• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
DAU LA MAISHA: Kajenga himaya ya biashara mtandaoni

DAU LA MAISHA: Kajenga himaya ya biashara mtandaoni

Na PAULINE ONGAJI

AGHALABU biashara ya uokaji huhusishwa na akina mama na ni watu wachache hudhani kwamba yaweza kuleta mavuno makubwa.

Lakini kwa Tamima Mohammed, 26, mambo ni tofauti kwani licha ya umri wake mdogo, anajiundia jina katika fani hii ambayo bado haijakumbatiwa vilivyo na wengi katika kizazi chake.

Alipojitosa katika biashara ya uokaji, hakujua kwamba miaka michache baadaye, angekuwa anashamiri na kutumika kama mfano kwa vijana wenzake.

Kwa sasa anahusika katika uokaji wa keki za kila aina na za hafla mbalimbali; iwe harusi au maadhimisho ya siku ya kuzaliwa miongoni mwa sherehe zingine.

Keki zake zote huokwa kulingana na maagizo ya wateja. “Kati ya Agosti na Desemba ambapo ni msimu wa kazi nyingi, mimi huoka takriban keki 15 kila mwezi ambapo bei yangu huwa kati ya Sh3, 000 na Sh4, 000 kwa kilo,” aeleza.

Kinachofanya bidhaa zake kuwa za kipekee ni ubunifu unaotokana na keki anazooka, huku mapambo anayoyaweka, yakimtenga na wengine katika biashara hii.

Hii leo, biashara yake kwa jina Tamima’s Tam Tam, ina zaidi ya wafuasi 8,000 kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

“Ubunifu wangu katika kuoka na kupamba keki hutokana na mambo ya kawaida yanayotendeka. Mara nyingi, huchochewa na filamu za katuni,” aeleza.

Bi Mohammed alizaliwa katika Kaunti ya Nakuru katika familia ambayo haikuwa na mapato mengi.

Uokaji haukuwa ndoto yake ya utotoni, azma yake ilikuwa kuwa mtangazaji na mjasiriamali kama babake.

“Baada ya kukamilisha masomo ya shule ya upili mwaka wa 2011, nilijiunga na chuo fulani ambapo nilisomea masuala ya mahusiano mema,” aeleza.

Lakini kutokana na matatizo ya kifedha, alilazimika kukatiza masomo yake hata kabla ya mwisho wa muhula wa kwanza.

“Nilirejea nyumbani na kuanza biashara ya kuuza vyakula ambapo nilikuwa nikitembeza vitafunio kama vile sambusa katika afisi mbalimbali,” aeleza.

Ni kazi ambayo aliifanya kwa takriban mwaka mmoja, lakini haikumletea faida nyingi.

“Baada ya muda fulani nilianza kukumbwa na matatizo ya kiafya ambapo daktari alinishauri nisiendelee kutumia jiko la makaa. Ni ushauri uliokatiza ghafla biashara yangu,” asema.

Huku akihisi kuchanganyikiwa, aliamua kuhamia kwa dadake jijini Nairobi, na ni hapa ndipo ndoto yake ya uokaji ilipong’oa nanga rasmi.

“Dadangu alikuwa akioka vyakula tu kujifurahisha. Lakini siku moja alitembelewa na wageni ambapo niliamua kuwaandalia keki. Mmoja wa wageni hao aliifurahia sana keki hiyo, licha ya kuwa yeye mwenyewe pia alikuwa muokaji,” aeleza.

Ni suala lililompa motisha na kumfanya aanze kujihusisha zaidi na kazi hii huku akishabikiwa vilivyo na dadake, ambaye pia alimfadhili.

“Nilikuwa naenda chumbani mwangu, kisha nazama kwenye mtandao wa YouTube, kupiga msasa ujuzi wangu,” asema.

Lakini bado hakuwa ameiva katika masuala ya kuweka bei kwenye bidhaa zake.

“Ni suala ambalo lilinifanya kwenda hasara kwani kuna nyakati ambapo gharama ya matumizi ingezidi faida,” akumbuka.

Hata hivyo, hakukata tamaa ambapo baada ya kutambua kwamba hakuwa anaunda faida, alianza kutafuta ushauri kutoka kwa waokaji wengine.

Kando na kutaka kupata ushauri kwa waliomtangulia, Bi Tamima anasema kwamba mojawapo ya mambo ambayo yamemwezesha kushamiri, ni moyo wake usiopoteza matumaini.

 

(Habari zaidi na Lilys Njeru)

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Msambao wa Kiswahili Uganda...

Ipoa yachunguza matukio ya maafisa kuwafyatulia risasi...

adminleo