Makala

FUNGUKA: Bila vipodozi 'sijaumbika'

May 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KUNA baadhi ya wanaume ambao mojawapo ya mambo kuhusu wanawake yanayowachukiza ni kutumia vipodozi kwa wingi.

Basi ikiwa wewe ni mmoja wao, bila shaka Mya hawezi kukuvutia.

Binti huyu mwenye miaka 30 ni mkazi wa jiji la Nairobi na mhudumu katika mojawapo ya benki maarufu nchini.

Ameolewa na pamoja na mumewe, Jose, mfanyabiashara maarufu jijni Nairobi, wamejaliwa watoto watatu.

Unapomtazama Mya ni vigumu kuamini kwamba ni mama wa watoto watatu.

Sio tu kutokana na umbo ambalo amefanikiwa kulidumisha licha ya kushika mimba mara tatu, bali pia mavazi ambayo hukumbatia vyema umbo lake la chupa na kumfanya kuvutia umati kila anapopita.

Lakini sio hilo umbo tu linalowaacha madume wakipinda shingo, bali pia vipodozi vyake ambavyo kila mara huonekana maridadi. Kutoka kwa wanja, hadi kwa lipstiki, hakuna wakati hata mmoja ambapo unaweza kutana naye uso wake ukiwa mkavu.

“Kila mara uso wangu ni mkamilifu, iwe ni asubuhi ninapowasili kazini, baada ya kula chakula cha mchana, au jioni ninapofunganya virago na kurejea nyumbani.

Ukamilifu huu pia uko nyumbani. Vipodozi vyangu viko ngangari kila mahali. Mimi hutumia vipodozi hata nikienda kulala na kwa miaka sita ambayo nimekuwa pamoja na mume wangu, kamwe hajawahi kuniona bila vipodozi.

Ili kudumisha mwonekano huu, kila kona kuna vipodozi, iwe kwenye choo, chumbani mwangu na mume wangu, kwenye mkoba wangu na hata katika dawati langu kazini. Hii ni hatua ambayo nimechukua kuhakikisha kwamba hakuna wakati hata mmoja sipendezi.

Ninapowasili nyumbani kutoka kazini, mara nyingi mume wangu huwa hajafika. Huelekea bafu kuoga na baadaye kujipaka upya vipodozi ili anaporejea atanipata nikiwa nang’aa.

Pia, kabla niende kulala, lazima niende msalani kuhakikisha kwamba vipo shwari.

Isitoshe, kila wakati nikiamka katikati ya usiku kwenda msalani au kupata angaa glasi ya maji, lazima niende kwenye kioo kuhakikisha kuwa uso wangu unapendeza.

Asubuhi, nahakikisha kwamba narauka kabla ya mume wangu, naingia bafu na kujiandaa.

Nimewekeza pesa nyingi katika kutafuta na kununua vipodozi vya kisasa na vya ubora wa hali uya juu. Mimi huwa situmii vipodozi hivi vya kawaida vinavyopatikana hata vichochoroni.

Kila wakati mimi hufanya utafiti kujua ikiwa kuna aina mpya ya vipodozi kwenye soko, na kuna wakati ambapo nalazamika kuagiza bidhaa hizi kutoka ng’ambo au hata mimi mwenyewe kusafiri kwenda kujiletea.

Matumizi ya vipodozi vingi hakujanizuia kudumisha usafi hasa wa malazi yangu na mume wangu, kwani kwenye kitanda chetu sisi hutumia shiti na mifarishi mieupe, hivyo lazima nizibadilishe kila siku”.