Gachagua sasa abuni mkakati mpya, ajipanga chini ya maji
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ameamua kutulia kujipanga upya kisiasa kufuatia kuondolewa kwake ofisini hivi majuzi.
Washirika wake wa karibu wanafichua kuwa kimya chake ni cha kimkakati huku akiendelea kujipanga upya.
Bw Gachagua mwenyewe amethibitisha kwamba ameamua kutulia kisiasa ili kujipatia wakati wa kupata nguvu mpya
Akiwa hatarini kupigwa marufuku kushikilia wadhifa wa umma iwapo mahakama itaunga mkono kuondolewa kwake, Bw Gachagua anaripotiwa kulenga kuwa kigogo au kuwaunga vigogo wa kisiasa.
‘Tunashinikiza kuondolewa kwa mashtaka,hatua ambayo itamsafisha kuwania wadhifa wa umma 2027. Hiyo ndiyo ajenda inayotarajiwa,’ alisema diwani wa Baragwi David Mathenge.
Bw Mathenge ndiye mwakilishi wa wadi ya Kaunti ya Kirinyaga ambaye alifanikiwa kupata agizo katika mahakama ya Kerugoya kuzuia kuapishwa kwa Prof Kithure Kindiki.
Kwa sababu kesi ambazo amewasilisha kupinga kushtakiwa kwake zimepangwa kusikizwa Januari mwaka ujao, alisema, ‘inatupa muda wa kupumzika na kujipanga kwa mapambano’.
Tayari, Bw Gachagua ametangaza kwamba hatasalimu amri, hataenda popote na atakuwa na nguvu 2027.
“Tutulie, tudumishe amani…tuwe na subira. Wakati unakuja hivi karibuni. Tutalipiza kisasi kwa wakati ufaao. Wakati huo hauko mbali. Nitarejea kutoa mwelekeo tutakaochukua,” Bw Gachagua alisema hivi majuzi akiwa Kaunti ya Kiambu.
Sababu nyingine inayoripotiwa kumfanya Bw Gachagua kutulia ni kuzima hisia.
Kulingana na Seneta wa Nyandarua John Methu, hali ya wasiwasi ambayo imekumba wapiga kura wa eneo la Mlima Kenya ni hatari ikiwa haitasimamiwa vyema.
‘Kuna hasira kali,’ alisema. “Unahitaji tu kutembelea majukwaa ya mitandao ya kijamii ya vituo vya habari vya Mt Kenya na kupitia maoni. Hisia za kumuunga mkono Gachagua lazima zidhibitiwe kwa uwajibikaji”.
‘Hii ndiyo sababu Gachagua, akiwa katika Kaunti ya Kiambu, aliomba amani, na kuwataka watu wanaomuunga mkono kutulia na badala yake wasubiri 2027 kueleza hisia zao,’ aliongeza.
Zaidi ya hayo, Bw Gachagua anasemekana kuwapa kazi washauri wake wa kisiasa kwanza kuchanganua ushindani ambao unaelekea kuchipuka huku mirengo ikiibuka katika Mlima Kenya na nchi kwa jumla.
Huku eneo la Mlima Kenya ambalo sasa linaonekana kukubaliana kwa kauli moja kwamba lilikuwa kosa kubwa kuingia katika Muungano wa Kenya Kwanza bila chama chake cha kisiasa, Bw Gachagua anasemekana kuwa na nia ya kujipanga kwanza na chama kwa ajili ya 2027.
Mmoja wa viongozi washirika wake eneo la Kati, Bw Mwangi Kibeti, aliambia Taifa Leo: ‘Tunataka kujipanga vyema, kuona jinsi tunavyoweza kusimamia vyema maslahi makubwa ambayo Gachagua anawakilisha akiwa nahodha wa meli 2027.’
Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa alisema kuna uwezekano wa Bw Gachagua kuungana na maeneo mingine ili kuongeza nafasi ya kufaulu.
Alisema kuna uwezekano kuwa Bw Gachagua ataungana na viongozi wakuu kutoka kote nchini kuwa na kikosi kikali ambacho kinaweza kushinda.
“Tuna marafiki, nao ni wengi. Wako tayari kuungana nasi na hilo linahitaji muda na mkakati. Rais Ruto alianza kujipanga dhidi ya bosi wake Uhuru Kenyatta mnamo 2013 na alikuwa na miaka 10 ya kujipanga. Tuna miaka miwili pekee,” alisema.
IMETAFSIRIWA Na BENSON MATHEKA