FUNGUKA: Sirejelei chupi, mara moja tu naitupa
Na Pauline Ongaji
Mara nyingi usafi wa mwili na hasa wa nguo za ndani huhusishwa na wanawake huku wanaume wakitarajiwa kutotilia maanani sana suala hili. Yamkini, kuna wanaume ambao huvalia suruali za ndani mara kadha kabla ya kubadilisha.
Lakini kwa Musa mambo ni tofauti kabisa. Kaka huyu anaenzi sana usafi kiasi ambacho kulingana na wenzake sio cha kawaida.
Musa ambaye ni mfanyabiashara mashuhuri jijini Nairobi anasisitiza kwamba kwake, usafi ni muhimu sana kiasi cha kuwa kwa kawaida havalii suruali ya ndani zaidi ya mara moja. Kila anapobadilisha chupi yeye hutupa iliyochafuka:
“Siwezi kuvalia suruali ya ndani zaidi ya mara moja kumaanisha kwamba kwa kawaida sifui chupi eti niivalie wakati mwingine. Kila ninapoivalia na kuivua, haina umuhimu kwangu huku masuala ya usafi vile vile kujipenda, yakifanya kutofikiria kutovalia vazi hili zaidi ya mara moja hata lifuliwe.
Sehemu nyeti huwa na uchafu mwingi hasa baada ya masaa kadha. Uchafu huu unaweza kusababisha maambukizi iwapo nitasafisha kwa kawaida na kurudia kuvalia hiyo chupi.
Kila mara napenda kuhisi msafi na kunukia vizuri kila siku. Naamini kwamba uchafu mwingi unaojirundika katika sehemu hii unaweza kusababisha maambukizi na harufu mbaya.
Aidha, tokea zamani mamangu alinifunza kwamba ni ishara ya uchafu kurudia kuvalia chupi hata baada ya kuisafisha.
“Chupi ni vazi la kuvaliwa mara moja na kutupwa na kuvalia nyingine mpya,” alisema.
Lakini haijakuwa rahisi kwani maisha ya aina hii yanahitaji mfuko mzito. Mapato yangu yananiwezesha kumudu maisha haya kwani kwangu pesa sio tatizo.
Kwa hivyo kila mwezi naagiza chupi mpya kutoka ng’ambo na hakuna chupi yangu ninayonunua kwa chini ya Sh2000, hivyo mimi hutumia kiwango hiki cha pesa kila siku kwa chupi pekee.
Nimetengea asilimia fulani ya pesa zangu kugharimia ununuzi wa chupi pekee. Sio hayo tu. Hata ukiwa mpenzi wangu, lazima uwe tayari kubadilisha chupi na kuzitupa kila siku, la sivyo hakuna uwezekano wetu kuwa pamoja. Lazima uwe unabadilisha chupi kila siku na kutupa uliyovalia awali. Ikiwa hauwezi kumudu haya maisha, niko tayari kukufadhili, la sivyo ushike njia.
Mbali na kifedha, maisha haya yamenigharimu kimapenzi. Kwa sasa sina mpenzi na imekuwa vigumu kudumisha uhusiano kwani mabinti wengi ninaokutana nao hudhani kwamba mimi ni wazimu wanapogundua kuhusu maisha yangu.
Hivi majuzi nilikuwa na mpenzi ambaye pia nilikuwa nimeanza kumfunza haya kwani nilikuwa namlazimu kutupa chupi yake pindi anapoivaa. Japo nilikuwa nimeahidi kufadhili maisha haya, hatimaye aliniacha.
Hata hivyo, hayo hayatanifanya nilegeze kamba kuhusu tabia hii ambayo ningependa iigwe na watu wengine sio tu kama mbinu ya kukabiliana na maambukizi yanayotokana na uchafu wa sehemu za nyeti, bali pia kama njia ya kudumisha usafi wa mwili.”