Makala

DINI: Ukitaka kesho nzuri toka katika shimo la jana, utukufu ni mbele kwa mbele

September 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTIN KAMUGISHA

YAJAYO ni mtihani.

Kioo cha mbele cha gari ni kikubwa kuonesha kuwa makubwa yako mbele. Vioo vya upande vya kutazamia nyuma ni vidogo kuonesha kuwa madogo yako nyumba, utukufu ni mbele kwa mbele.

“Yajayo ni mazuri zaidi kuliko yaliyopita” (Methali ya Kiarabu). Mungu ametuahidi mazuri. “Maana mimi Mwenyezi Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye” (Yeremia 29:11).

Watunzi wa hadithi na filamu hutumia mbinu inayoitwa “ploti” ambapo mhusika mkuu hupata matatizo makubwa na changamoto kubwa. Mwishowe hufanikiwa na hivyo kufanya hadithi au filamu ivutie. Mungu ni Mtunzi wa watunzi, ni Muumba wa watunzi. Anapotengeneza hadithi ya maisha yetu anataka mwisho wa siku ivutie. Anaweza kukupitisha kwenye matatizo makubwa mwisho wa siku utukufu ni mbele kwa mbele. Paka anaweza kupigwa teke akaangukia bakuli ya maziwa. Utukufu ni mbele kwa mbele lisilowezekana linawezekana.

Jana haiwezi kubadilishwa lakini kesho ipo ndani ya mikono yako. Usitazame nyuma yajayo hayapo kwenye jana, yapo kesho. Kuna baadhi ya watu wanaoiogopa kesho wakifikiria matatizo ya jana yatarudi.

“Namna nzuri ya kubashiri kesho itakavyokuwa ni kuiumba,” alisema Abraham Lincoln aliyewahi kuwa rais wa Marekani. Ukweli ni kuwa umetoka mbali, upo mbali, unakwenda mbali. Huenda upo mbali na ndoto zako, na maono yako na mipango yako. Kuzifikia ndoto zako, bado una mwendo wa kwenda. Lakini utukufu ni mbele kwa mbele.

“Sijui kikomo chako kitakuwa kipi, lakini neno moja najua: baadhi yenu watakaofurahi watakuwa wale ambao wametafuta na kugundua umuhimu wa namna ya kutumikia,” alisema Albert Schweitzer.

Mtoto anapopelekwa shule, wazazi hawajui atakuwaje mbeleni, utukufu ni mbele kwa mbele. Kuna mwalimu wa shule ya awali aliyekuwa anawainamia watoto wadogo walipokuwa wanaingia darasani.

Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo alisema: “Hao watoto ni wabunge wa kesho, ni maprofesa wa kesho, ni wafanyabiashara wa kesho.” Ni kweli utukufu ni mbele kwa mbele.

Nelson Mendela alipofungwa Roben Island miaka aliyokaa kwenye kisiwa hicho aliita miaka yenye giza. Lakini utukufu ni mbele kwa mbele baada ya kukaa gerezani miaka 27 alikuwa Rais wa Afrika ya Kusini. Baada ya miaka yenye giza alipata miaka yenye mwanga. Mungu alichokuwekea hakiozi. Ni methali ya Tanzania. Ni methali ambayo inatia matumaini kwa watafutaji na waliokata tamaa. Makubwa Mungu aliyokuwekea yatafunuliwa mbele kwa mbele. Mungu anaweza kubadili miiba ikawa maua, anaweza kubadili hasi ikawa chanya, anaweza kubadili machozi ya huzuni yakawa machozi ya furaha. Katika nyufa za maisha Mungu anaweza kuleta mwanga wa matumaini. Mwandishi wa nyimbo Leonard Cohen aliandika, “Kuna nyufa katika kila kitu; hivyo ndivyo mwanga unavyoingia.”

“Wale ambao wanatazama tu jana au leo kwa uhakika wanaikosa kesho,” alisema John F. Kennedy (1917 – 1963). Kama unautazama kwa muda mrefu mlango uliofungwa jana, utaukosa mlango utakaofunguliwa kesho. “Historia haina leo bali jana tu inayokiimbilia kesho, kujaribu kung’ang’ania jana ni kutupwa kando” (John F. Kennedy).

Nionavyo mimi, ili kuiumba vizuri kesho lazima utoke katika shimo la jana.

Kuna aliyesema, “ukiitumia leo yote kuilalamikia jana hakutaifanya kesho kuwa nzuri zaidi.”

“Kesho inategemea tunayofanya leo,” alisema Mahatma Gandhi.

Usiyalilie maziwa yaliyomwagika jana. Yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo. Iambie jana yako, nakushukuru kwa masomo uliyonipa. Iambie leo yako, nakufurahia, sijasahau kuishi. Iambie kesho yako, nakutumainia na nitafanikiwa. Niko tayari kuyakabili ya kesho kwa mtazamo chanya.