Makala

Dawa, chakula kupanda Mswada mpya ukipitishwa

Na Na Dominic Omondi May 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Watoaji wa huduma za afya na wakulima ni miongoni mwa watu watakaoathirika endapo pendekezo jipya la Wizara ya Fedha kuanzisha ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) wa asilimia 16 litapitishwa.

Kupitia Mswada wa Fedha wa mwaka 2025, Waziri wa Fedha John Mbadi anapendekeza kuondoa pembejeo na malighafi zinazotumika kutengeneza dawa na chakula cha mifugo, pamoja na usafirishaji wa miwa, kutoka  orodha ya bidhaa zisizotozwa VAT.

Bidhaa zisizotozwa VAT huwa na kiwango cha ushuru cha asilimia 0. Hii ina maana kuwa, tofauti na bidhaa ambazo zimeondolewa VAT, bado huzingatiwa kuwa bidhaa zinazotozwa kodi. Hata hivyo, biashara zinazojihusisha nazo bado zinaweza kudai  zirejeshewe ushuru wa pembejeo. Hivyo basi, hakuna VAT inayotozwa mteja wakati wa ununuzi.

Hata hivyo, katika marekebisho yaliyopendekezwa, Wizara ya Fedha imeondoa bidhaa hizi kutoka kwenye orodha ya bidhaa zisizotozwa VAT, jambo linalomaanisha kuwa wauzaji watalazimika kupitisha gharama hizo kwa wateja iwapo sheria hiyo itapitishwa. Hali hii huenda ikaongeza gharama ya chakula na huduma za afya.

Katika mabadiliko hayo, Wizara ya Fedha inataka Bunge kufuta vipengele nane vinavyohusu bidhaa zisizotozwa ushuru.

Serikali ya Rais William Ruto pia inaonekana kuachana na mipango ya matumizi ya magari ya umeme, huku Wizara ya Fedha ikipendekeza ushuru wa VAT wa asilimia 16 kwa mabasi ya umeme. Mpango wa mazingira pia utapata pigo baada ya serikali kupendekeza ushuru wa mauzo kwa betri za sola.

Usambazaji wa baiskeli za umeme pia umewekwa chini ya VAT ya asilimia 16 katika Mswada wa kwanza wa Fedha uliowasilishwa na Mbadi, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 kufuatia maandamano  ya vijana.

Utengenezaji na uunganishaji wa simu za mkononi pia umeondolewa kutoka orodha ya bidhaa zisizotozwa VAT.

Katika mabadiliko yaliyofanywa mwaka huu wa fedha kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kodi, serikali ilianzisha VAT kwa malighafi na pembejeo zinazotumika kutengeneza mbolea, hatua iliyoongeza gharama ya uzalishaji kwa wakulima.

Kwa kuwa bidhaa za kilimo ni muhimu katika uzalishaji wa mazao, serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiziondoa kwenye VAT ili kulinda watumiaji dhidi ya gharama kubwa za bidhaa za chakula.

Kwa Wakenya wengi, hasa maskini, chakula huchukua karibu nusu ya matumizi yao yote.

Mbolea na kemikali zilikuwa takribani nusu ya gharama ya jumla ya pembejeo za kilimo mwaka jana, kulingana na data ya Shirika la Takwimu la Taifa la Kenya (KNBS).