FUNGUKA: 'Aisee, si peremende eti itaisha utamu…'
Na PAULINE ONGAJI
KATIKA siku za hivi majuzi kumekuwa na ongezeko la visa vya wanandoa kukorofishana na hata kuuana ambapo katika vingi ya visa hivi, suala la udanganyifu limesemekana kuchangia pakubwa.
Hata hivyo, kwa Sternly, huo ni upuuzi.
Kaka huyu mwenye umri wa miaka 34 ni meneja katika kampuni moja jijini Nairobi. Ana mke ambapo wameoana kwa takriban miaka 10 sasa na kujaliwa watoto watatu.
Mkewe hana ajira lakini ni kutokana na uamuzi wake Sternly ambaye kazi yake inamwezesha kukidhi mahitaji ya familia yake.
Unapotazama wanandoa hawa utadhani ni wa kawaida hasa kutokana na penzi wanaloangaza hadharani bila haya.
Kwanza kabisa, wanapenda kufanya mambo pamoja kama vile kwenda dukani, kanisani na hata wakati wa chakula, wao hula kwenye sahani moja.
Hata hivyo, tofauti kubwa hujitokeza wakati suala la mahaba linapotajwa.
Licha ya kuwa uhusiano wa wawili hawa uko thabiti, wanandoa hawa wanaweza kukaa hata miezi mitatu bila kushiriki mahaba.
“Tunalala katika chumba kimoja na sio kwamba tumekosana lakini mke wangu hapendi kunipa haki yangu. Nikibahatika pengine naweza kupata siku mbili kwa mwezi. Ikiwa pengine nataka kutumbuizwa angalau mara mbili kwa mwezi, basi napaswa kuhakikisha kwamba siombi kila mara na nikipewa siku moja, naridhika. Sio kwamba ananichukia ila sababu ni kuwa niligundua anakata kiu kwingineko. Kutokana na sababu kwamba hafanyi kazi, yeye huwa na muda mwingi wa kupata burudani kutoka kwa madume kadhaa. Kuanzia kwa walinzi, wauzaji makaa, manamba na hata marafiki zangu, mke wangu hana mipaka. Mradi wewe ni kidume na mlingoti unasimama imara, basi kuwa tayari kuburudishwa naye. Sio siri kwani ni jambo ambalo ameniambia mara kadhaa na hata kuna wakati nimemfumania akitumbuiza dume nyumbani kwetu, na hakuna wakati ambapo nimezua kizaazaa wala kukorofishana naye. Badala yake, kutokana na sababu kuwa nampenda, nimeamua kuhakikisha kwamba wakati huu wote yeye yuko salama. Ndiposa nimejipa jukumu kuhakikisha kwamba nyumbani mwangu kondomu hazikosi. Wengi wanadhani kwamba mimi ni bwege kwa uamuzi huu, lakini mimi ni mstaarabu na ni binadamu. Naelewa kwamba inachosha kula chakula kimoja kila siku na huenda hii ndiyo sababu inamfanya kusaka ladha zingine huko nje. Kwangu mradi anahakikisha haniletei maradhi, basi sina tatizo. Nashauri wanaume wengine pia kufuata mkondo huu badala ya kuingiwa na hasira za kipumbavu kila wanapogundua kwamba wake zao wanasakata mechi za ugenini kiasi cha kuuana. Aisee, kiungo hicho huwezi kukila ukakimaliza. Kubali usaidizi!”