DJ anayetumia miguu kuburudisha Wakenya
Na PAULINE ONGAJI
Amekiuka vizingiti sio tu vya kijinsia, bali pia kiafya na maumbile na kutimiza ndoto yake ya kufanya kazi kama dijei.
Kutana na Bi Winfred Wanjiku Muchiri al-maarufu DJ Wiwa, dijei kutoka eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga, ambaye licha ya kuugua maradhi ya cerebral plasy – hali ambayo imepooza mikono yake – amejiundia jina kupitia kazi hii inayohusisha matumizi ya mikono kwa wingi.
Katika miaka 26 DJ Wiwa hajaruhusu kupoza kwa mikono yake kumzuia asitimize ndoto yake, ambapo kwa sasa anafanya kazi hii vizuri kwa kutumia miguu. Ni suala ambalo limemuundia jina na kumshindia mashabiki nyumbani na mbali, ambapo anajivunia kupata mialiko katika kaunti za mbali na nyumbani, ikiwa ni pamoja na Nairobi.
“Nachukulia ulemavu huu kuwa baraka kwangu kwa sababu siamini kwamba ningekuwa katika taaluma hii wapo singekuwa nakumbana na ulemavu huu. Pengine, ningekuwa nikifanya kazi ingine isiyofurahisha,” aongeza.
Ukakamavu wake umemfanya kuwa kigezo cha wengi, hasa wanaovutiwa na uwezo wake wa kufanya hivyo kwa kutumia miguu.
“Nimekumbana na watu wengi wanaokuja tu kuona jinsi nafanya kazi hii kwa kutumia miguu. Kupitia kazi hii naamini kwamba nimechochea wengi kufanya kazi ambazo awali walihofia, na kwangu huo ni ufanisi mkubwa sana maishani,” aongeza.
Lakini mwanzoni haikuwa rahisi kwake kwani alilazimika kukabilina sio tu na ulemavu wake, bali sauti za upinzani kutoka kwa baadhi ya watu waliohisi kwamba ndoto yake ilikuwa mzaha.
Lakini pia, asema kwamba nguvu za kusonga mbele zinatoka kwa marafiki wa karibu na jamaa zake ambao pia ni mashabiki zake wakuu.
“Lakini mamangu ndiye aikuwa nguzo yangu kuu katika safari hii, kabla ya kifo chake mwaka jana. Aliona jinsi nilivyopenda muziki na yeye ndiye aliyependekeza niwe dijei na hata kunisukuma kusomea kazi hii katika taasisi ya mafunzo.”
Lakini pia anazungumzia baadhi ya madijei wenzake wengine ambao wamekuwa nguzo katika kazi yake. “Kwa mfano, baada ya kukamilisha masomo yangu katika taasisi hiyo, madijei nitokako waliungana na kuninunulia mtambo wa kuchanganya muziki kama zawadi, na hivyo kunisaidia kuanzisha biashara yangu.”
Hata hivyo kutokana na janga la maradhi ya Covid-19, kidogo mambo yamekuwa magumu kwa Dj Wiwa. “Kabla ya janga hili, nilikuwa napata shoo nyingi, lakini baada ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko, imekuwa changamoto kufanya burudani. Hii imeathiri mapato yangu,” aeleza.
Lakini licha ya haya asema bado matumaini yapo hasa ikizingatiwa kwamba sasa amehamisha kazi yake mtandaoni.