FLORENCE NYAWIRA: Wema Sepetu wa Kenya
NA JOHN KIMWERE
Florence Nyawira Mutahi ni miongoni mwa wasanii wanaotarajia kujituma kisabuni ili miaka ijayo kuhakikisha wameibuka mahiri katika sekta ya uigizaji duniani.
Anasema ingawa alianza kujituma katika masuala ya sanaa ya burudani miaka mitatu iliyopita amepania kutimiza ndoto yake hasa kuona filamu zake zikipata nafasi kurushwa kwenye runinga za hapa nchini.
Binti huyu ni mwigizaji, meneja wa kuzalisha filamu pia mwanafunzi anayesomea kuhitimu kwa shahada ya diploma kuhusu masuala ya matangazo na uhusiano mwema katika Chuo cha Co-operative jijini Nairobi.
”Ndiyo nimeanza kupiga shughuli lakini ninaamini nitafanya makubwa katika sekta ya uigizaji,” alisema na kuongeza kuwa hakuna mwanadamu aliyezaliwa akifahamu jambo lolote mbali kila mmoja huanza kwa hatua moja.
“Binti huyu anasukuma gurudumu ya masuala ya uigizaji chini ya kundi la Do Art Centre kama meneja wa kuzalisha filamu tangu mwaka 2016. Ndani ya kundi hili anajivunia kushiriki filamu iitwayo ‘St Luke Gospel-stage play’ pia filamu fupi ‘Circumstances.’
Katika mpango mzima kipusa huyu anasema angependa kutinga zaidi ya kiwango cha waigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood).
Hata hivyo anadai hupenda kutazama filamu za baadhi ya waigizaji wazo kama ‘Heart of a fighter,’ na ‘Weeping souls,’ kazi zake Mercy Johnson, ‘Blood sister,’ na ‘Two Rats’, usanii wake Patience Ozonkwor bila kusahau Regina Daniels ambapo hupendezwa na kazi zake nyingi tu ikiwamo ‘Moments of sorrow,’ na ‘Thunder Child,’ kati ya zingine.
Kadhalika hapa Afrika Mashariki anasema angependa kufikia kiwango cha wasanii Bongo muvi kama Wema Sepetu anayejivunia kuhusika kwenye filamu nyingi tu ikiwamo ‘Red Valentine,’ na ‘Mapenzi Chungu,’ pia Elizabeth Michael aliyeshiriki ‘Gods Love,’ na ‘Tatoo’ kati ya zingine.
Anahimiza wasanii chipukizi kuvunjika moyo kwa kukosa nafasi za uigizaji mbali wazidi kujituma wanapopata fursa kushiriki majaribio na kuamini ipo siku Mungu atafungua milango ya mafanikio.
Ingawa Nyawira aliyezaliwa mwaka 1997 alitambua talanta ya usanii akiwa na umri wa miaka minane akiwa mdogo alidhamiria kuhitimu kama daktari.
”Bila mapendeleo wala kuongeza kachumbari sekta ya filamu hapa Kenya inayo nafasi nzuri kupiga hatua tena zaidi na kufaidi wasanii wengi wanaume kwa wanawake,” alisema na kuongeza kuwa hata hivyo inahitaji kufanyiwa kazi kubwa hasa katika uwekezaji.
Pia anasema kuna umuhimu mkubwa kwa waigizaji chipukizi kutambuliwa na kuanza kunolewa makali yao wakiwa wadogo kama ilivyo katika mataifa yanayoendelea.
Kadhalika anadokeza kuwa serikali za Kaunti zinastahili kuanzisha akademia za kufunza masuala ya uigizaji mashinani kusudi kutoa fursa kwa wasanii chipukizi kujifunza zaidi kuhusu taaluma hiyo.