Makala

DINI: Mungu akupenda kama kwamba ni wewe pekee uliye duniani kote

November 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTIN KAMUGISHA

MKAZI mmoja alimuuliza msomi Leith Anderson: “Kama ungetamka sentensi moja kwa umati wa watu wa ulimwengu, ungewaambia nini?

Alijibu, “Nyinyi ni wa muhimu kwa Mungu.” Kuna methali isemayo, Kinyonga anasema, wengine wanakuheshimu unapojiheshimu ni kwa sababu hii natembea kama mfalme. Wewe ni wa muhimu, tembea kama mfalme, tembea kama malkia.

Hadhi yako na umuhimu wako vinatajwa na mtunga Zaburi: “Mtu umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; umevitia vitu vyote chini ya miguu yake” (Zaburi 8:5-6).

Asiyekujua hakuthamini. Watu wakikujua watakuthamini. Wanasema wewe ni wa thamani. Wewe una umuhimu. Anayekudharau hakujui. Anayekudunisha hakujui. Asiyekuheshimu hakujui. Asiyekuthamini hakujui. Anayekubeza hakujui. Asiyekujua ukuita, “wewe.”

Hoja si watu wakujue bali na wewe ujijue. “Kujijua ni mwanzo wa kujiendeleza” (Methali ya Uhispania). “Anayewajua wengine ni msomi. Anayejijua ana hekima” (Laotse).

Tunaweza kutaja sababu kumi na mbili kwa nini wewe ni wa muhimu. Kwanza umeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu. “Kama umemuona ndugu yako, umemuona Mungu,” alisema Clement wa Alexandria. Maana yake ni kwamba, ndugu yako kama ulivyo wewe, ana sura ya Mwenyezi Mungu. Pili, wewe ni wa muhimu sababu unapendwa na Mungu. Mungu anakupenda kama kwamba ni wewe peke yake duniani.

Tatu, wewe ni wa muhimu, hakuna mbadala wa wewe, hakuna anayeweza kuziba pengo lako. Mtu akiaga dunia inasemwa, Ameacha pengo. Nne wewe ni wa muhimu kwa sababu Yesu anakujua kwa jina. Mfano, tunasoma kumhusu Zakayo. “Na Yesu alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, ‘Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako,” (Luka 19:5).

Tano, wewe ni wa muhimu, sababu Mungu anakukumbuka. “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake, aweza kumsahau mzao wa tumbo lake asimhurumie? Hata kama yeye angemsahau lakini mimi sitakusahau wewe hata kidogo” (Isaya 49: 15-15). Sita, wewe ni muhimu sababu ya upekee wako. Alama zako za vidole ni za pekee. Kidole gumba chako kila saini ambayo mtu mwingine duniani hana.

Saba, wewe ni wa muhimu Mungu amekuchora kwenye kiganja chake. “Tazama, nimekuchora katika viganja vya mikono yangu, kuta zako ziko mbele zangu daima” (Isaya 49: 16). Nane, wewe ni wa muhimu kwa sababu Yesu alizaliwa kwa ajili yako. Wewe ni wa muhimu kwa sababu Yesu alikufa kwa ajili yako.

Akili

Tisa, wewe ni wa muhimu kwa kuwa akili yako inatofautiana na ya wengine ili ulete kitu tofauti duniani. Akili ni nywele kila mtu ana zake.

Kumi, wewe ni muhimu kwa sababu umeneemeshwa. Neema ni kama baridi hata ukifunga mlango inapita. Hata kama watu hawatarajii wewe upate bahati, wewe ni wa muhimu kiasi cha kupata bahati. Methali ya Kiswahili inasema ukweli mtupu. Bahati humwacha wa mbele na kumfuata wa nyuma.

Kumi na moja, wewe ni wa muhimu sababu unapiganiwa. Mama mwenye ulemavu wa miguu alitupa magongo yake na kupanda ngazi ili kumwokoa binti yake wa miaka mitatu aliyekuwa kwenye chumba ghorofani kilichowaka moto. Kuna mama aliyekuwa ameumia vibaya sana kwenye ajali ya gari. Hakuweza kutembea bila magongo. Alikuwa jikoni alipogundua kuwa nyumba inawaka moto. Alisahau kutoweza kwake kutembea bila magongo. Alikimbia kwenda ghorofa ya pili na kumbeba binti yake. Rubani wa ndege akiwa kwenye ndege ndogo akipata ajali au ndege ikipotea, shughuli nyingi za watu zitasimama, kumtafuta.

Kumi na mbili, uwepo wako, ni wa muhimu. Uwepo wako ni tiba ya msongo wa mawazo kwa wafiwa na wagonjwa. Wafanye wengine wajisikie ni wenye umuhimu. Watakufanyia mengi mazuri na watakujali na watakuinua. Unapowafanya wengine wajisikie ni wa muhimu, watakufanya na wewe ujisikie ni wa muhimu.