GHARAMA YA MAISHA: Bei ya stima kupanda tena huku Safaricom ikizidi kuwa ghali
VICTOR JUMA Na BENSON MATHEKA
BEI ya stima inatarajiwa kupanda tena katika juhudi za Serikali kupata Sh66 bilioni za kulipa kampuni zinazojenga viwanda vya kutoa umeme.
Hii imefichuka huku Safaricom ikitangaza kupanda kwa ada za kupiga simu kuanzia Oktoba 18, 2018.
Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumatano kuagiza Wizara ya Kawi kutafuta mbinu za kupunguza gharama ya umeme hasa kwa wafanyibiashara wadogo.
Pesa hizo zitakazoongezwa kwenye bili za stima ni za kulipa viwanda ambavyo vimepewa kandarasi za kutengeneza viwanda 12 vya kuzalisha umeme.
Baada ya kukamilika, viwanda hivyo vinatarajiwa kutoa megawati 1752. Kwa sasa Kenya ina huzalisha megawati 2,351 na ikizingatiwa mahitaji ya sasa ni megawati 1800, kiwango zaidi cha umeme ambacho raia watalipia huenda kisitumike.
Maelezo kuhusu ongezeko la ada ili kulipa kampuni hizo yamo katika ripoti ya 2018 ya Wizara ya Fedha kuhusu deni la umma.
Tayari baadhi ya viwanda ambavyo vimepewa hakikisho kuwa vitalipwa kwa jasho la mwananchi vinaendelea kujengwa na vingine havijapata wafadhili. Kiwanda cha Lamu kitatoa megawati 1050 na walipa ushuru watalipa kampuni inayokijenga ya Centum Investment Sh36.3 bilioni.
Kampuni ya Africa Geothermal nayo inapanga kujenga kiwanda chenye uwezo wa kutoa megawati 140 na Wakenya wailipa Sh7.7 bilioni, nacho kiwanda cha kutengeneza stima kutoka kwa upepo cha Kipeto kitalipiwa Sh6 bilioni.
Kiwanda cha Akiira Geo kitalipiwa Sh3.7 bilioni kwa kutengeneza megawati 70 za stima nayo kampuni ya Triumph itapokea Sh2.4 bilioni kwa megawati 82. Gulf Power itakayotoa megawati 80.3 italipwa Sh1.8 bilioni.
Viwanda vingine vitalipwa kati ya Sh1.1 bilioni na Sh1.4 bilioni kwa kutengeneza stima ya kutoka megawati 35 hadi 40. Viwanda hivi vitajiunga na vingine vinavyotengeneza umeme nchini ambavyo vinalipwa mabilioni ya pesa kila mwaka kumaanisha gharama ya stima Kenya haitashuka wakati wowote karibuni.
Serikali pia imejifunga hivi kwamba hata ikitamatisha kandarasi kati yake na kampuni hizo italazimika kulipa mabilioni ya pesa kama faini.
Baadhi ya kampuni hizo ziliweka mkataba na serikali kujikinga dhidi hatari za kisiasa.
Ripoti hiyo inasema kwamba kampuni ya kutengeneza stima nchini KenGen pia ilikuwa imeomba kujenga kiwanda kingine Olkaria kitakachotoa megawati 140 kwa gharama ya Sh7 bilioni kwa mwaka.
Serikali ilikuwa imesimamisha mpango wa nchi kuongeza kiwango cha stima hadi megawati 5000 baada ya kubainika kuwa mpango huo ungefanya nchi kuwa na stima inayozidi uwezo wake wa ukuaji wa uchumi.