DOMO KAYA: Huyu mzee wa kiki hachoki?
Na MWANAMIPASHO
NIMEMALIZA wiki mbili sasa nikiwa namwaza Ringtone.
Huyu msanii mwana sijawahi kumwelewa kabisa.
Katika umri wake na utoto alionao kanishinda.
Jamaa kwa jinsi anavyopenda fursa ukipenda kiki, we acha tu.
Sasa baada ya mwaka 2018 kutuvurugia ubongo na mapenzi yake kwa Zari Hassan, mwaka 2019 kauanza kivingine kabisa.
Kama unakumbuka, mwaka jana alidai kuwa kamzimikia kishenzi kichuna Zari baada yake kuachana na Mondi.
Jamaa alifikia hatua ya kufanya ‘kufuru’ ya ‘kununua’ gari la kifahari aina ya Range Rover ili kumzawadia Zari, mama huyo wa watoto watano alipozuru nchini.
Kuna waliomwamini Ringtone ila kwa watu wenye akili zao, toka mwanzoni tulijua hamna kitu.
Halafu kama haitoshi, gari hilo wala hakununua, kikubwa alichofanya ni kuazima.
Hivi kweli unaweza kumnunulia mwanamke mwenye pesa zake zawadi kama ile wakati hata siku moja hujawahi kuzungumza naye hata kwenye simu, hata tu kumwambia jinsi macho yake madogo na ya kupendeza yanakupa taabu?
Ringtone kweli bwege kabisa.
Kwa hilo wengi wenu mlimkaushia, mlijua bayana jamaa alikuwa anasaka kiki tu sema ilikuwa kiki ya kipumbavu na ya kitoto.
Na kama mlidhania eti kakoma, mwaka huu sasa ndio kawagomea mpaka basi. Mzee wa fursa alipata upenyu wake kupitia ile bifu ya Mr Seed na Bahati, alikimbia nayo na kwa bahati nzuri kauli alizotoa kuhusu bifu baina ya wasanii hao wawili zilikuja kutimia.
Hii ikiwa ni baada ya Mr Seed kukiri kwamba aliyoyasema Ringtone kumhusu yeye na Bahati yalikuwa na ukweli kwa kiasi fulani.
Barua hatari
Sasa jamaa kwa kuona kama vile tumemwani, wiki iliyopita mzee wa fursa alitwamkia tena.
Safari hii aliibuka na barua moja hatari. Barua yenyewe msanii huyo alidai kaandikiwa na mwenyekiti wa mtaa wa kifahari wa Karen anakoishi, akidai kwamba wamemwagiza kuwaondoa ng’ombe 40 anaowafuga kwenye boma lake.
Ushenzi ndiyo huo sasa.
Kwa maarifa yake Ringtone aliamini kwamba tutamwamini na barua yake ya kujitungia. Ilikula kwake, namna aliisoma mwenyewe kwa namna Wakenya tulivyompasha.
Kwa kila aliyeisoma barua hiyo, aliamini aliyeiandika lazima alikuwa ni ng’ombe pia. Na ng’ombe mwenye hakuwa mwingine bali huyo Ringtone.
Mzee wa fursa alikosea kwa vitu vingi.
Mwanzo lugha ya Kiingereza iliyotumika pale ilikuwa na makosa chungu nzima. Ingelikuwa ni mtihani wa insha, pale Ringtone angeng’oka na alama nane juu ya arobaini.
Ukiachana na Kiingereza kibovu, barua ilidai kwamba imetoka kwa Chama cha Karen Langata District Association (KLDA).
Tatizo ni kwamba chama hicho hakipo, kwa mujibu wa wakili maarufu na tajiri, Grand Mullah aishie Karen, alipoulizwa ni kwa nini hana cheo KLDA.
“Nitakuwaje na cheo wakati chama chenyewe hakipo,” alijibu Ahmednasir Abdullahi al-maarufu Grand Mullah.
Kama haitoshi namba za simu za afisi ya chama hicho hewa hazikuwa zikifanya kazi. Wala hazikuita. Hata barua pepe haipo.
Kingine ni kwamba barua haikuwa imepigwa muhuri. Ringtone anapenda fursa sana, hilo lipo wazi, tatizo akili yake ndogo imefeli.
Ushauri wangu kwake ni huu, amwibukie Bad Man Shivoh yaani Otile Brown ili amfunze namna ya kuwa mbunifu na kiki zake.
Wakati Ringtone akifeli na barua yake bonoko, mzee wa fursa Bad Man Shivoh aliua mada alipoibuka katikati mwa jiji na mabunda ya noti akawa anawagawia wapita njia eti anawanunulia lanchi.
Labda angelikuwa mngwana zaidi, angewaibuikia machokosh na mayatima.
Lakini je, fursa angeipata? Hivyo kuibuka kitaa ilikuwa hesabu sahihi.