Makala

FUNGUKA: 'Nabadilisha waume za watu kama chupi’

February 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

Kwa ufupi:

  • Navutiwa na wanaume waliooa zaidi ya akina kaka ambao hawana wake
  • Ili kufuzu lazima uwe mume wa mtu ambapo sibagui umri. Lazima pia uwe umeoa kwa angaa miaka mitano
  • Uhusiano wangu na waume za watu hauna mambo mengi na ikiwa kuna kaka anayetaka uhusiano wa pembeni, basi hakuna mtu anayefaa kama mimi
  • Baada ya kumzaa mwanangu wa kwanza ndipo nilitambua tabia za mume wangu nilipomfumania na kahaba chumbani mwetu

KUNA baadhi ya watu wanaoamini kuwa ili kuwa mkamilifu hasa kama mwanamke, basi lazima uwe umeolewa.

Lakini kwa Jacinta, 36, hizo ni ngano. Kwa mama huyu wa watoto wawili na ambaye ametaliki mara mbili, ndoa ni ndoto na kamwe haiwezi kudumu.

Bibi huyu ni meneja katika kiwanda cha kuoka mikate katika eneo la viwandani jijini Nairobi. Kwa sasa yuko katika uhusiano wake wa 11, mwaka mmoja baada ya kumtaliki mumewe.

Suala linalofanya hadithi yake kushangaza ni kuwa licha ya kuwa ameamua kuwa kamwe hatoolewa tena, anaendeleza mahusiano na wanaume kukidhi ashiki huku akiwapuuza makapera na badala yake kuwaelekezea waume za watu macho.

“Navutiwa na wanaume waliooa zaidi ya akina kaka ambao hawana wake. Ninapohusiana na wanaume waliooa nia yangu sio kuvunja ndoa ya mtu ila ni kuwa napendezwa nao.

Ili kufuzu lazima uwe mume wa mtu ambapo sibagui umri. Lazima pia uwe umeoa kwa angaa miaka mitano, suala ambalo lazima niulize tunapokutana. Sina haja na fedha zako. Suala la fedha sio muhimu mradi ukubali ngoma bila mwunganisho.

Sina majuto yoyote ya kuwavizia waume wa watu kwani sina muda wa kuanzisha uhusiano na makapera watakaonishusha chini baada ya kuwekeza muda wangu kwao.

Naamini kuwa hakuna mwanamume mwaminifu na hivyo sina muda wa kuchumbiwa na kapera ambaye ataniahidi mambo mengi na akose kutimiza hata moja.

 

Ni burudani tu

Kwa upande mwingine ninapoanzisha uhusiano na mume wa mtu, hakuna matumaini ya kuwa uhusiano huu utaimarika na kuwa ndoa na najua kwamba baada ya burudani nitarudi nyumbani pasipo kuwa na matumaini ya mwunganisho wowote.

Uhusiano wangu na waume za watu hauna mambo mengi na ikiwa kuna kaka anayetaka uhusiano wa pembeni, basi hakuna mtu anayefaa kama mimi.

Ukiwa mwangalifu hakuna hatari kwamba mkeo atajua, kwani tofauti na vimada wengine wanaotaka kuchukua nafasi ya mkeo mnapoanza uhusiano, mimi sina haja. Sitaki uhusiano wala kuzaa mtoto nawe.

Niliingia katika uhusiano wangu wa kwanza nikiwa na miaka 15 ambapo nilichumbiwa na mwanariadha wa miaka 21.

Mwanzoni nilifurahia uhusiano huo lakini nilipigwa na butwaa nilipomfumania peupe akirina asali ya binti fulani chumbani mwetu.

Nilipotimu miaka 18 nilikutana na mume wangu wa kwanza ambaye wakati huo alikuwa na miaka 37.

 

Kahaba chumbani

Baada ya kumzaa mwanangu wa kwanza ndipo nilitambua tabia zake nilipomfumania na kahaba chumbani mwetu, suala lililopelekea ndoa yetu kuvunjika mwaka wa 2002.

Lakini miaka miwili baadaye nilikutana na mwanamume wa miaka 38 ambaye alikuwa akihudumu kama mkurugenzi wa kampuni fulani na nikadhani kuwa wakati huu mambo yatakuwa tofauti.

Baada ya kuzaliwa kwa mwanangu wa pili miaka minne baadaye, tabia ya mume wangu ilibadilika ambapo ilikuwa kawaida kukutana na kondomu mifukoni mwake.

Hata hivyo baada ya kuvumilia kwa miaka niliamua kushika hamsini zangu mwaka jana. Mambo ambayo nimeptia katika mahusiano yalinifanya kuchukua uamuzi huu.”