Makala

Gharama ya juu kutibu Saratani ingali changamoto Kenya

February 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

KATIKA duka lake la nafaka lililopo Kiganjo, Thika, Bi Ann Njeri anaonekana kama ambaye amezama katika mawazo. Si mawazo ya biashara yake inavyoendelea, ila ni kusononeka kufuatia hali ngumu anayopitia baada ya kumpoteza mume wake baada ya kuugua Saratani.

Mume wake aliaga dunia mapema 2015, na mahangaiko aliyopitia kutafuta matibabu yangali mabichi mawazoni.

Wakati huo walikuwa wakiishi Kangari, kaunti ya Murang’a na walikuwa wakisafiri kila siku asubuhi kuelekea katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH iliyoko jijini Nairobi kwa kliniki.

Licha ya kujaliwa gari la kibinafsi, gharama ya kulijaza mafuta na bili ya matibabu hawakuiepuka.

Bi Njeri alistaafu uuguzi ili kufanya biashara na kilimo, ikizingatiwa kwamba Murang’a ni mojawapo ya kaunti tajika nchini katika ukuzaji wa majani chai na kahawa.

“Kiatu usikichovalia ni vigumu kufahamu kinapobana. Nilipitia changamoto chungu nzima kutafutia mume wangu matibabu, ukosefu wa fedha ukiwa wa kwanza. Mapato tuliyopokea tuliyaelekeza hospitalini,” asema Bi Njeri.

Mume wake aligundulika kuugua Saratani ya koo mwaka 2013; na anasema ilikuwa imekomaa kiasi cha kutoweza kudhibitika.

Madaktari wanafafanua ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa ikiwa utagunduliwa mapema, hasa kabla ya seli zake kusambaa mwilini.

Chemotherapy na Radiotherapy ni baadhi ya matibabu anayopitia mgonjwa ili kudhibiti ukuaji wa chembechembe au seli zinazosababisha ugonjwa huu.

Ni hatua ghali, pamoja na dawa anazopaswa kunywa mwathiriwa.

Mtambo wa kisasa

Radiotherapy ni matibabu kwa njia ya mtambo wa kisasa unaotoa miale ya X-Ray kuua seli zinazosambaza Saratani.

Aidha, ni hospitali na zahanati chache mno nchini zenye huduma hizi. Wenye uwezo kifedha husafiri mataifa ya ughaibuni kama vile India, ili kupata matibabu.

Mnamo Februari 4 Kenya iliungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani 2019. Siku kama hiyo, Njeri anasema serikali inapaswa kutangamana na waathiriwa wa Saratani kwa njia moja ama nyingine kujua bayana masaibu wanayopitia. Kwa kuandaa tamasha pekee si ishara wadau wamepokea pandashuka wanazopitia, ila kuzuru wahanga hospitalini itaonesha wazi taswira iliyopo ya Saratani.

Mbali na juhudi za serikali kutafuta mwafaka wa matibabu nafuu, mama huyu anapendekeza iweke mikakati ya kuangazia janga hili katika zahanati na hospitali kule mashinani.

“Kuna waathiriwa wengi sana wa Saratani mashambani (akimaanisha mashinani), kusafiri hadi hospitali kama KNH kupata matibabu inakuwa kisunzi kwa sababu ya gharama ya usafiri na ya matibabu pia,” anasema.

Huduma za afya ziligatuliwa mwaka wa 2013, kupitia katiba ya sasa iliyoidhinishwa 2010.

KNH hushuhudia msongamano wa wagonjwa wa Saratani, Bi Njeri akieleza kuwa mwaka wa 2014 aligharamika zaidi ya Sh500,000. “Iwapo kaunti ya Murang’a ingekuwa na huduma za Saratani na wataalamu, singegharamika kiasi hicho. Mume wangu pia alipaswa kupata lishe bora, mbali na matibabu,” aeleza.

Kisa cha mama huyu ni kimoja tu kutaja, ambapo Wakenya wengi wameishia kuwa fukara kwa sababu ya kuuza mali yao ili wapendwa wao wapate matibabu. Kansa ya sehemu ya uzazi, koo, mapafu na ya damu ndio hushuhudiwa zaidi miongoni mwa wanaume.  Kwa wanawake, visa vinavyoripotiwa sana ni vya matiti na sehemu ya uzazi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka uliopita, 2018, ugonjwa huu Kenya husababisha vifo vya watu 90 kila siku. Takwimu za WHO zilifafanua kwamba jumla ya wagonjwa 32,900 hufariki kila mwaka, hii ikiwa asilimia 69 ya wanaougua.

Aidha, takwimu hizi zinaonesha kuwa mauaji ya Saratani ni mara kumi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabara. Kwa mwaka Kenya husajili visa vipya 47,887 vya waliopata ugonjwa huu, kwa siku vikikadiriwa kuwa 130.

Bw James Mwangi, ambaye ni muuguzi na mtaalamu wa masuala ya afya anasema ugonjwa huu haubagui jinsia wala miaka. Anasema kuwa ulaji wa lishe duni, vyakula vya kemikali na mazingira tata, ni baadhi tu ya visababishi vya Saratani.

“Serikali kwa ushirikiano na mashirika husika ya kuangazia janga hili yanapaswa kuongeza kasi ya hamasisho la watu kukaguliwa kiafya mara kwa mara, ili wanaopatikana na ugonjwa huu waanze matibabu mara moja kuzuia usambaaji zaidi,” anasema Bw Mwangi.

Baadhi ya waathiriwa wanaopatikana kuwa na ugonjwa huu mapema kabla seli zake hazijasambaa, hupata matibabu na kupona.

Unyanyapaa katika jamii kwa wagonjwa wa Saratani pia ni suala linalofaa kuangaziwa.