Makala

DAU LA MAISHA: 'Kazi ni kazi, mradi wapata tonge la siku'

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KWA baadhi, kazi ya uendeshaji teksi haipaswi kufanywa na wanawake hasa kutokana na sababu za kiusalama.

Hasa unapozingatia uendeshaji teksi za Uber ambapo mara nyingi unatarajiwa kufanya kazi nyakati zisizo za kawaida na kuwahudumia wateja usio wafahamu, sio mabinti wengi wanaweza kuimudu.

Lakini Faridah Salim Khamis, 37, amejitosa mzimamzima bila wasiwasi na kwa miaka miwili sasa, hii ndiyo imekuwa ajira ambayo inawalisha wanawe watano.

Ni ajira ambayo mara nyingi imemlazimu kufanya kazi usiku wa manane kati ya saa saba na saa kumi na moja alfajiri.

“Kisha mimi huelekea nyumbani na kuwaandaa wanangu na kuwapeleka shuleni halafu narejea kazini hadi saa nne asubuhi,” aeleza Faridah.

Akitoka hapo hupeleka gari lake kusafishwa na kuelekea nyumbani tena kwa lepe la usingizi kabla ya kurejea kazini tena hadi saa kumi jioni.

“Baadaye, mimi huenda kuwachukua wanangu kutoka shuleni na kuelekea nyumbani kuwaandalia chajio huku wakifanya kazi zao za ziada, kabla ya sote kuelekea kulala na kusubiri masaa ya kazi kuanza,” asimulia.

Ni kazi aliyoanza miaka miwili iliyopita baada ya kupitia magumu maishani.

“Baada ya talaka yangu ya pili, niliachwa na watoto ambapo sikuwa na namna ila kujipa nguvu na kuendelea na maisha badala ya kusononeka,” asema.

Ni kazi anayoifanya kwa bidii na ukakamavu na imemwezesha kukidhi mahitaji yake pamoja na wanawe na hana majuto.

Lakini, kama ajira zingine kazi hii haikosi changamoto.

“Kama mtu mwingine yeyote, mimi hukumbwa na woga hasa ninaposikia visa vya wenzangu ambao wameshambuliwa wakiwa kazini, lakini hujikakamua tu na kujiweka mikononi mwa Mungu,” aeleza.

Huku akitoa mfano wa wakati mmoja alipojipata matatani, Bi Khamis anakiri kwamba haikuwa rahisi kwake kuzoea.

“Nikiwa bado mbichi katika kazi hii, kuna wakati kulikuwa na mgomo fulani na nikapata mteja. Hakukuwa na madereva wengi wa huduma hii siku hiyo. Nilipokea ombi kutoka kwa binti fulani na baada ya kukamilisha safari, ada yake ilikuwa imeongezeka na kuwa Sh4,000. Hakuelewa jinsi huduma hii inavyofanya kazi wakati kama huo ambapo wateja ni wengi na madereva ni wachache na nilipokuwa nikimwelezea, alinizaba kofi. Hata hivyo sikukasirika kwani nilimwelewa,” aeleza.

Hiyo tu ni mojawapo ya changamoto za usalama anazokumbana nazo, lakini anasema kwamba sio kila wakati anakubali kujiweka katika hali ya hatari.

“Kuna wakati ambapo nikihisi kana kwamba sehemu fulani sio salama, huvunja safari hiyo,” aeleza.

Kando na changamoto za usalama, analalamikia idadi kubwa ya watu wanaotoa huduma hii, suala ambalo limesababisha ushindani mkali.

“Wakati mwingine inakuwa vigumu kupata wateja na kufikisha shabaha kwani bei huwa ya chini, na hivyo sharti tufanye kazi masaa yasiyo ya kawaida angalau tupate tonge la siku,” aeleza.

Mbali na kuendesha teksi, pia anajihusisha na shughuli za maandalizi ya hafla na mapishi ili kuongeza pato.

Anawarai mabinti pia kujisakia riziki badala ya kusubiri vya bwerere.

“Ikiwa una mtu anayekutazamia, anza kufanya kazi. Pesa unazofanyia kazi huridhisha nafsi zikilinganishwa na unazopewa bure. Sio tu kazi ya aina hii, mradi waweza kufanya kazi nyingine ile, basi changamka,” aeleza.