu ya kunasua kizazi hiki kutokana na minyororo ya mapuuza, jambo ambalo asema limekuwa kizingiti cha maendeleo na chanzo cha utovu wa maadili.
“Elimu ni nguvu na kusoma ni sawa na kuwa na ufahamu wa mambo yanayokuzingira. Ukisoma vitabu unafahamu mambo mengi ambayo yaweza kukuongoza na kukuepusha na majanga baadaye maishani. Aidha, kulingana na tafiti kadhaa za kisayansi, kusoma vitabu kumeonekana kuuchangamsha ubongo na hivyo kuimarisha uwezo wa mtu kufikiria,” aeleza.
Kulingana naye, kusoma kunakupa nguvu za kujua mambo ambayo huenda haungejifunza ukiwa darasani. Ni ujumbe ambao ameueneza katika sehemu mbalimbali eneo la Pwani huku akilenga watu tofauti. “Nimekuwa nikilenga hasa vijana na watoto, bali na marafiki zangu,” asema.
Ni jitihada ambazo japo hazijamshindia tuzo, zimemvunia sifa na utambuzi mwingi katika jamii. Na ushauri na himizo la kusoma sio tu kwa watu wengine, kwani hata yeye ni mfano mwema huku kufikia sasa tangu mwaka uanze, anasoma kitabu chake cha tisa. “Nimejiwekea shabaha la kusoma angaa vitabu vitatu kila mwezi,” aeleza.
Isitoshe, mapema mwezi huu, alikuwa miongoni mwa waandishi 15 kutoka sehemu mbalimbali nchini waliozindua kitabu Kaskazi, walichoandika kwa ushirika.
Ndoto yake ya kutaka kujihusisha na mradi wa kuimarisha masomo katika jamii ilianza akiwa angali mtoto mdogo. “Tangu utotoni nilifurahia sana kusoma ambapo nilipata kichocheo kutoka kwa babangu ambaye pia alikuwa mpenzi wa vitabu. Nakumbuka alikuwa na mkusanyiko wa vitabu tofauti ambapo mara kwa mara angenihimiza kusoma, na hata wakati mwingine kunitafutia makala gazetini ili niyasome,” aeleza.
Ni penzi aliloliendeleza hata akiwa mwanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Coast Girls. Lakini, ari yake ya kutaka kujihusisha na masomo ilishika kasi akiwa katika chuo kikuu alipokuwa akisomea masuala ya usimamizi wa kibiashara.
“Ni wakati huu ambapo penzi hili lilichochewa kwani nikiwa chuoni nilikumbana na kikundi cha Writers Guild Kenya, ambacho kilikuwa kikiwahimiza watu kusoma na kuandika. Niliungana nao na chama hiki kilipozindua tawi jijini Mombasa ili kuwakilisha eneo la Pwani, niliona hii kama fursa ya kukuza tabia hii eneo hili,” aeleza.
Lakini haijakuwa rahisi kwake Bi Mwanyume huku akikumbana na changamoto mbalimbali.
“Sio rahisi kushawishi watu kusoma ilhali wao pia wanakumbwa na changamoto za maishani. Ni vigumu kumshawishi mtu kusoma ilhali anahitaji chakula. Aidha, kuna wale ambao kila unapowazungumzia kuhusu umuhimu wa kusoma vitabu, wanaona kana kwamba unawakera,” aeleza.
Hata hivyo ni matatizo ambayo anasema japo mara kwa mara yamepunguza kasi yake katika mwito huu, kamwe hayajazima azma yake ya kuendeleza ujumbe huu hata katika sehemu mbalimbali nchini.
Kwa sasa ndoto yake ni kuhakikisha kwamba anaeneza ujumbe huu sio tu katika sehemu zingine eneo la Pwani, bali pia nchini kote. “Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, anapanga kufikia watu zaidi, na hivyo kukuza kizazi kinachoelewa umuhimu wa kusoma vitabu katika siku zijazo,” aongeza.