• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
DOMO KAYA: Nai-Fest inazidi kukosa shangwe

DOMO KAYA: Nai-Fest inazidi kukosa shangwe

Na MWANAMIPASHO

STORI kubwa ya Showbiz iliyotrendi wiki hii inamhusu soshiolaiti maarufu Bridget Achieng, aliyelala siku moja na kesho akaamka akiwa promota ‘mwitu.’

Lazima utakuwa unaikumbuka ile shoo yake ya Nai-fest wiki mbili au tatu zilizopita. Kusema kweli wazo la kuja na tamasha kama ile hakika sikutegemea kuliona likiibuliwa na soshiolaiti. Hatujawa na mazoea ya kuwaona masoshiolaiti wa Kenya wakiibuka na mawazo ya kimaendeleo kama haya.

Ndiyo maana hata Huddah Monroe alipozindua biashara yake ya vipodozi, sikuwa mwepesi wa kumwamini. Hakika kumbe sikukosea kuamini nafsi yangu iliyomshuku. Baada ya kuanza vizuri siku hizi nimesikia malalamishi ya warembo wengi wakidai bidhaa zake ni feki. Hii stori acha tupige siku nyingine, niruhusu nirudi kwa Bridget.

Bridget alipoibuka na wazo hilo la kuwepo na tamasha ya Nai-Fest mwaka jana, vile vile sikumwamini. Ile nafsi iliyomshuku Huddah na biashara yake ya vipodozi ndio iliyoshuku uwezo wake kuwa promota. Kwa miaka ambayo nimefanya showbiz, nilikuwa nashindwa ni vipi ghafla Bridget kapata pesa za kuandaa tamasha kubwa kama ya Nai-Fest.

Huku nikiendelea kuwa na dukuduku zangu, aliniacha hoi apotangaza kuwa atamleta staa wa Nigeria Joey Boy, aliyehiti mwaka jana. Hakika Bridget alimleta na jamaa akapiga shoo na kisha akarudi zake kwao. Ila yale mashaka niliyokuwa nayo kuhusu uwezo wake yalidhihirika wazi pale kulipoibuka wadau kadhaa waliodai kutolipwa kwa kazi walizofanya. Wapo watoaji huduma ambao mpaka sasa nasikia wanadai. Ipo kampuni ya PR inayodai haijalipwa mpaka leo. Bridget aliamua kuwaosha na stori ikalala.

Mwaka huu akatangaza tena ujio wa makala ya Nai-Fest ya pili. Kama kawaida aliamua kumwendea staa mwingine wa Nigeria aliyehiti. Hapo akamleta Reekado Banks. Uwanja wa Ngong Race Course ulifurika kinoma na wengi walitarajia kuona Reekado akitumbuiza. Aisee! Ilikula kwao mtunzi huyo wa hiti ya Rora hakupanda stejini, kisa na maana, Bridget hakumlipa stahili yake kwa mujibu wa makubaliano.

Naarifiwa kwamba alipaswa kumlipa salio ya malipo yake dola 5,000 asubuhi ya Jumamosi kabla yake kupanda stejini baadaye jioni ya siku hiyo, ila binti wa watu akaingia mitini asipatikane. Shoo ilipomalizika, Bridget alitoa taarifa kwamba jamaa alikosa kupiga shoo kwa sababu muda ulikuwa umekwenda sana na lazima sheria za kafyu zingezingatiwa.

Keshoye Jumapili, ikabainika kuwa jamaa kumbe hakupiga shoo sababu soshiolaiti huyo hakumlipa. Hivi alikuwa na uhakika Reekado hangeanika ukweli kwa sababu alihepa na ‘deposit’. Lakini kama unadhani ni Reekado tu, pia naye shogake Tanasha Donna, hakupiga shoo baada ya kukosa kulipwa na huyu soshiolaiti. Pia wapo madansa wanaodai hawakulipwa.

Sasa nafikiri utakuwa umenielewa kwa nini nilitanguliza kwa kumwita promota ‘mwitu’. Hapa nilipo najiuliza; je, mwakani pia bado anaandaa Nai-Fest au ndio imekufa hivyo? Ila kwa namna ambavyo hawa masoshiolaiti hujiamini, hamna wasichoweza kukifanya hata ikiwa hawawezi!

You can share this post!

KAMAU: Tutathmini upya suala la urithi kuzuia mizozo

Mazishi ya Mbunge yapigwa breki