Makala

DAU LA MAISHA: Sio muuguzi ila wengi wapona kupitia kwake

August 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

ANAWAPA matumaini wanawake wanaokumbwa na Gigantomastia, hali isiyo ya kawaida ambapo matiti hukua kupindukia na wakati mwingine kufika hata tumboni.

Hii ni shughuli ambayo Ruth Makena amekuwa akiifanya kupitia Gigantomastia Foundation, wakfu alioanzisha mwaka wa 2015 kusaidia wanawake wanaokumbwa na hali ili kupata huduma ya kimatibabu kurekebisha kasoro hiyo.

Mradi huu hujishughulisha na kuhamasisha watu kuhusu hali hii. “Hapa, tunaelimisha umma jinsi ya kutambua ishara zinazoambatana na hali hii. Hii ni mbinu ya kuwasaidia wahusika kuelewa kwamba hili ni tatizo la kiafya na laweza kurekebishwa humu nchini,” aeleza.

Lakini jukumu lao kuu ni kuwasaidia wanaokumbwa na hali hii kupokea huduma ya matibabu ambayo huwa ni upasuaji ili kupunguza ukubwa wa matiti.

“Upasuaji huu ni ghali mno ambapo kwa mtu mmoja, gharama inaweza kufikia shilingi laki tano, pesa ambazo ni wachache sana wanaweza kumudu. Kwa hivyo jukumu letu ni kukusanya hizi fedha kupitia wahisani na washirika na kuhakikisha kwamba waathiriwa wanafanyiwa upasuaji huu,” aeleza.

Aidha, wanasaidia waathiriwa kukabiliana na unyanyapaa.

“Wasichana na wanawake wengi wanaokumbwa na hali hii huwa na woga wa kujitokeza hadharani ambapo sisi huwasaidia kupata ushauri nasaha,” asema.

Kufikia sasa zaidi ya wanawake 80 kutoka kaunti mbalimbali nchini wamenufaika kutokana na mradi huu na kurejeshewa uhuru wa kuvalia nguo zinazowapendeza na pia ujasiri wa kutembea bila woga.

Ili kuchagua wanawake wanaostahili usaidizi huu, wana vigezo wanavyofuata. “Kwanza kabisa lazima uwe na tatizo hili. Hii itadhihirishwa kwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kuhakikisha hali hii inakuletea matatizo ya kiafya kama vile kuumwa na mgongo na mabega,” anasema huku akisisitiza kwamba sharti wabaini kwamba hauna uwezo wa kifedha kumudu gharama ya matibabu.

Anafanya hivi kwa ushirikiano na washirika wengine. “Ushirikiano wetu ni pamoja na wataalamu wa kiafya, wakuu wa hospitali na madaktari wa upasuaji,” asema.

Ari yake ya kutaka kujihusisha na mradi huu ilianza miaka minane iliyopita baada ya yeye pia kutaabika na hali hii kwa muda mrefu.

“Kutokana na ukubwa wa sehemu hii, nilikuwa nakumbwa na majeraha ya mabega kila mara, kiasi cha kufanyiwa upasuaji mara mbili,” aeleza.

Lakini licha ya matatizo haya ya kiafya, hakutambua kwamba ni ukubwa wa matiti yake uliokuwa ukimletea matatizo haya. Hii ni hadi mwaka wa 2011 daktari aliyekuwa akimfanyia uchunguzi alipotambua tatizo hili na kumpendekezea upasuaji wa matiti.

“Nilifanyiwa upasuaji huu Februari mwaka huo,” aongeza.

Wakati huo, licha ya kwamba alikuwa chini ya mpango wa bima ya afya ya wazazi wake, haingeweza kugharimia upasuaji wake.

“Kulingana nao, licha ya matatizo ya kiafya niliyokumbana nayo kwa sababu ya hali hii, walihisi najitafutia starehe tu. Kwa hivyo, wazazi wangu walilazimika kulipia gharama ya takriban shilingi laki tano,” asimulia.

Gazetini

Baada ya hapo anasema kwamba hadithi yake ilichapishwa kwenye gazeti na watu wakaanza kumfuatilia sana wakitaka kujua mengi zaidi kuhusu hali hii, jambo ambalo awali halikuzungumziwa hadharani na hivyo akaona haja ya kuhamasisha watu.

Lakini ari kuu ilitokana na gharama ya juu ya utaratibu huo.

“Mimi nilikuwa na bahati kwa kuwa wazazi wangu waliweza kulipia utaratibu huu. Na je, wale ambao hawana uwezo wa kifedha watasaidika vipi?” anauliza.

Kwa sasa changamoto kuu asema ni ukosefu wa wafadhili wa kudumu, suala ambalo limeathiri shughuli za kuhakikisha wanawake zaidi wanafaidika.

Lakini licha ya matatizo haya, Bi Makena anasema kwamba hana nia ya kulegeza kamba. “Uwezo wa kuwarejeshea wasichana na wanawake ujasiri maishani na kujithamini pia, ni ridhisho tosha,” asema.