Makala

DKT FLO: Mbona napata UTI kila nikigawia mume asali?

December 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Mpendwa Daktari,

Mume wangu anafanya kazi katika mji mwingine na sisi hukutana baada ya miezi miwili na mitatu. Tatizo ni kwamba nimekuwa nikikumbwa na maradhi ya njia ya mkojo, UTI, kila baada ya kushiriki tendo la ndoa naye. Kwanza kabisa, je maambukizi haya ni maradhi ya zinaa? Na je anaweza kuwa ana uhusiano wa pembeni au kuna jambo lingine linalonisababishia maambukizi haya?

Vera, Nairobi

Mpendwa Vera,

UTI ni maambukizi yanayokumba njia ya mkojo, kutoka kwa figo hadi kwa urethra. Kwa hivyo, la, sio maradhi ya zinaa. Kwa wanawake, maradhi ya zinaa huathiri mfumo wa uzazi na mara nyingi husababisha majimaji yenye harufu mbaya kutoka ukeni, kuwashwa sehemu ya uke, uchungu wakati wa tendo la ndoa na maumivu sehemu ya chini ya tumbo. Pia yaweza kusambaa na kufika mfumo wa mkojo na kusababisha maumivu wakati wa kukojoa, kuhisi kukojoa kila mara na maumivu sehemu ya chini ya tumbo.

Yawezekana kwamba maambukizi ya kila mara ya UTI yanasababishwa na honeymoon cystitis; hali inayomkumba mwanamke anaposhiriki tendo la ndoa baada ya kukaa muda mrefu kabla ya kufanya hivyo. Maambukizi ya UTI husababishwa na bakteria ya kawaida kwenye ngozi ya mwenzako unayeshiriki naye tendo la ndoa, ambayo hupitishwa wakati wa kushiriki tendo la ndoa baada ya kukawia kabla ya kufanya hivyo. Pia maambukizi haya ya kila mara yaweza kutokana na maradhi ya zinaa.

Ni muhimu kujua iwapo pia mwenzako anaonyesha ishara hizi na ni vizuri ikiwa mtafanyiwa uchunguzi wa kiafya. Pia, unapaswa kufanyiwa uchunguzi wa mkojo na sehemu ya uke kutambua iwapo mfumo wa uzazi umeathirika.

Nyote mnapaswa kuoga kabla ya kushiriki tendo la ndoa na kukojoa pindi baadaye kuhakikisha kwamba mnaondoa aina yoyote ya bakteria ambayo huenda imeingia kupitia urethra. Pia wakati wa kushiriki tendo la ndoa tumia mafuta ya kulainisha ili kupunguza msuguano wakati huu. Kunywa maji kwa wingi na uhakikishe kwamba choo ni kisafi kabla ya kukitumia. Aidha, unapojipangusa baada ya kwenda choo kikubwa, jipanguse kuanzia mbele ukirudi nyuma.

Mpendwa Daktari,

Mwanamume anapaswa kushiriki tendo la ndoa mara ngapi kwa wiki? Nauliza kwa sababu mke wangu ana hamu ya karibu kila siku na siwezi kabisa kumridhisha. Sasa nahofia kwamba atakuwa na uhusiano wa pembeni. Amezidi au ni mimi mzembe katika majukumu yangu kama mume?

Denno, Nairobi

Mpendwa Denno,

Ni nadra sana kwa kiwango cha ashiki kati ya wanandoa au wapenzi katika uhusiano kuambatana. Ni kawaida kwa mmoja kumzidi mwenzake. Hili sio jambo kuu na wala halipaswi kukupa wasiwasi, ila tu iwapo kuna tatizo ambalo limekupunguzia hamu.

Kuna baadhi ya matatizo ya kihomoni na kiakili ambayo yaweza kusababisha kiwango cha juu cha ashiki. Kwa upande mwingine, mabadiliko ya viwango vya homoni, msongo wa akili, wasiwasi, mafadhaiko, uchovu, matatizo kwenye uhusiano pia yaweza kuchangia upungufu wa viwango vya ashiki.

Hata pasipo matatizo haya, inamaanisha kwamba wahusika wanapaswa kushirikiana kutambua tatizo liliopo na kujaribu kulitatua ili kuhakikisha kwamba kila mmoja anaridhika. Hii inamaanisha kwamba kuna siku ambazo mkeo atakubali kutoshiriki mapenzi kwa sababu anaelewa hali yako, na kwamba wewe pia unatia bidii kuridhisha mahitaji yake.

Pia, nyote mwaweza kuunda ratiba ya wakati wa kushiriki tendo la ndoa. Jadilianeni kwa uwazi pasipo kulaumiana. Ikiwa anakupenda na anafahamu kwamba unajitahidi kuridhisha mahitaji yake, basi uwezekano wa yeye kuwa na uhusiano wa pembeni kwa sababu ya udhaifu huu utakuwa chini sana.

Mpendwa Daktari,

Nitakabiliana aje na vidonda vinavyoshambulia ngozi ya kichwa changu na kusababisha nywele kung’oka kila mara?

Melanie, Mombasa

Mpendwa Melanie,

Tatizo la vidonda vya kila mara kwenye ngozi ya kichwa, vile vile nywele kung’oka, laweza kuwa lasababishwa na maambukizi (kwa mfano maambukizi ya ukuvu), au kutokana na maradhi ya ngozi kama vile psoriasis, eczema, seborrheic dermatitis miongoni mwa mengine.

Ili kukabiliana na tatizo hili, lazima tatizo litambuliwe na kutibiwa. Itakuwa vyema ikiwa utachunguzwa na mtaalamu wa ngozi, sampuli ya ngozi kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi. Pindi maradhi yakishatambuliwa, utapewa tiba inayofaa ambayo mara nyingi huhusisha mafuta na/au tembe za kumeza.