Makala

DAU LA MAISHA: Anapalilia talanta za watoto wadogo

July 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KULINGANA na tafiti nyingi, vipaji vingi hutambulika mtoto akiwa katika umri mdogo

Hii ni sababu kuu ambayo imemshinikiza Venessa Micere, 31, kujitwika jukumu la kutambua vipaji vya watoto wakiwa bado katika shule za msingi.

Kwa miaka miwili sasa amekuwa akifanya shughuli za kutambua vipaji vya watoto eneo la Kirinyaga huku akinuia kuwaandaa katika maisha ya baadaye.

Shughuli hii amekuwa akiiendesha kupitia mradi alioanzisha wa TalentsAndPotential TAPKidsAfrica, ulio chini ya Talent Acquisition Program huku akijitambua kama mjumbe wa kukuza talanta za watoto.

Hasa shughuli hii inahusisha kutoa mafunzo ya ujuzi tofauti kama vile kusema mbele ya umma, uanamitindo, uigizaji, uchezaji densi na spoti miongoni mwa mambo mengine.

“Utagundua kwamba kuna watoto ambao licha ya kuanza kuonyesha vipaji vyao mapema, hawapati usaidizi unaofaa kutoka kwa walimu au wazazi wao, suala linalowafanya kuvipoteza baadaye maishani,” aeleza.

Kulingana na Bi Micere, mafunzo haya pia yanahusisha mambo mengine kama vile kuwapa ujuzi wa jinsi ya kujithamini, kujali maslahi ya wengine na kuwa na maadili mema.

Mchango wake unatambulika hasa miongoni mwa walimu katika sehemu hii, suala ambalo limemwezesha kupeleka shughuli hii katika shule mbalimbali katika Kaunti hii.

“Nimezuru shule kama Kerugoya Municipality, Skylimit Academy, All Saints Academy na Kabare Boarding Primary. Katika harakati hizi nafurahi kwamba mamia ya wanafunzi wamenufaika kutokana na mafunzo haya,” aeleza.

Ari ya kuanzisha mradi huu ilitokana na kiu ya kutaka kusaidia watoto kutambua uwezo wao sio tu kimasomo bali pia kulingana na vipaji walivyo navyo.

Nia yake ilikuwa kubadilisha mtazamo sio tu wa wanafunzi, bali pia walimu na hata wazazi kwamba sio masomo pekee yanayoweza kumsaidia mwanafunzi kufanya vyema maishani.

“Msukumo wangu mkuu ulikuwa kupanua mawazo ya watoto, walimu na wazazi kwamba japo masomo ni muhimu sana, watoto wanapoendelea kusoma, vipaji walivyozaliwa navyo havipaswi kupuuzwa, na badala yake vinafaa kutambuliwa na kupaliliwa,” aeleza.

Amekuwa akifanya haya kwa ushirikiano na shule za msingi ambapo pamoja na walimu wanatafuta mbinu mwafaka kutekeleza mtaala huu mpya wa umilisi (Competence Based Curriculum).

“Tuko katika harakati za mashauriano na shule mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mtaala wa umilisi. Tunafanya hivyo kwa kuandaa maonyesho ya vipaji na kuunda uhusiano na wadau,” aeleza.

Miradi ya manufaa

Mbali na hayo, pia wameanzisha miradi ya kuleta manufaa kwa jamii.

Mwaka 2019 wameshirikiana na shirika la uhifadhi wa mazingira chini ya dhamira, Trees, Food & Books, na katika harakati hizo kutembelea shule za msingi za umma na kushiriki katika shughuli za upanzi wa miti na uzinduzi wa maktaba.

“Tangu mwanzo wa mwaka huu tumepanda miti na kufungua maktaba katika shule za msingi za Kahiro, Ikulungu na Kiabarikiri,” aeleza.

Kwa sasa TAPKidsAfrica imeandaa ziara ya kipindi cha mwaka 2019 – 2020 ambapo wananuia kuzuru maeneo mbalimbali katika eneo la Mlima Kenya.

“Pia, baadaye tunapania kupanua shughuli hizi ili kuhusisha mataifa mengine barani Afrika,” asema.