Makala

DAU LA MAISHA: Bidii yake yatambuliwa kazini

May 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA umri wa miaka 33 pekee, yeye ni meneja mkurugenzi wa VAELL Kenya, mojawapo ya mashirika makuu ya kukodisha bidhaa (Leasing) katika eneo la Afrika Mashariki na ya Kati.

Ni wadhifa ambao Bertha Mvati, 33, ameshikilia tangu mwezi Machi 2019, huku akiwa mfanyakazi wa kwanza wa kike mwenye umri mdogo kuwahi kuchukua nafasi hiyo.

Katika wadhifa huo Bi Mvati anashughulikia utekelezaji wa mikakati, kutoa suluhu za kifedha kwa wateja na mali zao ambapo kwa sasa anasimamia matawi kumi ya shirika hili huku takriban wafanyakazi 100 wakiwa chini yake.

“Nina uzoefu wa takriban miaka kumi katika masuala ya ukodishaji mali nchini Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda,” aongeza.

Bi Mvati amechangia pakubwa katika shirika hili kiasi kuwa katika kipindi cha miaka kumi kwenye nyadhifa mbalimbali, amewezesha kampuni hii kukua hasa ikizingatiwa kwamba alipojiiunga nayo ilikuwa na wafanyakazi kumi pakee.

Kwa sababu ya jitihada zake, kwa ushirikiano na wafanyakzi wengine katika shirika hili wamewezesha kampuni hii kushinda tuzo sita katika kipindi cha miaka 15 iliyopita ambapo hivi majuzi walitajwa kama kampuni bora ya kutoa huduma katika eneo la Afrika Mashariki.

Safari yake katika sekta hii ilianza Januari 2009 alipojiunga na idara ya mikopo ya shirika hili kama mwanafunzi ambapo alifanya kazi kwa miezi mitatu.

Baadaye alifanya kazi katika nyadhifa mbalimbali katika mashirika tanzu ya kampuni hii nchini Kenya na Uganda, kabla ya kuteuliwa katika wadhifa huu Machi 2019.

Kinachotia moyo zaidi ni kwamba kinyume na matarajio kwamba sharti uwe na kisomo cha juu ili kupata nafasi kubwa ya ajira, Bi Mvati amehudumu katika baadhi ya nyadhifa kuu akiwa na shahada ya diploma tu.

“Nilipojiunga na shirika hili sikuwa na shahada ya digrii ambapo nilijiendeleza kimasomo nikiwa katika shirika hili. Wakati huo, kampuni hii kupitia afisi ya Uganda ilinisaidia kusomea shahada ya digrii ya masuala ya Usimamizi wa Biashara na Fedha katika Chuo Kikuu cha Uganda Christian University ambapo kwa sasa nasomea shahada ya uzamili, vilevile masuala ya fedha,” aeleza.

Hii anasema kwamba haingewezekana pasi na usaidizi wa shirika hili.

“Nilipokuwa nikihudumu kama mwanafunzi nilibahatika kulipwa, pesa zilizoniwezesha kulipia gharama yangu ya mahitaji ya kila siku,” aongeza.

Hata hivyo, haimaanishi kwamba mambo yamekuwa rahisi kwa Bi Mvati kwani changamoto si haba amekumbana nazo.

“Kufanya kazi katika sekta hii haijakuwa rahisi hasa ikizingatiwa kwamba ingali mbichi hasa katika soko hili,” aeleza.

Lakini ni hali ambayo imemfanya kushamiri na kuimarika katika tasnia hii. “Ninafurahia kazi yangu na nina motisha wa kuhudumu kila wakati,” aeleza.

Wazazi

Ni maadili ambayo asema amejifunza kutoka kwa wazazi wake.

“Wazazi wangu walitia bidii kuhakikisha mimi na ndugu zangu tunapata elimu bora. Kushuhudia jinsi walivyokuwa wakitia bidii kulinifanya niendeelee kukua nikijua kwamba bidii inalipa,” asema

Aidha, anasema kwamba ufanisi wake umetokana na imani yake kuu.

“Wazazi wangu ni Wakristu na mamangu alikuwa mwalimu ambapo hivi viwili vilihakikisha kwamba anatutia adabu,” aeleza huku akiongeza kwamba usaidizi kutoka kwa mumewe pia umechangia ufanisi wake.

“Pia, Meneja Mkurugenzi mkuu wa VAELL, Paul Njeru vilevile mwenyekiti wa shirika hili Joseph Kiiza wamechangia pakubwa ufanisi wangu,” aeleza huku akiongeza kwamba ikiwa unataka kufanikiwa, basi sharti udumishe uhusiano mzuri na wakuu wako kazini.

Lakini ni unyenyekevu wake ambao umemwezesha kufanya kazi na kila mtu katika shirika hili, na hata kuenziwa na wenzake na hili anasema limechangia pakubwa kuinuka kwake.