Makala

Duale alipoweka kando heshima ya kikazi na kumkosoa Mudavadi paruwanja

Na BENSON MATHEKA January 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Afya, Aden Duale, aliweka kando heshima ya kikazi kwa kumshambulia mkubwa wake, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kutokana na pendekezo lake kwamba kura ya maamuzi ifanywe pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Katika taarifa aliyochapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii Jumatatu, Duale alieleza, kwa lugha kali, kuwa pendekezo la Mudavadi linaweza kusababisha misukosuko nchini.

“Ingawa wito wa kura ya maamuzi si jambo jipya, Katiba yetu imeweka wazi taratibu za kushughulikia masuala ya kitaifa, huku mahakama zikitoa mwelekeo pale kunapozuka utata,” aliandika Duale.

Duale aliorodhesha sababu kadhaa kueleza kwa nini kura ya maamuzi inaweza kuwa hatari.

Kuhusu tathmini ya mipaka ya maeneobunge, alisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikuweza kutekeleza jukumu hilo mapema kwa sababu haikuwa imeundwa ipasavyo na muda wa kikatiba ulikuwa umeisha.

Alisema masuala hayo sasa yanahitaji mwelekeo kutoka Mahakama ya Juu na IEBC, akionya kuwa kusukuma kura ya maamuzi bila mwongozo huo kunaweza kuzua taharuki isiyo ya haja.

“Kifungu 255 cha Katiba kinaorodhesha wazi masuala yanayopaswa kufanyiwa kura ya maamuzi. Hivyo basi, pendekezo lolote lazima lipimwe kwanza kwa kigezo hicho,” alisema.

Mudavadi alikuwa amependekeza kuwa kura ya maamuzi ifanywe pamoja na uchaguzi mkuu ujao kusaidia kutatua masuala ya muda mrefu ya kikatiba.

Akizungumza katika mahojiano ya mwisho wa mwaka na runinga moja ya humu nchini, alisema masuala ambayo hayajapata ufumbuzi, yakiwemo yaliyoainishwa katika ripoti ya NADCO, yanaweza kushughulikiwa kupitia maswali yaliyoandaliwa vyema katika kura ya maamuzi ikiwemo kuundwa kwa ofisi ya Waziri Mkuu.

“Wakenya wanapaswa kukumbatia wazo hili, na tuanze mjadala huu mwaka wa 2026 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027,” alisema.

Hata hivyo, japo pendekezo lake lilikosolewa na upinzani, ukisema anasaka njia za kuhalalisha wadhifa anaoshikilia usiotambuliwa katika Katiba, hakuna aliyetarajia waziri anayepaswa kuwa chini yake, anaweza kumkosoa hadharani na hivyo kumsawiri kama asiyeelewa Katiba na hali ya kisiasa nchini.