Makala

FUNGUKA: 'Mimi nyani mwenda pweke…'

November 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

WANASEMA kwamba binadamu kamwe hawezi kuishi kama kisiwa, kumaanisha kwamba lazima uwe na uhusiano na wenzako.

Ingawa hivyo, kwa Jelly mambo ni tofauti kabisa kwani kwa miaka sasa, binti huyu amejitahidi kuishi maisha yake kivyake.

Jelly ana miaka 35 na ni meneja wa mauzo katika shirika moja jijini Nairobi. Kutokana na kazi yake, ana mshahara mzuri na hivyo anaweza kujikimu kimaisha.

Anamiliki nyumba katika mojawapo ya mitaa ya kifahari jijini. Pia, ana magari kadha. Mbali na hayo, anaweza kumudu kwenda likizo nje ya Kenya mara kadha kwa mwaka.

Kimaumbile, pia yeye ni mrembo. Uso mpana, macho ya gololi, ngozi nyororo na mdomo mnene, vilevile umbo lake la chupa, ni sifa ambazo zimemfanya kuwa kivutio ambapo kila anapotembea anawaacha madume wengi wakidondokwa mate.

Lakini ni kivutio ambacho hutokomea pindi unapopata fursa ya kumjua vyema.

“Mimi sipendi uhusiano wowote ndiposa nimeamua kwamba sitawahi kuolewa wala kupata mtoto. Nafurahia upweke wangu kiasi kwamba sitaki mgusano na mtu yeyote.

Ndiposa nimenunua gari ili nikitaka kusafiri, sina haja kusongamana na wengine kwenye magari ya umma au kuomba lifti. Isitoshe, sibebi mtu kwenye gari langu. Ikinibidi kuabiri matatu au gari la umma, nalipia viti viwili ili nisiwe na jirani.

Kuna wakati ambapo gari langu liliharibika na hivyo nikalazimika kuabiri matatu. Nilinunua viti sita; kimoja kando yangu, viwili nyuma yangu na viwili mbele yangu, ili kuepuka mgusano wowote na binadamu. Na baada ya gari hilo kufika kituo cha mwisho, ilinibidi nisubiri kila mtu adondoke ili nami nipate nafasi ya kuondoka bila bughudha.

Mkahawani pia mimi hukaa peke yangu kwenye meza ambapo kiti kimoja ni cha begi langu na hakuna anayekaribishwa karibu nami hata katika baa.

Aidha, mara kwa mara mimi husafiri nje ya Kenya ambapo sharti nisafiri kwa ndege na huhakikisha nimenunua tiketi ya kiti mkabala wangu ili nisikaribie yeyote.

Kabla ya kununua nyumba yangu, nilikuwa nimekodisha fleti moja ambapo ilinibidi kukodisha pia nyumba iliyokuwa kando yangu kupunguza mgusano na majirani.

Siwezi kuwa na mchumba wala mume kwani uhusiano utanilazimu mara nyingi kuwa karibu na mtu.

Kazini nina afisi kubwa kumaanisha kwamba mgusano na wafanyakazi wengine ni mchache. Mikutano yetu mingi hufanyika kupitia jukwaa la mtandaoni la Skype, na pengine unajiuliza ni vipi nimeweza kuhifadhi wadhifa wangu licha ya kutokuwa na uhusiano na wafanyakazi wenzangu?

Mimi ni mchapakazi ambapo katika kipindi changu katika wadhifa huu, kampuni yetu imekuwa ikiunda faida tele, na hivyo naamini kwamba ni wachache wanaoweza jaza pengo langu”.