Makala

Gen Z: Jinsi tunavyomkumbuka Raila

Na WINNIE ONYANDO October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAARIFA za kifo cha Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Amolo Odinga, maarufu kama Baba, zilitanda kote nchini Jumatano asubuhi huku mamia wakijitokeza kumuomboleza shujaa huyo.

Kilio, simanzi na mshtuko vilitanda kila mahali — kutoka mitaa ya Nairobi iliyojaa makelele ya matatu hadi fukwe tulivu za Ziwa Victoria.

Wakenya walipigwa na butwaa, wakitafakari maisha ya mtu ambaye alitambulika kama kigogo katika masuala ya siasa nchini.

Kwa zaidi ya miongo minne, Raila alikuwa kigogo wa siasa za Kenya. Alipendwa, alipingwa, lakini hakuwahi kupuuzwa.

Kwa wengi, alikuwa ishara ya ujasiri, demokrasia na imani kwamba Kenya inaweza kuwa bora.

Paul Ochieng Ouma Gen-Z Nairobi anasema kuwa anamkumbuka B w Odinga kwani alikuwa kiongozi aliyependa kuwaungansha Wakenya.

Paul Ochieng Ouma anasema Raila aliwaunganisha Wakenya. PICHA | WINNIE ONYANDO.

“Raila alikuwa mtu wa kuunganisha Wakenya. Uamuzi wake wa kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza ulikuwa njia ya kutuliza hali ya nchi baada ya maandamano ya Gen Z. Alihakikisha amani na umoja ndani ya ODM na nchi kwa jumla. Huu ndio wakati ambao sisi kama vijana na kama taifa, tunapaswa kubaki pamoja na tusubiri mwelekeo kutoka kwa viongozi wetu. Raila alifariki akiwa serikalini, hivyo jukumu ni letu kuendeleza pale alipoachia.”

Kwa Paul, hatua hiyo haikuwa udhaifu, bali hekima ya uongozi. “Alitaka amani idumu nchini baada ya maandamano,” anasema. “Alijua hakuna maendeleo bila umoja.”

Kwa vijana wengi, Raila hakuwa tu mwanasiasa, bali kiongozi wa taifa ambaye alileta matumaini mapya.

“Raila alikuwa mtu mwenye heshima na aliyepigania haki zetu,” anasema Kevin Otieno, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kevin Otieno, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema Raila alipigania haki za Gen-Z. PICHA | WINNIE ONYANDO.

“Aliwapigania vijana kama sisi, hasa kizazi cha Gen Z. Nakumbuka jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kwenye maandamano kupinga maamuzi yasiyofaa ya serikali. Alisimama nasi — si kwa maneno pekee bali kwa matendo.”

Kwa Kevin, kifo cha Raila ni pigo kubwa kwa vijana.

“Sasa tuna hofu,” anasema. “Tulikuwa tukimtegemea kutetea sauti zetu. Bila yeye, hatujui mustakabali wetu utakuwaje.”

Kwa upande wake, Maxwel Kabaka anakumbuka maneno ya Raila ambayo sasa yanaonekana kama unabii.

Maxwel Kabaka roho ya Raila Odinga ya ukombozi itabaki daima. PICHA| WINNIE ONYANDO.

“Hii ni siku ya huzuni sana,” anasema.

“Nakumbuka Raila aliwahi kusema kwamba hataishi milele, lakini roho ya Raila Odinga itabaki daima. Alikuwa akimaanisha roho ya ukombozi. Ni jukumu letu sisi vijana kuendeleza mapambano pale alipoyaacha.”

Kwa Maxwel, kipaji kikubwa cha Raila kilikuwa uwezo wake wa kuhamasisha.

“Alitufanya tuamini kwamba mabadiliko yanawezekana. Alitupa matumaini kwamba mambo yangekuwa sawa siku moja.’