Makala

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Nyaega Mogere

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na CHRIS ADUNGO

HAKUNA tofauti kati ya Kiswahili na masomo kama vile Kemia, Fizikia na Hisabati.

Mtaalamu wa Kiswahili ana uwezo wa kujipatia chochote kile kinachoweza kununuliwa kihalali na mhandisi, wakili, daktari au rubani kwa kukitumia na kukitumikisha Kiswahili!

Muhimu zaidi ni kufuata msukumo wa ndani ya nafsi hadi lengo lako lifikiwe. Mola anapogawa mvua habagui. Kwa hivyo, lenga kuwa bingwa au mtaalamu katika kila unachoteua kukifanya siku zote.

Huu ni ushauri wa Bw Geoffrey Nyaega Mogere, mwalimu wa somo la Kiswahili, Katibu wa Michezo katika Kaunti ya Garissa (KSSSA) na Naibu Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Garissa.

Maisha ya awali

Bw Mogere alizaliwa miaka 44 iliyopita katika eneo la Ekerenyo, Kaunti ya Nyamira na kuanza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Keng’uso.

Wavyele wake walipohamia Naivasha kusaka tonge, alilazimika kujiunga na Shule ya Msingi ya Naivasha DEB kuanzia darasa la tatu.

Lugha ya kufundishia huko ilikuwa Kiswahili ambacho kwake kilisalia adhabu ya kumuamrisha samaki kukwea mti mrefu usiku.

Aliyekuwa mwalimu wake, Bi Ouma aligundua hili na akamtwika Beatrice Bichang’a jukumu la kumfunza limbukeni Mogere Kiswahili.

Beatrice, mwanafunzi wa darasa la tatu akawa ‘mwalimu’ wa Kiswahili wa mwanafunzi mwenzake mshamba!

Kufikia darasa la sita, Mogere alikuwa mmoja wa wanafunzi bora katika somo la Kiswahili.

Mwalimu wake wa Kiswahili, Bw Gideon Nguu alimtunuku nakala asilia ya riwaya ya ‘Utengano’ baada ya Insha yake kuishindia shule yake miche mia moja ya miti katika mashindano ya Mazingira yaliyoandaliwa katika kiwango cha Tarafa.

Vipindi vya redio shuleni vilivyosimulia “Mashimo ya Mfalme Sulemani” viliwasha moto wa kutukuzwa kwa Kiswahili moyoni mwa Mogere. Aliuendeleza moto huo katika Shule ya Upili ya Nakuru (sasa Nakuru Boys) ambapo katika Kidato cha Pili, shairi lake la kwanza kabisa, ‘Mashemeji’ (AFC Leopards na Gor Mahia) lilichapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo.

Shairi hilo lilimfanya aheshimiwe sana na wanafunzi wenzake. Mwaka mmoja baadaye, alitunga shairi lililosifu “Blueband”.

Shairi hili lilighaniwa katika kipindi kimoja cha mashairi katika Idhaa ya KBC.

Shairi hilo lilimshindia shati-tao jeupe lenye picha kubwa ya “Blueband” ambalo limesalia kuwa gumzo kijijini hadi leo.

Mogere aliasi ukapera mnamo 2001 na kufunga pingu za maisha na Nana Zipporah Kerubo ambaye kwa sasa ni mwalimu wa somo la Kiingereza katika Shule ya Upili ya Heshima mjini Nakuru.

Mchango kitaaluma

Chuo Kikuu cha Moi (Bewa Kuu) kilimpa Mogere fursa ya kusomea Hisabati na masuala ya umeme katika Idara ya Teknolojia na Elimu.

Muumano kati ya Fizikia na umeme ulimtia kiwewe kwa vile usuhuba wake na Fizikia ulikuwa umeishia shuleni Nakuru pindi baada ya mtihani wa KCSE.

Aliamua kusomea Hisabati na Kiswahili katika Kitivo cha Elimu ili kutii mwito wa Kiswahili uliokuwa ukimteketeza ndani kwa ndani na kubatilisha dhana kuwa wanaosomea Kiswahili hukimbilia taaluma za lugha hiyo kwa kuogopa au kufeli Hisabati na masomo mengine ya ‘hadhi’.

Anamkumbuka Bw John Gichuki Munyua na jinsi aliyokichapukia Kiswahili kwa mapenzi ya dhati.

Ukuruba wao uliendelea zaidi walipokuwa wakitekeleza mengi ya maazimio ya Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi (CHAKIMO); Munyua akiwa mlezi naye akiwa Mwenyekiti.

Katika kufundisha kozi ya ‘Introduction to Language and Linguistics in Kiswahili’, Munyua alifanikiwa kuwashawishi wanafunzi wengi kuteua Kiswahili baada ya kujipata katika ulazima wa kutema masomo mawili mwishoni mwa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Moi.

Pamoja na Munyua, magunge wengine waliomuoka Mogere ipasavyo na kumpokeza malezi bora kiakademia ni Maprofesa Isaac Ipara Odeo, Nathan Oyori Ogechi na Naomi Luchera Shitemi (marehemu); na Madaktari Noordin Mwanakombo na Abel Gregory Gibbe (marehemu).

Magalacha hawa walikitendea Kiswahili haki na watasalia vielelezo katika safari nzima ya Mogere kitaaluma. Baada ya kuhitimu Shahada ya Ualimu, aliaminiwa kuhariri machapisho ya Chuo cha Kiswahili na Taasisi ya Lugha kilichomilikiwa na marehemu Dkt Gibbe.

Akiwa chuoni, alishiriki na kuwasilisha makala katika Semina Kuu za Kiswahili (SEKUKI) zilizoandaliwa kwa faida ya walimu wa shule za msingi na upili katika maeneo ya miji ya Eldoret, Kericho, Bungoma, Kakamega, Kisumu, Nakuru na Chuka.

Alishiriki kikamilifu mchakato wa kuanzishwa kwa Shule ya Kajiado Hill Girls’ Academy.

Anakumbuka kuumbuliwa na mwanafunzi wake Irene Mrabu aliyemuelimisha kuwa sentensi haziandikwi katika “uchache” bali kwa “umoja.” Irene alimfaa sana Mogere ambaye hadi leo anaamini kuwa akiwa mwalimu, yeye huwafunza wanafunzi wake machache huku wao wakimfunza mengi zaidi.

Mnamo 2001, alihamia katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Garissa kwa ajira ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).

Walimu wa asili ya Kisomali wanaofundisha Kiswahili katika eneo hilo la Kaskazini Mashariki ya Kenya ni adimu mno. Kati ya walimu wa hivi karibuni zaidi kufundisha Kiswahili shuleni Garissa, Msomali asilia alikuwa mmoja tu; Bw Abdikadir Ali ambaye tayari ameondoka shuleni humo.

Kwa zaidi ya miaka 17, Mogere amekuwa akilenga kuimarisha nafasi za wanafunzi wa Kisomali kusomea “kozi za kifahari” kwa kufanya vizuri katika somo la Kiswahili. Ujuzi wake wa utahini umemfaa pakubwa katika kuwaandaa wanafunzi wake kuikabili mitihani ya KCSE Kiswahili ipasavyo.

Mnamo 2013, alivikwa Shahada ya Umahiri Katika Elimu. Hii ilikuwa baada ya kuwasilisha Tasnifu “Teachers Instructional Strategies in Insha and their Influence on Class Seven Pupils’ Performance in Garissa County” chini ya usimamizi na uelekezi wa Profesa Sheila Ryanga na Dkt Adelheid Bwire.

Amewahi kufundisha kozi ya ‘Introduction to Kiswahili Literature katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara (Bewa Kuu) mnamo 2016. Kwa sasa ni mhadhiri wa muda katika Kitivo cha Sayansi za Kijamii, Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu Mount Kenya na Chuo Kikuu cha Garissa.

Amewafaa wanafunzi na walimu wengi ambao humualika kuwahimiza, kuwaelekeza na kuwashauri kila mwaka kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandalia kwa mitihani ya kitaifa.

Baadhi ya shule alizowahi kuzifaidi ni Al-farouq, Mnara Girls, Fafi Girls na Khalifa. Anaandaa mikakati ya kuzamia taaluma za Kiswahili ili kuhalalisha lakabu yake ya tangu utotoni “Doctor” ambayo ingalipo nyumbani kwao Nyamira hadi leo!

Baadaye anapalilia ndoto ya kustaafu akiwa Profesa wa Kiswahili na Mhadhiri wa chuo Kikuu.

Uandishi

Akiwa mwalimu shuleni Garissa, Mogere alitunga ‘Kalia’, mchezo ulioigizwa na wanafunzi wake katika tamasha za kitaifa za muziki na drama mjini Nakuru mnamo 2008.

Shairi lake ‘Nyamoita’ lilituzwa cheti cha ustahiki katika Daraja 1116J katika tamasha za kitaifa za muziki jijini Mombasa mnamo 2009.

Mnamo 2008, akishirikiana na mwanafunzi wake Jibril, waliasisi Daraja 1125J (Mafoka) ambalo tangu wakati huo, limeendelea kuimarishwa na kuwavutia wengi washiriki wengi wasiojua kuwa kitovu chake ni Shule ya Upili ya Garissa, Kaskazini Mashariki mwa Kenya!

Ameandika makala kadhaa za makongamano ya kimataifa ambazo anatarajia zichapishwe hivi karibuni. Daima atamshukuru, kumstahi na kumkumbuka Prof Ryanga aliyemhimiza masomoni na kumuingiza katika mkondo wa kiakademia.

Anakumbuka kongamano lake la kwanza la kimataifa (CHAKAMA-Rongo) ambalo alihudhuria kwa ufadhili wa Prof Ryanga aliyemwelekeza pia kuandaa makala aliyowasilisha katika kongamano hilo.

Kwa pamoja na Prof Ryanga, wamechapishiwa makala “Hadhi ya Kiswahili Miongoni mwa Wakufunzi wa Shule za Upili na Vyuo Vikuu” katika Kiswahili na Utandawazi (2016) na Twaweza Communications na CHAKITA. Zaidi ya makala ‘Isimu na Fasihi ya Lugha za Kiafrika’ (2018), amechapishiwa pia makala ya kitaaluma katika Jarida la Mulika nchini Tanzania (2017).

Jivunio

Mogere anajivunia wanafunzi wake wa zamani ambao alama zao za “A” ziliwakweza kusomea ‘taaluma za kifahari’ ndani na nje ya Kenya.

Hawa ni pamoja na Dkt Abdullahi Abdi (Garissa Doctors’ Plaza), Dkt Mohamed Yarrow (Nakuru) na Dkt Ali Gure (Garissa PGH).

Amewahimiza na kuwakuza Hamza Yussuf (Star FM- Nairobi, zamani akiwa KTN na NTV), Yunis Mwana wa Dekow (Chuo Kikuu cha Nairobi) na Mwalimu mwenzake wa Kiswahili Abdullahi Kassim ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu shuleni Sankuri Girls.