Makala

DAU LA MAISHA: Utunishaji misuli wampa tonge la siku

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

AMEITAMBULISHA Kenya katika ulimwengu wa utunishaji misuli kimataifa ambapo mapema mwezi huu alituzwa taji la bingwa wa Afrika kwa upande wa akina dada, katika hafla iliyoandaliwa nchini Angola.

Lakini hiyo sio tuzo ya kwanza kwa Evelyn Okinyi Owala.

Mei 2019 alitwaa tuzo ya uzani ya Arnold Classic Wellness. Pia ni yeye ndiye anashikilia taji la Miss Kenya Figure.

Lakini umaarufu wake hautokani tu na mataji haya, bali pia jitihada zake za kuhakikisha kwamba watu wanadumisha uzani unaowahakikishia afya njema.

Yeye pia ni mkufunzi wa mazoezi ambapo amekuwa akitoa huduma zake kupitia kampuni yake ya Eveal Health and Fitness. Hapa, huduma zake zinajumuisha mawaidha ya lishe, mazoezi na afya njema.

Ustadi wake katika nyanja hii umemzolea wateja sio tu humu nchini, bali pia katika mataifa ya ng’ambo. “Nina wateja wanaotoka sehemu za mbali kama vile Amerika, Uingereza, Australia na hata Vietnam,” aeleza.

Aidha, wateja wake ni kutoka jinsia na umri tofauti. “Wateja wangu wengi ni wanawake ambao huvutiwa na mwonekano wangu. Nimekutana na wanawake wanaotaka kujua nimwezaje kudumisha misuli thabiti ya tumbo na kama ujuavyo hii ni sehemu moja inayotuhangaisha sisi kina dada,” aongeza.

Anasema kwamba bei ya huduma zake huwa tofauti kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. “Hii ni kutokana na sababu kwamba watu hawafanani kimaumbo, kumaanisha kwamba kila mmoja ana mahitaji tofauti ya lishe na umbo ili kuweza kudumisha uzani unaofaa,” asema.

Alijitosa katika masuala ya mazoezi na uzani mwaka wa 2015 baada ya kuacha kazi katika benki.

“Lakini kabla ya kuacha kazi, nilikuwa bado najihusisha na mazoezi. Nakumbuka nyakati hizo nilichochea wafanyakazi wenzangu pia kufanya mazoezi, suala lililonifanya kutambuliwa kazini kwani ilionekana kama mbinu ya kudumisha afya njema, na hivyo kupunguza gharama ya matibabu,” aeleza.

Lakini pia ari yake ya ilichangiwa na hali ya kiafya aliyokuwa akikabiliana nayo iliyomlazimu kuingia katika ukumbi wa mazoezi.

“Aidha, mume wangu alikuwa akifanya mazoezi na hilo pia lilinichochea,” aongeza.

Lakini mwanzoni haikuwa rahisi kujitosa katika fani hii hasa wasiwasi mkubwa ukiwa kuwajulisha wazazi kuhusu uamuzi wa kuacha kazi. “Niliwajulisha miezi sita baada ya kukata kauli kuacha kazi,” aeleza.

Mtunishaji misuli Evelyn Okinyi Owala (kushoto). Picha/ Hisani

Mbali na hayo, changamoto nyingine ilikuwa jinsi ya kujitambulisha katika fani hii hasa ikizingatiwa kwamba hakuwa bado amejiundia jina, kumaanisha kwamba ingekuwa vigumu kupata wateja.

“Nilikuwa nimetenga pesa kununua vifaa vya mazoezi, lakini kwa bahati mbaya nikatapeliwa katika harakati hizi. Kwa hivyo nilikuwa natafuta jinsi ya kujitosa katika fani hii bila kutoboa mfuko zaidi,” asema.

Ili kujiundia jina, alihitaji kuonyesha uwezo wake, suala ambalo hangeweza afikia pasipo kuwa na mteja.

“Nakumbuka nilijitolea kumpa huduma ya bure bibi mmoja ili awe mfano wangu. Lakini kwa bahati nzuri, kutokana na sababu kuwa alifahamu jitihada zangu katika masuala ya mazoezi nikiwa ningali nahudumu katika benki, aliamua kunilipa,” aeleza.

Mteja apata matokeo mazuri

Baada ya miezi minne, mteja wake alipata matokeo mazuri sana kiasi cha kumpendekeza kwa wenzake, na ni hivyo alijiundia himaya ya wateja.

“Na tokea hapo nimekuwa nikitumia mbinu hii kupata wateja zaidi kwani huduma zangu hupendekezwa na wateja walioridhika na kazi yangu,” asema.

Bi Owala anasisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi na kudumisha uzani ufaao.

“Mbali na masuala ya kiafya, uzani unaofaa huongeza kiwango cha kujithamini.”