DAU LA MAISHA: Si kazi ya kawaida ila inafaidi jamii pakubwa
Na PAULINE ONGAJI
AMEKUWA kimbilio la akina mama wengi wanaokumbwa na matatizo ya kunyonyesha baada ya kujifungua.
Kwa takriban mwongo mmoja sasa, Josephine Karoki, amekuwa akitoa mafunzo ya jinsi ya kunyonyesha; hasa kwa kina mama wanaokumbwa na matatizo haya baada ya kujifungua.
Ni kazi ambayo amekuwa akiifanya kupitia shirika aliloanzisha la HunySuckle Kenya Ltd.
Kupitia jukwaa hili anasaidia akina mama wanaonyoshesha kwa kuwapa mafunzo kuhusu mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mbinu za kuzalisha maziwa zaidi, lishe bora ili kuimarisha uzalishaji maziwa, na jinsi ya kumweka mtoto kwenye titi ili kuhakikisha kwamba ananyonya vilivyo na pasipo kumsababishia mama maumivu.
Aidha anawafunza kuhusu jinsi ya kukamua maziwa na kuyahifadhi kwa matumizi ya baadaye. “Pia, mafunzo yangu yanahusisha kuwahimiza wanaokumbwa na matatizo haya kwa kuwakumbusha kwamba shida hizi hazimaanishi kwamba wameshindwa na majukumu yao kama mama, suala linalowapunguzia mzongo wa mawazo,” asema.
Mara nyingi kazi yake inahitaji ushirikiano na madaktari wa watoto, wanajinakolojia na wataalamu wa lishe.
Kwa sasa wateja wake ni akina mama wenye mapato wastani ambapo yeye huwatembelea nyumbani huku mara nyingi wakielekezwa kwake na madaktari wa watoto. “Kwa wiki moja naweza kuhudumia kati ya wateja wawili au watatu ambapo ada ya ziara yangu huwa Sh5,000 kwa kila masaa mawili,” aeleza.
Lakini ni juhudi ambazo anatumai kuzipeleka katika hospitali za umma ambapo kupitia ushirikiano na Kenya Association for Breastfeeding, pamoja na wenzake, wanatumai kufikisha huduma hizi mashinani.
Jitihada zake zimemfanya kuidhinishwa kama kiongozi wa La Leche League International Afrika Mashariki na Kati. Shirika hili hutambua uanaharakati, elimu na mafunzo yanayohusiana na masuala ya unyonyeshaji.
Kupitia jukwaa hili atahitajika kuandaa mikutano miwili kila mwezi na kusaidia akina mama kujifunza kutoka kwa wenzao kuhusu masuala ya kunyonyesha.
Isitoshe, baadaye mwaka huu anatarajiwa kuhudhuria kongamano la Lactation Conference for Young Mothers nchini Uingereza, chini ya ufadhili wa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa UNICEF.
Ari yake katika fani hii ilianza baada ya yeye pia kukumbwa na matatizo ya kunyonyesha alipojifungua mwanawe wa kwanza. “Baada ya kumzaa mwanangu wa kwanza, nilikumbwa na matatizo yaliyosababisha chuchu zangu kukatika na kupata nyufa kutokana na jinsi nilivyokuwa nikimnyonyesha,” aeleza.
Japo jeraha hilo lilipona lenyewe, anasema kwamba ilimchukua muda mrefu kupata nafuu, tofauti na endapo angekuwa na ufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kumnyonyesha mwanawe.
Ni hapa aliamua kujitosa kikamilifu katika nyanja hii na kuanza kufanya utafiti zaidi, suala lililomfanya kuacha kazi katika idara ya uwakala katika kampuni moja ya kuunda pombe nchini, ili kupata mafunzo zaidi kuwaelimisha wanawake wenzake wanaokumbwa na matatizo hayo.
Ili kupata ufahamu wa kina katika nyanja hii ameshiriki mafunzo mbalimbali katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Lakini safari yake haijakuwa nywee kwani amekumbwa na changamoto kadha wa kadha. “Changamoto kuu imekuwa kuelezea umuhimu wa kazi ninayofanya sababu kuna watu wanaodhania haifai. Wengi wanachukulia kwamba ni kawaida kwa mama kujua jinsi ya kumnyonyesha mtoto anapozaliwa na hivyo hahitaji mafunzo wala ushauri,” aeleza.
Ni changamoto ambayo inafanya iwe vigumu kutoza ada ya huduma zake jinsi inavyostahili. “Kwa mfano pesa ninazopata mara nyingi hunisaidia kukidhi gharama za nauli. Hii ni tofauti kabisa na mataifa yaliyostawi ambapo huduma hii inatambuliwa kama taaluma yenye pato kubwa,” asema.
Licha ya changamoto hizi hata hivyo, anazidi kupambana akitumai kueneza huduma zake ili kuwafikia hata akina mama wenye mapato ya chini.