Makala

DOMO KAYA: Size 8, DJ Moh kutoza wageni elfu 10 Valentino

January 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANAMIPASHO

HAYA mwana Valentine Dei hiyo inakaribia japo ipo mbali kidogo, kama wiki tatu hivi zimesalia.

Naambiwa tarehe hiyo wanaume watakuwa na Men’s Conference, ila naona ni kama vile DJ Moh hakupata memo.

Sababu naona yeye na mke wake Size 8, tayari wanao mpango. DJ Moh ambaye kwa majina ya kitambulisho ni Sammy Muraya, kwenye siku hiyo Februari 14, wamepanga kuandaa karamu waliyoipa jina Dine With The Murayas.

Karamu hii itafanyika katika hoteli ya Emory ambayo kama sikosei ipo katika mtaa wa Kileleshwa, Nairobi.

Waalikwa ni wanandoa kama wao na wanaochumbiana. Mpango wa siku hii ya wapendano ni kujumuika pamoja kwa msosi, kutangamana, na kubadilishana mawazo kuhusu maisha ya ndoa.

Pia kutakuwa na michezo, sijui ni michezo gani hiyo, ya kiutu uzima ama ipi, sina habari. Pia kutakuwepo na wanenaji au ndio sijui washauri wa ndoa? Kutakuwa na ngoma na pia atakuwepo DJ kutoa burudani ya muziki.

Hii ndio shughuli watakayokuwa nayo hawa kina Murayas siku hiyo ya Valentine. Nafikiri ni mpango mzuri tu sana. Wamejitahidi kuwaalika wanandoa kuhudhuria. Iwapo wapenzi wa kutosha watatokea, basi itakuwa karamu ya kupendeza.

Hata hivyo mimi nina shaka ikiwa karamu hii itafanikiwa. Na hii ni kwa sababu, kuingia sio bure. Kina Murayas wameweka bei za ndege kwa wanandoa wanaotaka kuhudhuria karamu yao. Zipo tiketi aina mbili mzee. Kwa tiketi ya kawaida ni Sh7,000. Kwa VIP, basi Sh10,000 zitawatoka.

Mpaka hapo sijui kama umenishika. Eeeh! Najua ni mkwanja mrefu tena sio kwa Njaanuari hii. Bei hiyo mwenyewe imeniacha na mshangao. Hawa Murayas bwana watakuwa wana maisha mepesi sana, au ni kwa sababu bado hawajaanza kulipa karo ya maana ndo wanachukulia ishu kawaida sana. Wakati kila mmoja akiwa analemewa na maruweruwe ya Januari, wao wapo makini kukamua zaidi.

Sasa basi kama unashindwa kuelewa tiketi za bei hiyo zinagharimia nini, mwanawani, utashangaa. Kwa Sh7,000, watapata msosi mara nne (4 course meal) kwa kimombo, glasi ya juisi, chokoleti, kazawadi na maua.

Na kwa Sh10,000 watapata msosi mara nne, chupa ya divai, glasi ya juisi, chokoleti, maua na tiketi ya bahati nasibu inayoweza kumshindia yeyote baina yao likizo sijui ya kwenda wapi.

Nimekaa nikajiuliza maswali jinsi unavyojiuliza wewe hapo. Yaani mimi mwanamume mzima niondoke nyumbani na mke wangu kwenda kutoa kiasi hicho cha pesa ili nipewe glasi ya juisi huku nikisikiza stori za ndoa na mahusiano ya watu wengine? Mpaka kuna chokoleti jamani. Huu si utoto? Maua kwa wana wa kiume ni ya faida gani?

Kina Murayas wanatuzengua tu. Hawa watakuwa wanasaka hela tu. Ila siwezi kuwashtumu, wameamua kutumia akili za kuzaliwa. Sijui ni kina nani waliopanga kwenda ila ningetamani kujua sana matokeo. Na pia sitashanga watu wakikosa kufika.

Kwa hili, kina Murayas wametubeba ufala. Labda tiketi zingeuzwa kwa Sh2,000 na Sh3,000 pia mwenyewe ningefumba macho niende kushuhudia. Kwa hela hizo bora niziweke au nifanye kununulia tiketi ya shoo ya Luciano iliyoratibiwa kufanyika mapema Aprili.