Makala

EPRA yazima mpango wa kutimua matatu jijini Nairobi

Na RICHARD MUNGUTI November 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAHAKAMA kuu imezima hatua ya Mamlaka ya kusimamia sekta kawi na mafuta (EPRA) kutimua vyama 13 vya magari ya uchukuzi kutoka Nairobi.

Jaji Enock Chacha Mwita aliagiza EPRA ikome kabisa kuwatimua Sacco hizo 13 zinazosafirisha abiria zaidi ya milioni moja kwa mwaka  na kutoa ajira ya wafanyakazi zaidi ya 200,000.

Jaji Mwita alisema hatua hii ya EPRA kufukuza magari haya ya matatu yanayohudumia zaidi ya kaunti 15 nchini itazua mtafaruku ikitiliwa maanani siku kuu za Krismasi na mwaka mpya zimekaribia.

Na wakati huo huo Jaji Mwita aliwaamuru mawakili wa EPRA , Mwanasheria Mkuu, mawakili wa serikali ya kaunti ya Nairobi pamoja na wakili Danstan Omari anayetetea vyama hivi vya uchukuzi wa abiria wakutane katika muda wa siku saba washauriane kuhusu utendakazi wa vyama hivi.

Agizo la kuzima kufurushwa kwa vyama hivi lilifuatia ombi la Bw Omari kwamba EPRA imetoa arifa kwa vyama hivi vikome kuhudumu katika vituo vya Petroli vya OLA na Total Kenya katika jengo la Afya Centre na OTC na pia River Road.

“Naomba mahakama izime hatua hii ya EPRA kutimua matatu kuhudumu katika vituo vya OLA (afya centre) na Total Kenya (otc) na River Road,” alirai Bw Omari.

Wakili huyo pia alisema mbali na EPRA kuna walalamishi wengine wawili Ezekiel Oyugi na John Gaku waliowasilisha kesi wakiomba matatu zitimuliwe kwenye vituo hivi itakayosikizwa Januari 26,2026.

Akaamuru Jaji Mwita,“Mamlaka ya EPRA imezuiliwa kutimua magari ya matatu kwenye vituo vya petrol vya OLA na Total Kenya Limited hadi kesi iliyowasilishwa na vyama 14 vya wahudumu wa matatu isikizwe na kuamuliwa.”

Jaji Mwita aliamuru jopo la mawakili wa Mwanasheria Mkuu , EPRA, Kaunti ya Nairobi na Bw Omari wawasilishe ripoti Desemba 1,2025 kuhusu mashauri waliyofanya.

Mwenyekiti wa Sacco hizi 14 Clinton Kioko Wambua alieleza mahakama kwamba kutoelewana kulizuka kati ya Serikali ya kaunti ya Nairobi na vyama hivyo.

Wanachama wa Sacco 13 wakiwa mahakama kuu Milimani Novemba 19 2025. Picha|Richard Munguti

“Kamwe hatutabanduka kwenye vituo tunakohudumu. Namsihi Rais William Ruto aamuru mashirika ya EPRA, NEMA na Kaunti ya Nairobi zikome kusumbua wahudumu wa matatu,” Bw Wambua alisema.

Mwenyekiti huyo alisema endapo Rais Ruto atashindwa kuzugumzia EPRA na NEMA basi itabidi awaonyeshe kule watabebea abiria kati kati mwa jiji.

Katika ushahidi aliowasilisha mahakamani Bw Wambua ameeleza Serikali ya kaunti ya Nairobi hupokea kodi ya Sh291.5milioni.

Kodi hii ni ya kuegesha magari haya ya uchukuzi wa abiria.

Magari ya Nissan ni 1.,117 na mabas ni 124.

Bw Wambua alisema kwamba vyama hivi hulipa mamlaka ya ushuru nchini zaidii ya Sh7.8bilioni.

Vyama hivi viliwasilisha kesi hii Oktoba 2025 na kuomba kaunti ya Nairobi, EPRA , Oyugi na Gaku wazuiliwe kutekeleza arifa ya kutimua matatu kuabiriwa kwenye vituo vya petrol wakidai ni tisho kwa biashara ya mafuta.

Mawakili wa vyama hivi wameeleza magari haya ya abiria yanahudumia wakazi wa kaunti zaidi ya 15 nchini na kufurushwa kwao kati kati mwa jiji kutasababisha mtafaruku mkuu na mihemko katika lingo za kisiasa.

Na wakati huo huo makampuni matatu ya kuuza mafuta ya petrol pia yamepinga hatua ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuyaamuru yafunge biashara zao hadi pale yatakapofuata sheria za mamlaka ya mazingira –Nema na mamlaka ya huduma ya mafuta ya petrol-Epra.

Mbali na familia na jamii kuathiriwa na hatua hii inayotokana na ubinafsi wa baadhi ya madiwani wa bunge la kaunti ya Nairobi walioitishwa hongo ya Sh2milioni ili wasipeleke mswada wa kutimuliwa kwa matatu hizi na biashara za mafuta ya petrol kufungwa, serikali kuu itakosa ushuru wa Sh7.2bilioni.

Wenye magari haya walidokeza kwamba kila mwaka wanalipa  kaunti ya Nairobi kodi ya Sh291.5milioni.

Kila mwezi vibao vinavyowekwa kwenye paa za magari ya matatu zikionyesha kule gari inaenda vinalipiwa Sh15,000 kila mwezi kwa kaunti.

“Ni unafiki na ulafi wa  hali ya juu wa kutaka hongo wa madiwani katika kaunti ya Nairobi wanaotaka magari haya yafurushwe,” mawakili wanaowakilisha wahudumu hawa wanadai katika stakabadhi zao mahakamani.

Wahudumu hawa wa vyama hivi wameeleza mahakama kuu kwamba magari yao huwahudumia wakazi wa maneo ya kaunti za Murang’a, Embu, Kirinyaga,Machakos, Makueni, Kisii, Nyamira, Kitale, Kisumu,Mombasa na Kakamega

Miongoi mwa Makampuni ya mafuta yaliyoshtakiwa ni Total Energies (Rhino), Ola Energy (Afya Centre) na Ola Energy (Afya Centre).

Oyugi na Karuu wameshtaki pia Serikali ya Kaunti ya Nairobi (NCC).

Vyama vya matatu vilivyoshtakiwa (Sacco) ni:- Ena Investiment Limited, Transline, Prestige, Kinatwa, Kam,Makos, Thika Road,Muna, Kamuna, Kangema Travellers, Libera Impex Empire, Inter-County Travellers, Muna Shuttle Limited,Kigumo T,Supreme T & T, GTS Supreme, Matco na Nnus Shuttle.

Mahakama imeelezwa na wenye matatu hawa kwamba maisha yao nay ale ya watu wanaowategemea ikiwa ni pamoja na Mekanika, makampuni ya kuuza magurudumu ya magari yatapata hasara kuu isiyopungua Sh10bilioni.

Mawakili Omari na Stanley Kinyanyui wanaowakilisha wahudumu hawa wameomba mahakama kuu izingatie maslahi ya familia zinazotegemea matatu hizi.

Mahakama imeorodhesha kesi hii kusikizwa Januari 26,2026.

Magari ya Sacco hizi yalifikishwa kortini na wahudumu hawa wanaomba jaji anayesikiza kesi hii atembelee maeneo wanayohudumia ashuhudie kama kuna uchafu na ikiwa shughuli zao zinahatarisha maisha ya umma kama inavyodaiwa na Oyugi na Gaku.