Makala

Fahamu Shareting, mtindo hatari wazazi wanatumia ‘kuuza’ watoto bila kujua

Na BENSON MATHEKA August 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZAZI wamekuwa wakiweka watoto wao katika hatari ya kuvamiwa na wahalifu wa mitandao bila kujua.

Na sasa, wataalamu wa malezi kidijitali wanaonya wazazi kuepuka tabia ya kusambaza picha na video za watoto wao katika mitandao ya kijamii.

Mtindo huu wanaouita Shareting wanasema ulishika kasi wakati wa janga la Covid 19 ambapo ilikuwa vigumu kwa familia na marafiki kukutana ana kwa ana.

Shareting ni mtindo wa wazazi kuchapisha au kupakia kwenye mitandao ya kijamii habari na picha kuhusu watoto wao.

Wanasema kabla ya kuchapisha picha ya mtoto wako katika mitandao ya kijamii fikiria mara mbili, iwe ni kufurahia siku yake ya kwanza shuleni, kufuzu kwenda gredi ya juu, kuhitimu kwake au kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Ni njia ambayo wazazi wengi wanatumia kushiriki matukio muhimu ya maisha ya watoto wao na watu wa familia na marafiki wa mbali na karibu.

Hata hivyo, wataalamu wa malezi kidijitali wanaonya kuwa kuchapisha picha za watoto katika mitandao ya kijamii zinazopendwa na watu wengi wakiwemo wa familia na marafiki wa wazazi, kunaweza kuweka mtoto kwenye hatari.

Wanasema kuwa kuanika picha za watoto kwenye mitandao ya kijamii kunaweza kuwafanya walengwe na wahalifu na pia kunaathiri afya ya akili yao.

“Mara nyingi, wazazi huwa wanachapisha picha za watoto wao katika mitandao ya kijamii na kutoa nafasi kwa wahalifu kuwanyemelea, hasa wanapoanika pale mtoto anasomea, kutaja walimu wao na hata majina ya watoto wenyewe,” asema mtaalamu wa malezi kidijitali ambaye pia ni mwanasaikolojia na tabibu, Dkt Susan Alber.

Anasema japo huenda athari za kuchapisha picha ya mtoto kwenye mitandao zisionekana mara moja, madhara yanaweza kujitokeza katika maisha yao ya baadaye hasa katika mahusiano yao na watu na kukosa kujiamini.

“Unaposambaza habari kuhusu mtoto wako mtandaoni, wahalifu huwa wanaunda na kutoa taswira kuhusu watoto wao. Hii inawapa presha watoto hao kutaka kuwa kile ambacho unawasawiri kuwa na wanapofanya hivi, inawaathiri kisaikolojia. Pia, inasababishia watoto fedheha kubwa wasipofikia kile ulichowasawiri kuwa,” aeleza Dkt Alber.