ESTHER KALONDU: Nikipewa fursa kwa uigizaji nitatesa
Na JOHN KIMWERE
WAHENGA waliposema penye nia pana njia hawakudanganya maaana ndivyo ilivyo tangu zama hizo mpaka sasa.
Msemo huo umeonyesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii. Hili linazidi kudhihirishwa na vijana wengi, wavulana na wasichana ambao wameamua kujituma kisabuni kwenye juhudi za kusaka riziki. Ingawa alianza kushiriki maigizo mwaka uliyopita anaamini ana talanta ya kufanya vizuri katika sekta ya uigizaji.
Esther Kalondu Ngungu ni miongoni mwa waigizaji wanaoibukia wanaopania kufikia hadhi ya kimataifa miaka ijayo. Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1999 ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kwenye Chuo Kikuu cha East Africa Institute of Certified Studies (ICS) anakolenga kuhitimu kwa shahada ya Diploma kama mwana habari wa Televisheni.
Aidha hufanya biashara ya kuuza nguo na viatu maana bado hajafanikiwa kupata ajira katika masuala ya maigizo.
”Ingawa imekuwa vigumu kwa waigizaji chipukizi kupata nafasi katika maigizo bado ninaamini ipo siku watanikubali,” alisema na kuongeza kwamba haileti shangwe kuona wasanii waliokuwa akiona washiriki maigizo akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi hadi sasa bado ndio wametawala katika tasnia ya uigizaji.
LUPITA NYONG’O
Msichana huyu anasema anatamani sana kushiriki filamu na kupata mpenyo kupeperushwa kwenye runinga maana hatua hiyo itamsaidia kutambulika.
”Katika mpango mzima ndani ya miaka mitano ijayo naona pengine wengi watakuwa nikiniuliza jinsi nilivyofanya ndipo nikapiga hatua katika taaluma ya uigizaji pia biashara yangu,” akasema kisura huyu.
Kadhalika anadokeza kuwa angependa sana kifikiwa kiwango cha mwana maigizo wa Mkenya, Lupita Nyong’o anayetaamba katika filamu za Hollywood.
Kipusa huyu anajivunia kushiriki filamu moja mwaka jana itwaayo Morio ingawa iliyotengenezwa na kundi la wanafunzi wa chuo hicho haikufanikiwa kupeperushwa kwenye runinga. Ingawa hajapiga hatua
WEMA SEPETU
Kuhusu kwa nini Wakenya wengi hupenda kutazama filamu za kigeni kuliko za wazalendo nchini anasema ”Kiukweli sekta ya maigizo nchini ni kama maprodusa wetu wameshindwa kuonyesha vitu mpya maana wanastahili kuwa wabunifu ili kuchota nyoyo za watazamaji wa filamu zetu.”
Anadokeza kuwa katika mataifa mengine waigizaji huwa wabunifu zaidi ambapo huwa wanatengeneza filamu mpya.
Kama wasanii wengine pia angependa kufanya kazi na wenzake ambao wamepiga hatua kisanaa. Anasema anatamani sana kufanya kazi na Brenda Wairimu pia Sanaipei Tande ambao wameshiriki filamu kama Mali na Aziza mtawalia. Kwa waigizaji wa Afrika anatamani sana kufanya kazi na Wema Sepetu (Tanzania) na Destiny Etiko (Nigeria).
Anatoa mwito serikali iwazie kuunga mkono sekta ya maigizo kikamilifu ili kusaidia waigizaji chipukizi ambao wamefurika katika kila kona ya taifa hilo.
Licha ya kuwa mrembo anasema hana mahusiano ya kimapenzi maana mwanzo analenga kujibrandi katika usanii pia biashara yake.