Makala

Gavana Sakaja ameshindwa kuhudumia wakazi wa Nairobi ahadi zake zikisalia kuwa hewa?

Na WINNIE ONYANDO December 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

ALIPOKUWA akiapishwa Agosti 25, 2022, katika Jumba la Mikutano la KICC, Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, alitoa ahadi kadhaa zilizolenga kuboresha kuboresha maisha ya wakazi wa jiji.

Hata hivyo, baadhi ya ahadi hizo, ambazo ziliwavutia wapigakura na kumpa ushindi kupitia tikiti ya United Democratic Alliance (UDA), bado hazijatimizwa.

Ni zaidi ya miaka miwili sasa tangu Gavana Sakaja alipochukua hatamu za uongozi, lakini changamoto zilizokuwa zikikumba wakazi wa Nairobi bado zipo, na hata zinaonekana kuzidi kuwa mbaya.

Baadhi ya ahadi alizotoa Bw Sakaja ambazo bado hazijatimizwa ni:

Kujenga mji unaoleta matumaini

Wakati wa kampeni, Bw Sakaja alijipigia debe huku akiahidi kuifanya Nairobi kuwa ‘mji unaoleta matumaini.’

Wakati huo, mwanasiasa huyo alitumia maneno ya kuvutia akisema kuwa kila Mkenya anahitaji nafasi ya kuendesha maisha yake kwa amani, kujipatia riziki, na kuhakikisha mustakabali wa watoto wake unatimizwa.

Katika manifesto yake, aliahidi kubadilisha sura ya Nairobi kuwa mji wa mpangilio, heshima, na mji unaotoa fursa kwa wote.

Alisema serikali ya kaunti itahakikisha wakazi wote wanaheshimiwa na kupewa huduma sawa kwa utu na heshima.

Hata hivyo, hii inaonekana kuwa ndoto ya mchana kwani baadhi ya wakazi wa jiji bado wanakumbwa na changamoto kama vile kupata huduma duni kutoka kwa kaunti.

Kujenga reli ya gari moshi la abiria jijini

Mojawapo ya ahadi kubwa alizotoa Bw Sakaja ilikuwa kujenga reli ya gari moshi la abiria jijini ili kupunguza msongamano katikati mwa jiji na kuboresha sekta ya uchukuzi wa umma.

Aliahidi kwamba mradi huu ungeleta heshima na unadhifu katika sekta ya uchukuzi wa umma.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye, hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kutekeleza mradi huu.

Wakazi wa Nairobi wanaendelea kutumia muda mwingi barabarani kutokana na msongamano mkubwa wa magari.

Kuifanya Nairobi kuwa safi

Najua hata wewe unashangaa sana ukitembea katikati mwa jiji la Nairobi.

Kila mahali kuna taka. Katika baadhi ya mitaa, kuna mlima wa taka zilizotapakaa kila mahali.

Wakati wa kampeni, mwanasiasa huyo aliahidi kuweka mfumo wa kushughulikia suala la kukusanya na kutupa taka ili kuhakikisha mji unakuwa safi.

Katika manifesto yake, alieleza kuwa serikali yake ingeanzisha miradi ya maji taka ili kuzuia mifereji ya maji taka kumwagika mitaani.

Hata hivyo, najua hata katika mtaa wako, huwezi kosa mfereji wa majitaka.

Hii inaonyesha kuwa hali ya usafi katika sehemu nyingi za Nairobi bado ni mbaya.

Takataka zinaendelea kurundika mitaani, na maeneo mengi ya jiji yamejaa harufu mbaya inayotokana na mifereji ya maji taka iliyoziba.

Hii ilimfanya Rais William Ruto mnamo Septemba 2024 kuulenga utawala wa Bw Sakaja, akisema kuwa uchafu ambao umekuwa ukishihudiwa jijini Nairobi ni wa kuaibisha nchi.

Rais Ruto ambaye alikuwa akizungumza katika Mkutano na Maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO), alisema juhudi zinahitajika kuhakikisha jiji la Nairobi ni safi na pia Mto Nairobi unasafishwa na kurejeshewa hadhi yake.

“Nairobi ni jiji letu na ndiyo sura ya Kenya na inafanya wale ambao wanatutembelea wawe na dhana kuhusu taifa letu. Hatuwezi kuendelea hivi na tuambiane ukweli,” akasema Dkt Ruto.

“Ukipita kila mahali unapata uchafu, mabomba ya maji taka, mifuko ya plastiki na sasa hata viwanda vinaachia uchafu na kuuelekeza jijini,” akaongeza.

Kutatua changamoto ya maji

Novemba 25, 2024, wafanyakazi wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Nairobi (NCWSC) walitishia kugoma.

Wafanyikazi hao walitishia kusitisha shughuli zao iwapo Bunge la Kaunti ya Nairobi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei wangeshindwa kumzuia mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo ya maji kuongeza muda wake mamlakani.

Muungano wa Wafanyakazi wa Maji na Maji Taka nchini (Kuwase) ulidai kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NCWSC Nahashon Muguna anataka kuendelea kushikilia wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitatu kinyume na sheria.

Hii ingefanya wakazi wa Nairobi kukosa maji ambayo ni ya maana sana katika maisha ya kila siku.

Kando na hayo, kumekuwa na changamoto ya maji safi katika baadhi ya mitaa jijini, jambo ambalo Bw Sakaja aliahidi kushughulikia wakati wa kampeni.

Hata hivyo, sehemu nyingi za Nairobi bado zinakumbwa na tatizo la upatikanaji wa maji.

Wakazi wanalazimika kununua maji kwa bei ya juu kutoka kwa wasambazaji wa maji wa kibinafsi, huku baadhi ya maeneo kama vile Huruma yakikosa maji kwa wiki au hata miezi.

Kuwahamisha wachuuzi

Utawala wa Gavana Sakaja umekuwa ukikashifiwa kwa kuwa na mpangilio mbaya wa jiji huku wachuuzi wakiwa wamejaa kila mahali na kufika hata katikati mwa jiji.

Kwa sasa, unapotembea katikati mwa jiji hasa jioni, unashindwa hata mahali pa kukanyaga kwani wachuuzi wametandika bidhaa zao kila mahali.

Baadhi yao, unapotofautiana nao huzua fujo na hata vita.

Hii inaleta msongamano mkubwa jijini jambo ambalo pia linachangia uchafu.

Japo kuahidi mara kadhaa kuwahamisha wachuuzi, Bw Sakaja anaoenekana kuzidiwa nguvu.

Naibu Rais aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua alitofautiana pakubwa na Sakaja kuhusu hoja ya kuondoa wachuuzi Jijini.

Mbali na kutotimiza ahadi hizi kuu, wakazi wa Nairobi bado wanakumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo huduma duni za afya, ukosefu wa usalama na ukosefu wa nafasi za kazi.

Hii imewafanya baadhi ya wakazi kuanza kupoteza matumaini katika uongozi wa Sakaja.

Kwa mfano, hospitali za umma zinakosa dawa na vifaa vya kutosha, hali inayosababisha wagonjwa wengi kutafuta huduma katika hospitali za kibinafsi kwa gharama ya juu.

Kwa sasa, wakazi wa jiji wanaendelea kusubiri kwa matumaini huku wakihofia kwamba ahadi za kampeni zitatimia tu kwa nadharia, si kwa vitendo.