Gwiji wa utangazaji Charles Omuga Kabisae aombolezwa
WAKENYA wanaombeleza kifo cha gwiji wa utangazaji wa redio, Mzee Charles Omuga Kabisae, aliyefariki dunia Agosti 11, 2025 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mzee Kabisae alikuwa mmoja wa watangazaji wa zamani wa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), na alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na sauti yake tulivu na ya heshima, hususan alipokuwa akitangaza matangazo ya vifo, misiba, na hafla za kumbukumbu.
Alianza kazi yake katika Idhaa ya Dholuo ya KBC mjini Kisumu kabla ya kuhamia katika Idhaa ya Kiswahili katikati ya miaka ya 1990, hatua iliyomletea umaarufu miongoni mwa wasikilizaji kote nchini.
Uwezo wake wa kutumia lugha kwa ustadi na weledi ulimfanya kuwa kipenzi cha wengi katika nyanja ya utangazaji wa redio.
Mzee Kabisae alikuwa mzaliwa wa Nyamasaria, Kaunti ya Kisumu, na kwa miaka mingi, alihusishwa na matangazo ya heshima na tanzia yaliyowagusa mamilioni ya Wakenya waliokuwa wakimsikiliza kila wiki kupitia redio ya taifa.
Alijulikana kwa kutoa matangazo ya vifo kwa sauti ya upole, yenye kumfariji msikilizaji, hata katika nyakati za huzuni kuu.
Katika mahojiano ya awali, Kabisae alisimulia tukio la kipekee katika maisha yake ya kazi alipolazimika kutangaza kifo cha mtu ambaye baadaye alibainika kuwa hai.
Alieleza jinsi alivyolazimika kurejea hewani kuomba msamaha kwa hadhira, tukio lililomuimarisha kama mtangazaji mwenye maadili na ujasiri wa kukubali makosa.
Mwaka 2008, alistaafu rasmi kutoka utumishi wa umma, lakini sauti yake ilibaki hai katika kumbukumbu za wengi, hasa wale waliowahi kupoteza wapendwa wao na kusikia ujumbe wa rambirambi ukisomwa naye kwa heshima isiyotikisika.
Familia yake imethibitisha kuwa mipango ya mazishi inaendelea, na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti jijini Nairobi.
Wakenya wengi wakiwemo watangazaji wenzake, viongozi wa serikali na wanahabari wameeleza masikitiko yao, wakimtaja Mzee Kabisae kuwa nguzo kuu katika historia ya utangazaji wa kitaifa.
Mzee Kabisae ataendelea kukumbukwa kwa weledi wake, sauti yake ya utulivu na mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari nchini Kenya.