FUNGUKA: 'Mke wa mtu raha tupu'
Na PAULINE ONGAJI
MANU ni mwanamume mwenye umri wa miaka 42 ambaye ameoa na kutalikiana mara tano, suala ambalo limemfanya kuwakataa kina dada wabichiwabichi ambao hawajaolewa na badala yake kuwachangamkia wake za watu.
Kwanza kabisa Manu ni mfanyabiashara shupavu ambapo anamiliki maduka kadha ya ujumla katika miji tofauti humu nchini.
Tayari ana watoto sita kutoka kwa wanawake tofauti lakini asema hayuko tayari kuwapa mama kwani anaamini kwamba wanawake hawaaminiki.
Tangu kuvunjika kwa ndoa yake ya mwisho miaka minne iliyopita, tayari ashachumbia wanawake zaidi ya ishirini, wote wake za watu.
Baada ya talaka yake ya mwisho na pia kuwasikia marafiki zake wakilalama kila mara kuhusu udanganyifu wa wake zao, aliamua kupoteza imani na wanawake na sasa anaamini kwamba ni kawaida kwa wanawake kudanganya.
“Ni sababu hii ambayo imeelekeza hamu yangu kwa wake za watu hasa waliofunga pingu za maisha na kuhalalisha uhusiano wao.
Hakuna umri ninaolenga hasa kwani uwe na umri wa miaka baina ya 20, 30, au 90, mradi una mume, basi umefuzu kuwa windo langu.
Sifanyi hivi kuharibu nyumba za watu ila nawaendea wake za watu kwani wanawake hawaaminiki na hivyo hata nikishiriki mapenzi na mmoja leo, yeye sio wangu kumaanisha kuwa sitahisi uchungu kwani atarejea kwa mumewe.
Sina muda wa mabinti ambao hawajaolewa kwani kwa kawaida watakuja na matumaini ya kugeuza raha yetu ya muda kuwa uhusiano wa kudumu. Nafasi yangu ni kwa mabinti wanaonionjesha asali na kwenda zao.
Ninapoanza kumvizia mke wa mtu, hakuna kudanganyana kuwa raha hii ya muda itageuka na kuwa penzi la kudumu kwani najua kuwa mwishowe atamwendea mumewe, nami nitarejea kwangu bila mzigo wa kuwepo na mwunganisho wowote.
Uhusiano wangu na wake za watu hautababaisha bora tu mwenzangu anataka uhondo pekee.
Nina haja na kukata kiu pekee kwa hivyo ujumbe wangu kwa waume ni kwamba hawapaswi kuingiwa na wasiwasi kwani nikishatosheka, sina haja na mkeo tena. Kwa hivyo sina nia ya kukupokonya jiko lako.
Lakini mambo huwa sio shwari kila mara kwani kuna baadhi wanaonionjesha na kutaka kuendelea na uhusiano nami.
Hasa nakumbuka kisa cha binti moja ambaye baada ya kuzubaishwa na penzi nililompa, nusura atake kumuacha mumewe ili aje kuishi nami. Lakini nilimkanya vilivyo kabla ya kumtema na ku-block namba yake.
Mimi hufurahia ngoma tu lakini ninaposhuku kana kwamba unaanza kuvutiwa nami, nitakutema haraka upesi.
Naamini kuwa wanawake kamwe hawaaminiki na mwanamume mmoja hawezi zima moto wao ndiposa sitaki kuwa huyo mwanamume anayechezewa shere na mkewe anayetafunwa na kila mtu huko nje.
Ushauri wangu kwa madume wenzangu ni kukaa chonjo na kutozubaishwa na wake zao ilhali huko nje wanagawa asali kwa kila aliye na tamaa ya kuonja. Pia wao wajikakamue na kuanza kuwachangamkia wake za watu”.