DOMO KAYA: Mbona 001 atukanganya?
Na MWANAMIPASHO
KUNA kitu alichokisema juzi Gavana 001 au ukipenda ‘Sultan’ ambacho sina uhakika kama nilimwelewa vizuri na hata ikiwa nilimwelewa basi alinipoteza kabisa.
Nitaanza kwa utangulizi tu, kisha nitamalizia nacho. Acha nianze hivi.
Hakuna asiyefahamu jinsi 001 anapenda starehe. Yeye ni mfano mzuri wa mtu anayezingatia ule msemo wa ‘ukipenda starehe, usiogope, gharama’.
Ataogopaje gharama wakati yeye ni gavana mwenye ushawishi mkubwa halafu kama haitoshi ana himaya ya biashara kibao zinazomwingizia mamilioni ya pesa licha yake kupata D-ondoa kwenye KCSE?
Gavana hula maisha kwa kijiko mzee. Anaishi kama ‘Sultan’ wa kweli jinsi walivyokuwa hata kabla ya ukoloni. Amegomea uzee, anapiga pamba hatari, fasheni yake sio mchezo, sema tu hajui kuimba.
Laiti angelikuwa na kipaji hicho, basi huenda angelikuwa staa mkubwa hata kuliko Domo au ukipenda Mondi.
Kwa magavana wote, Sultan anapenda burudani sio siri. Kahusika kwenye ufanikishaji wa miradi mingi ya wasanii. Kawasaidia wengine kibao kwa kufadhili kazi zao.
Kaandaa matamasha ya kutosha Mombasa na kuwaalika wasanii.
Hata ile shoo Chris Brown aliyoipiga Mombasa, watu wa karibu wamedai mkono uliohusika pakubwa ni wake Sultan. Unaweza ukabisha ila kama unakumbuka, aliwahi kula bata na Fat Joe wakati fulani kule Dubai na inawezekana alitengeneza koneksheni nyingi ikiwemo ya kumfikia Breezy.
Kwa wanaomtoa rangi hasa wapinzani wake, watakuambia ‘maendeleo’ makubwa aliyofanya Mombasa ni uandaaji wa shoo za burudani.
Aidha inaweza ikawa iliwakera wengi kwa mfano kumleta Breezy kisha kumlipa Sh90 milioni kwa shoo ya dakika 90.
Lakini kama ni kero, hili halikuwa la kwanza. Nimezisikia ripoti za wasanii kibao wa Mombasa wakidai kwamba kuna mafia wanaoongozwa na mtangazaji Gates Mgenge, waliomzingira ambao ni washauri wake wa masuala ya burudani Mombasa.
Akothee miongoni mwa wasanii wengine wamedai genge hili huwazuia wasanii wengine wa Mombasa kumfikia Sultan. Ili kumfikia lazima upitie kwao na ukiwa msumbufu sana, wanakuchomea picha kwake.
Lawama
Lawama hii ambayo nimeisikia kwa muda sasa, imenipelekea kuhoji ikiwa, hii ndio sababu 001 anawafagilia sana wasani wa Bongo. Baadhi yao wapo karibu sana naye utadhani kama vile ni pacha.
AliKiba na Ommy Dimpoz ni kama vile wao humwabudu kwa zile sifa ambazo wao humlimbikizia.
Ukaribu wao naye umewasaidia kupata shoo zenye mpunga Kenya hasa Mombasa.
Sasa homa hiyo ya wasanii wa Mombasa iliwafikia wa Nairobi. Nao wameibuka na lao wakihoji ni kwa nini anaonyesha kuwapendelea na kuwasapoti sana wasanii wa Bongo.
Juzi aliwajibu kwa kusema eti, ukaribu wake na wasanii wa Kibongo, ni mkakati na mpango wa kuwafungulia milango wasanii wa Mombasa ili nao wakubalike Tanzania.
Hili ndilo linanikanganya. Bado sijamuelewa Gavana 001. Kauli yake mbona ya kiungo sana.
Kama kweli ndio kusudi hilo, kwa miaka yote hiyo amekuwa karibu na mastaa wa Kibongo mbona bado hatujashuhudia milango ikiwafungukia wasanii wa Mombasa? Au itakuja kutokea hatamu yake itakapomalizika. Mmmh! Sisemi. Bado nagunaguna kama Willy Pozee.