FATAKI: Mabinti weusi wana haki kufurahia mvuto uliopo sasa
Na PAULINE ONGAJI
HIVI majuzi kulikuwa na gumzo katika kikundi fulani ambapo rafiki yangu alikuwa akilalama jinsi mabinti Waafrika lakini wenye ngozi nyeusi wamekuwa wakipendelewa hasa katika mashindano ya urembo na majukwaa mengine ya kimataifa.
“Hata wanaume wa Kizungu wanapozuru humu nchini hukimbilia mabinti wa rangi nyeusi wakituacha sisi weupe,” akalalama.
Kabla ya kuanza kurusha mawe ningependa kukufahamisha hakuwa na nia mbaya na najua kuna wengine kama yeye wanaolalama kimya kimya.
Ikiwa wewe ni mmoja wao, basi ujumbe huu ukufikie. Tokea nyakati za utumwani, Waafrika na hasa wenye ngozi nyeusi walibaguliwa zaidi sio tu na waliokuwa wakitekeleza unyama huu, bali pia na Wafrika wenzao.
Kwa muda mrefu wanawake wa Kiafrika wenye ngozi nyeusi hasa walikumbwa na changamoto ya kudhihirisha urembo wao hata nyakati uzuri wao ulikuwa wazi.
Kwa mfano, katika uwanja wa Hollywood japo wanawake wa Kiafrika kwa jumla walinyimwa nafasi kubwa za uigizaji, mambo yalikuwa magumu hata zaidi kwa wale wenye ngozi nyeusi.
Hata hapa barani, ni hivi majuzi tu ambapo tumeanza kuona mabango na matangazo ya urembo yakihusisha zaidi wanawake wa ngozi nyeusi.
Katika jukwaa kubwa zaidi la filamu barani; Nollywood, mambo yalikuwa mabaya zaidi kiasi cha kushinikiza waigizaji wengi wa kike kujichubua kupata nafasi.
Ubaguzi
Tukirejea hapa karibu na nyumbani kule Tanzania, tazama video za nyimbo zao ili kuelewa jinsi mwanamke mweusi amezidi kubaguliwa; ndio sababu mabinti wengi huko wanazidi kujichubua, na sio kupenda kwao, ni kwa sababu jamii imeunda dhana kwamba hiyo ndio rangi ya urembo.
Hata hapa nchini, kwa muda mrefu, weupe ulichukuliwa kuwa urembo kiasi cha kupewa jina ‘rangi ya thao’ kuashiria kwamba rangi hii ni mgodi kwa mabinti.
Nakumbuka wakati mmoja mjadala ulichipuka kuhusu vyombo vya habari humu nchini kutawaliwa na mabinti weupe.
Hata kuna wakati mtangazaji mwenye ngozi nyeusi alikiri jinsi alivyolazimika kutia bidii maradufu ili kudumisha uwepo wake.
Kumbuka hii ni licha ya kwamba kwa maoni ya wengi yeye ndiye mtangazaji mahiri wa kike hapa nchini.
Mabinti wenye ngozi nyeusi katika kila pembe duniani wana kila haki ya kuzidi kufurahia fursa na mvuto wanaopokea.
Hata sidhani kwamba daima ni muda wa kutosha kuwalipa kwa dhuluma walizopitia na wanazozidi kukumbana nazo.