Makala

FUNGUKA: 'Nywele bandia hawesmake…'

August 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KUSEMA kweli nywele za kubandika zimekuwa mwokozi kwa mabinti wengi kwani mbali na kufanya iwe rahisi kudumisha mwonekano, pia zinasaidia nywele halisi kukua.

Hata hivyo kwa wanaume wengi, nywele hizi zimekuwa kero ambapo idadi kubwa ya ndugu zetu hawazifurahii kamwe.

Leyton, 42, ni mmoja wao. Ni mfanyabiashara hodari katika mojawapo ya miji mikuu nchini.

Kwa sasa, ana watoto watatu kutoka kwa wanawake wawili tofauti, lakini hajafanikiwa kuwa na mke.

Japo ana pesa na pia kimaumbile kabarikiwa, kutokana na chuki yake isiyo ya kawaida kwa nywele hizi, imekuwa vigumu kudumisha uhusiano wa kimapenzi.

Leyton kamwe hataki kujihusisha na binti ambaye huweka nywele zozote za ziada kichwani. Iwe za kusonga, kusokota au zile za kubandika. Msimamo wake maishani ni kwamba kila kitu mwilini kinapaswa kuwa halisi.

“Nywele hizi zinanikera kiasi kwamba kwa mara ya kwanza nikikutana nawe na umezisonga, basi umepoteza alama na hata iwapo kidogo ulikuwa unafurahisha macho, hamu kwako inakwisha.

Ukiwa mpenzi wangu, basi unapaswa kuhakikisha kwamba hakuna wakati hata mmoja utazisonga, kwani hiyo siku utakapofanya hivyo, basi utakuwa mwisho wangu nawe.

Tangu nilipoanza kujihusisha katika mahusiano, kamwe sijawahi kumchumbia binti anayesonga hizi nywele, na pindi unapozisonga, hata iwe nakupenda vipi, basi huo ndio mwisho wetu.

Pengine wengi watauliza kwa nini nachukia nywele hizi. Kwanza kabisa napenda binti asili, na kwangu unapozisonga, hiyo ni ishara ya ulaghai kwani huo sio mwonekano wako halisi.

Pili, nahusisha nywele hizi na uchafu. Kwa nini nasema hivi? Mara nyingi mabinti wanaposonga hizi nywele, wanaweza kuchukua mwezi mmoja au hata miwili kabla ya sehemu hii ya mwili kusafishwa, suala linaloacha uchafu mwingi na harufu mbaya.

Kwa upande wangu nafurahia mwanamke nimpendaye kuosha kichwa chake angalau mara mbili kwa siku kama mbinu ya kukabiliana na mkusanyiko wa jasho na uchafu.

Isitoshe, wakati wa mahaba nataka kumgusa binti kila sehemu kichwani, jambo ambalo siwezi kufanya ukiwa na hizo za kubandika.

Jambo linalonikera pia ni kwamba mabinti wengi hutumia maelfu ya pesa kununua nywele hizi. Binti anatumia shilingi elfu hamsini kwa nywele? Kwangu hiyo hawesmake!

Siko tayari kukupa hizo pesa, afadhali uniitishe fedha za kuanzisha biashara au kujiendeleza kimasomo, lakini sio katika masuala ya kipuuzi kama nywele hizi. Hata kama sio mie ninayekupa hizo pesa, nina uhakika kwamba waweza kuzitumia kujiimarisha kimaisha.

Kwa sasa niko katika uhusiano wangu wa 11 mwaka huu, na japo imekuwa changamoto kumpata binti atakayekubaliana vilivyo na vigezo vyangu, sina nia ya kulegeza kamba”.