DCI yatii amri ya Ruto kukamata vijana walionaswa na CCTV wakiharibu na kuiba mali wakati wa maandamano
SIKU moja baada ya Rais William Ruto kutangaza kuwa wahuni waliopora na kuharibu mali wakati wa maandamano kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 watatiwa mbaroni, Idara ya Upelelezi na Uhalifu wa Jinai (DCI) imetii amri ya kiongozi wa nchi na kuanza oparesheni kukamata washukiwa.
Mswada huo tata, hata hivyo, Rais Ruto alikataa kuutia saini na badala yake kuufutilia mbali kutokana na fujo na ghasia zilizotawala maeneo mengi nchini.
Juma lililopita, maandamano hayo yaliyopangwa na vijana wa kizazi cha Gen Z yalikumbwa na uharibifu, majeraha na maafa ya zaidi ya watu 20.
Vijana walikataa mswada huo licha ya bunge kuufanyia marekebisho, wakitaka matakwa yao kuangaziwa.
Rais Ruto alilazimika kusalimu amri baada ya kushinikizwa asiutie saini.
DCI sasa inakiri kuwa vijana wa Gen Z waliandamana kwa amani kote nchini, lakini wahuni wakavuruga kwa kuharibia wanabiashara vyanzo vyao vya uchumi.
“Wakijifanya waandamanaji, watu wabaya waliojipanga walilenga maduka ya nguo, vifaa vya kielektroniki na maduka makuu wakayavunja na kuiba mali ya wanabiashara wasiokuwa na hatia,” DCI ilisema kupitia chapisho katika akaunti yake ya mtandao wa X (awali Twitter).
“Tumepata kanda nyingi za video za CCTV zilizonasa watu wanaoweza kutambuliwa kwa matendo yao mabaya ndani ya mamia ya maelfu ya watu waliojikita katika malengo yao (ya kuandamana),” DCI iliongeza.
Bila kutaja idadi, DCI ilieleza kuwa washukiwa kadhaa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Ilisema: “Tutawaondoa miongoni mwetu kwa manufaa ya wale ambao hawakufaa kupoteza njia zao za kipekee za kutega uchumi.”
Akisikitishwa na matokeo ya maandamano hayo ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, Rais Ruto alisema zaidi ya mali ya Sh 2.4 bilioni ziliharibiwa.
Akiwa kwenye kiti moto Ikuluni mnamo Juni 30, 2024 aliporushiwa maswali mazito na wahariri kutoka mashirika makuu ya habari nchini, Rais alibabaika alipotiwa lawamani polisi walipowakamata na kuwapiga waandamaji risasi kiholela.
Dkt Ruto alitetea polisi akisema walifuata sheria walipokuwa wanadhibiti waandamanaji.
Huku DCI wakiegemea CCTV kukamata washukiwa, Rais alipotakiwa kuelezea kuhusu polisi walionaswa na kanda zizo hizo wakipiga waandamanaji risasi alijibu wahariri; “Nyinyi mlikuwa hapo wakati wakifyatua risasi…”