FATAKI: Ishara za mume asiyekupenda huonekana mapema
NA PAULINE ONGAJI
Hivi majuzi tulikuwa tunajadiliana iwapo ni suala la busara kuanika kila kitu kuhusu uhusiano wako wa kimapenzi mtandaoni, hasa ikiwa mwenzako amekimya kuhusiana na suala hili.
Hii inafuatia tukio la siku kadha zilizopita ambapo tulikumbana na binti fulani akimgombanisha kaka fulani aliyedai kuwa mumewe kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba yuko single, ilhali binti huyo alikuwa ameandika kwamba ameolewa.
Ni suala lililorejesha kumbukumbu ya miaka kadha iliyopita, ambapo binti mmoja kutoka Amerika, kwa jina Monyetta Shaw, alichumbiana na mwanamuziki wa R&B, Ne-Yo.
Bi Shaw aligonga vichwa vya habari baada ya uhusiano wake na mwanamuziki huyo kuvunjika ambapo alidai kwamba kaka huyo alimhadaa eti afanyiwe upasuaji wa kufunga uzazi, kabla ya kumtema na kumuoa binti mwingine kwa jina Crystal Renay.
Kulingana naye, wakiwa pamoja, Ne-Yo alipendekeza wote wafanyiwe upasuaji wa kuwazuia kupata watoto katika siku za usoni, ambapo baada ya kutii alipigwa na butwaa dume hilo lilipomchumbia Bi Renay na kuzaa naye.
Ni suala lililoibua mjadala iwapo kwa kweli kaka huyo alipaswa kulaumiwa kwa uamuzi aliochukua binti huyo. Kwa wengi, hiyo ilikuwa ishara tosha kwamba bwana huyo hakuwa na haja na kipusa huyo, na hivyo ilikuwa juu yake kutambua mapema na kuachana naye.
“Je unahitaji ukweli upi ikiwa kaka amekuambia wazi wazi kuwa hataki kupata mtoto nawe?” Bibi mmoja aliuliza.? Tatizo ni kwamba watu wengi na hasa mabinti hujitia hamnazo kiasi cha kufumbia macho ukweli na kukataa kuchanganua mambo hata ujumbe unapoanikwa peupe. Ishara hizi hujitokeza kwa njia mbali mbali.
Kwa mfano, umekuwa ukimuona akipiga gumzo na mabinti hadharani mtandaoni lakini unapuuza. Umekuwa ukichumbiana na kaka kwa muda ? ilhali dume hilo halitaki kukutambulisha kwa jamaa na marafiki zake.
Hataki kutembea nawe wakati wa mchana na ikiwa ni kukutana mahali, basi ni heri kila mmoja awasili kivyake.? Kaka anazima simu Ijumaa jioni na kuwasha Jumapili jioni, na iwapo kwa bahati mbaya atasahau kufanya hivyo basi hatapokea simu yako wakati huu.
Unadinda kuona kuwa unachezewa na kaka ambaye kila wakati anapompigia simu anaikata na kukupigia mwenyewe masaa kadha baadaye.
Naye mwingine amekuwa akichumbiwa na kaka ambaye kwa miaka mitatu hajawahi mpeleka kwake wala kwao.? Ninachofahamu ni kwamba hakuna jinsi mtu anavyoamka siku moja na kuamua kwamba hakutaki.
Bila shaka kuna ishara ambazo amekuwa akikuonyesha lakini unazifumbia macho huku ukiendelea kukuza imani ya uwongo kwamba huenda wakati mmoja mambo yakabadilika na akakuonyesha penzi.