Makala

DIMBA: Dominik Szoboszlai ni kiungo mchawi

October 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

DOMINIK Szoboszlai ni kiungo mshambuliaji aliyejaliwa kipaji cha kupasi mpira na pia ni ‘mchawi’ katika upigaji wa ikabu anayechezea klabu ya Red Bull Salzburg.

Klabu hii ndiyo ilikuza wachezaji matata wa Liverpool Sadio Mane na Naby Keita, na Erling Braut Haaland anayevumisha Borussia Dortmund.

Kinda huyo kutoka Hungary, ambaye anasherehekea siku moja ya kuzaliwa na nyota wa zamani wa Manchester City na Chelsea Shaun Wright-Phillips mnamo Oktoba 25, pia anafahamika kwa kasi ya juu, kuchapa kazi akiwa na presha na kufanya uamuzi mzuri mbele ya lango.

Dominik anafuata nyayo za Zsolt Szoboszlai, 45, ambaye ni babaye. Katika enzi yake, Zsolt alicheza soka ya malipo kama mshambuliaji na pia beki wa kupanda na kushuka nchini Hungary.

Zsolt, ambaye alijitosa katika ukocha akiwa bado mchezaji mwaka 2000, anasema Dominik alianza uchezaji wa soka akiwa na umri wa miaka mitano. Alimfanyisha mazoezi kwa muda wa jumla ya saa tano kila siku.

Dominik amekuwa akimezewa mate na klabu kutoka Ligi Tano-Bora barani Ulaya – La Liga (Uhispania), EPL (Uingereza), Serie A (Italia) Ligue 1 (Ufaransa) na Bundesliga (Ujerumani).

Kuna orodha ndefu ya klabu ambazo zimehusishwa naye zikiwemo Arsenal, Liverpool, Chelsea, Leicester, Juventus, Napoli, AC Milan, Lazio, Paris Saint-Germain, Dortmund na Bayern Munich.

Yeye ni mmoja wa wachezaji wakali kuwahi kutoka Hungary baada ya miongo kadhaa. Dominik, ambaye pia si mchache katika kuchenga wapinzani, anafananishwa na viungo matata Paul Pogba (Ufaransa na Manchester United) na Toni Kroos (Ujerumani na Real Madrid). Hata hivyo, wengi wanaona soka yake inakaribiana sana na ile ya Kroos, 30, na kiungo wa Serbia na klabu ya Lazio, Sergej Milinkovic-Savic, 25.

Tangu utotoni, Dominik amekuwa akijaribu kukuza soka yake kuwa kama ya mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Real Madrid Cristiano, 35, ambaye pia ni kielelezo kwake. Anafahamika kwa makombora makali ya kutoka mbali yanayosalia kumpa mshambuliaji wa Ureno na Juventus Cristiano Ronaldo umaarufu.

Dominik alizaliwa mjini Szekesfehervar nchini Hungary mwaka 2000. Ukuaji wake katika tasnia ya soka ulianzia katika akademia ya klabu ya mtaani mwake ya Videoton (inayofahamika sasa kama Fehevar FC) mwaka 2006. Kabla ya hapo, hata hivyo, babaye alinukuliwa akisema kuwa alimfundisha soka kuanzia umri wa miaka mitatu.

Kisha, alihamia Fonix-GOLD alikokuwa kutoka 2007 hadi 2015. Klabu hiyo pia ilimpeleka Ujpest kwa mkopo mwaka 2011. Alijiunga na MTK Budapest mwaka 2015 kabla ya mchezo wake wa kupendeza kuvutia maskauti wa Red Bull.

Mara kadhaa, Dominik alipelekwa katika timu ya Liefering inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili Austria, ambayo ni timu moja na Red Bull Salzburg. Alichezea Liefering mechi 42 na kufunga mabao 16 na kuchangia pasi 11 zilizofungwa.

Dominik alijiunga na Salzburg kwenye Ligi Kuu ya msimu 2017-2018 kwa Sh63.4 milioni, ingawa bado alitumiwa zaidi katika timu hiyo ya daraja ya pili.

Alijituma zaidi mazoezini na uwanjani na kujitokeza kuwa tegemeo chini ya kocha wa mabingwa hao wa Austria, Jesse Marsch.

Msimu wa 2018-2019, Dominik alisakata mechi 16 kwenye Ligi Kuu akiona lango mara tatu na kumega pasi nne zilizofungwa. Mambo yake yaliimarika msimu uliopita wa 2019-2020 pale alipotumiwa na Salzburg katika michuano 27 ligini akipachika mabao tisa na kumega pasi 14 zilizozalisha magoli.

Alishiriki mechi saba za mashindano ya Ulaya zikiwemo mechi mbili za makundi za Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya waliokuwa mabingwa Liverpool.

Mchezo wake wa kuvutia kambini Salzburg umefanya Hungary kumjumuisha katika timu yake ya taifa mara nane. Alifunga roketi dhidi ya Uturuki taifa lake likishinda 1-0 kwenye Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya hapo Septemba 3.

Bila familia yake kusimama naye, kumpa ushauri na babaye kufundisha soka hadi alipoingia akademia ya Salzburg, Dominik anasema asingefika umbali aliko sasa. Bei yake sasa imepanda na kufika Sh3.2 bilioni.