GWIJI WA WIKI: Geoffrey Mung'ou
Na CHRIS ADUNGO
MSIMAMO ni mhimili wa ufanifu; usiwe bendera ya kufuata upepo.
Msimamo kuhusu yaliyo na mantiki – si upotoshi. Tabasuri na uandame mkondo wenye tija, ukupao maarifa, kisomo pia kipato!
Kulaza damu na kupenda anasa ni ubatili…ubatili wa kuhiliki, halafu majuto na vilio vya mbwa mdomo juu!
Msingi wa yote, mtegemee aliyekuhuluku (Mungu); ambaa makatazo na utii maagizo yake. Kutenda mema kwazaa mema. Kutenda mawi kwazaa mawi! Adui mpende, ila usile akupacho. Usitie fundo moyoni. Maudhi ya leo yaishe leo; ukilia leo, cheka kesho na ugange yajayo!
Huu ndio ushauri wa Bw Geoffrey Mung’ou (Simba) – mwalimu, mwanahabari, mhariri na mwandishi mbobevu wa vitabu vya Kiswahili.
Tueleze kwa ufupi kukuhusu
Maisha yangu ya awali yalikuwa ya kifaranga ambaye usingejua kwamba angekuwa jogoo. Nililelewa na wazazi wakali kama simba; waliadilisha kwa mijeledi. Nami nikajua kujituma, kuthamini utiifu, utu, bidii na ucha Mungu. Marehemu mama (mzawa wa Seguton, Baringo) hakunilea kwa mikate ya siagi. Nilikulia vijijini, kupeleka mifugo malishoni na mtoni kuwanywesha maji vilevile kuwasaidia wazazi katika kazi za shambani.
Nilichana mbuga miguu mitupu kule vijijini Elgon kama kilomita tano kila siku, kwenda na kutoka shuleni. Mwanzoni, nilijiokotaokota tu kimasomo kwa kutomakinika, sikwambii sarakasi za kila nui za utotoni. Nisingekosa ‘kumfungia mtu shule’ na kupewa noma (disk) hata mara mia kwa kuzungumza lugha ya kwanza.
Ndoto yako ya uanahabari ilianza lini?
Tangu chekechea, nilikuwa kasuku wa kuwaiga watangazaji wa ndani na nje ya nchi. Wazazi wangu walipenda sana kusikiliza habari. Hapo ndipo ndoto ya utangazaji iliponijia. Nikawa nawatumbuiza wanafunzi wenzangu kwa kuwasomea taarifa ya habari na kubadilibadili sauti iwiane na ya mtangazaji huyu au yule. Kufikia darasa la saba, nilikuwa moto wa kuotea mbali!
Ulisomea wapi?
Safari yangu ya elimu ilianzia Shule ya Msingi ya Kapsokwony, Elgon. Nilianza kujielewa kimasomo nilipofikia darasa la saba. Nikawa kidedea hadi sasa. Nilifanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya Kibuk. Nilifaulu vyema kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Cheptais, halafu Shule ya Wavulana ya Kimilili nilikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Sekondari (KCSE). Niliweka rekodi ya kupata gredi ya ‘A’ tena ya pekee katika somo la Kiswahili shuleni humo, mnamo 2001. Halafu nikajiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Shahada ya Ualimu. Lisingekuwa janga la UVIKO-19, ningehafili mwaka wa 2020 katika shahada ya uzamili, kisha nizamie uzamifu. Ndiyo mipango yangu ya mwakani, Inshallah!
Nani aliyekuchochea kujitosa katika ulingo wa uandishi wa vitabu?
Ni miaka ayami sasa tangu niotee ndoto tasnia hii; angaa nami nitie guu…nitembee mumo kwa mumo. Kwa umbuji, niibue tungo adhimu, zitue machoni pa wasomaji na kukubalika katika nyoyo zao. Nilikuwa kidato cha pili ambapo ilhamu ya kuwa mwandishi ilinijia baada ya kuisoma riwaya ya kusisimua ya ‘Siku Njema’ ya Ken Walibora (kwa mauko yale, Dayani ni mlifi!)
Mgomo wa wahadhiri uliochukua muda mrefu nilipokuwa chuoni ulinipa fursa ya kudariji mswada wa ‘Mkakasi’. Mashallah! Ndoto ikatimia punde baada ya Bw Ochoi wa Jomo Kenyatta Foundation (JKF) kuupitia mswada wenyewe ulionichukua miaka mitano hivi kuuandika, na mingine minne ya kujaribu kuwafikia wachapishaji. Baadhi walinipuuza; baadhi hawakunijibu, baadhi wakaniweka katika ngojangoja. Wiki moja tu baada ya Bw Ochoi kutia kiganjani ule mswada, akanipigia simu na kuniambia hivi, “Tutachapisha. Kwa hakika ni mswada mzuri!” Sauti ile ingali hai masikioni mwangu hadi leo. Iliamsha ile ilhamu. Nikanuia kuchovya asali tena na tena katika buyu hili la uandishi.
Umechapishiwa vitabu vingapi kufikia sasa?
Vingi tu. Mnamo 2013, novela ya ‘Falme Tisa’ (Oxford) yenye falsafa tele ilifuata. Huachi ng’o uanzapo kuisoma! Kabla ya kuchapishiwa novela ya ‘Ufalme wa Mende’ (Queenex), kalamu yangu ikawa tayari imetia vitabuni hadithi nyingine – ‘Raha za Peponi’ katika mkusanyiko wa ‘Kigoda cha Simanzi na Hadithi Nyingine’, vilevile ‘Safari ya Ahadi’ katika mkusanyiko wa ‘Safari ya Ahadi na Hadithi Nyingine’ (One Planet), kutaja tu baadhi.