Makala

GWIJI WA WIKI: James Wanjagi Mutwiri

May 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

ONDOA akilini mwako dhana potovu kwamba Kiswahili ni kigumu ili ujiundie fikra mpya kuwa mbali na kusalia kito adimu na adhimu chenye thamani kubwa maishani mwa kila mpenzi wa lugha, Kiswahili kinalipa sana hasa kwa wale wanaojitolea kukitumikia kikamilifu.

Mafao ya Kiswahili yatabakia kuwa mengi na yasiyo kifani kwa kila anayeipenda lugha hiyo.

Pania mno kuongozwa na mapenzi ya dhati katika chochote unachokifanya huku ukijiweka huru kutembea na waliofanikiwa katika nyanja unazozizamia ili nao wakushauri zaidi, wakuchochee sana na kukuelekeza ipasavyo.

Huu ndio ushauri wa Bw James Wanjagi Mutwiri -mwalimu mbobevu, mwandishi chipukizi wa Fasihi Pendwa na mtaalamu wa ushairi ambaye kwa sasa anafundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Chogoria Boys, Kaunti ya Meru

Maisha ya Awali

Bw Mutwiri ndiye mziwanda katika familia ya watoto saba wa Mzee David Njagi na Bi Beterine Thereru. Alizaliwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita kijijini Ereani, eneo la Chuka, Wilaya ya Meru Kusini katika Kaunti ya Tharaka-Nithi.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Chuka DEB kati ya 1986-1994 na kuibuka mwanafunzi bora Wilayani alipokwangura alama 525 kwa 700 katika mtihani wa KCPE mwishoni mwa 1994. Alijiunga na Shule ya Upili ya Ndagani Mixed mnamo 1995 na kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 1999.

Bw Mutwiri alikuwa miongoni mwa wanafunzi watatu bora waliotokea Ndagani Mixed na kuingia chuo kikuu baada ya kufaulu vyema na kuletea shule yao sifa sufufu. Kutoka pale, Mutwiri alijiunga na Chuo Kikuu cha Laikipia kusomea ualimu akizamia sana Kiswahili na somo la Dini kati ya 2001 na 2005.

Huko, alifundishwa na wahadhiri mahiri waliompa kila sababu ya kukichapukia Kiswahili ala-kulihali bila ya kukionea aibu.

Dkt Sheila PAM Wandera alimfaa pakubwa katika suala la kujiendeleza kitaaluma, hasa katika ulingo wa sanaa ya utunzi wa mashairi. Mutwiri anaungama kuwa amechangia zaidi ya mashairi 2,000 katika kurasa za Ushairi zinazochapishwa na Taifa Leo kila wikendi na siku ya Jumatatu.

Walimu wake wa shule za msingi na upili walitambua mapema ukwasi wa kipaji chake katika utunzi wa mashairi ya Kiswahili kutokana na umilisi wake wa lugha.

Ualimu

Kabla ya kuhitimu chuoni, Mutwiri aliwahi kufundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Wise Dove akiwa mwalimu wa msimu. Aliaminiwa kuwanoa wanafunzi wa darasa la sita na saba shuleni humo.

Baada ya kufuzu mnamo 2006, alishika chaki katika shule ya St Paul’s Mariani akiwa Mkuu wa somo la Kiswahili na Naibu Mwalimu Mkuu. Mnamo 2007, alipata uhamisho hadi Kieni Girls, Embu alikoamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuhamia rasmi katika Shule ya Kitaifa ya Chogoria Boys, Kaunti ya Meru mnamo 2008.

Huko ndiko anakojipatia riziki yake mpaka leo.

Akiwa kwa sasa Mkuu wa Idara ya Kiswahili, Bw Mutwiri pia ni mtunzi na msahihishaji wa mitihani ya kitaifa ya KCSE hasa Karatasi ya Kwanza (Insha) na Karatasi ya Pili (Sarufi na Matumizi ya Lugha).

Mnamo 2008, alijiunga na Chuo Kikuu cha Chuka kusomea shahada ya Uzamili katika Fasihi, akijikita zaidi katika fani ya ushairi chini ya usimamizi na uelekezi wa Bw Enock Matundura, Bw Mugambi Bita na Profesa John Kobia waliomsaidia pakubwa kuandaa na kuwasilisha tasnifu yake.

Hamu ya Mutwiri ya kuzamia Kiswahili chuoni ni zao la kutangamana kwake kwa karibu mno na baadhi ya wanafunzi wenzake waliomwamshia ujasiri wa kukiasisi Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka (CHAKICHU).

Akiwa mtahini mwenye tajriba pevu na uzoefu mpana katika Insha na Sarufi ya Kiswahili, Mutwiri anajivunia kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuwaelekeza, kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya KCSE.

Anakiri kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Chogoria Boys, ni nguzo kubwa katika ufanisi wapatao kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotangazwa.

Mnamo 2017, Kiswahili kilikuwa miongoni mwa masomo yaliyofanywa vyema zaidi na watahiniwa wa KCSE kutoka Chogoria Boys ambao walijizolea alama wastani ya 9.5. Tangu 2008, Kiswahili kimekuwa kikiibuka bora kati ya masomo ya lazima yanayotahiniwa kila mwaka.

Akipania kuvumisha zaidi matokeo ya Kiswahili shuleni Chogoria Boys, Mutwiri analenga kuwachochea wanafunzi wake kusajili alama wastani ya 10.5 katika KCSE katika somo la Kiswahili mwaka huu.

Uandishi

Mnamo 2016, National Education Services (NES) ilimfyatulia Mutwiri diwani ‘Miale ya Mashairi’. Akishirikiana na Bi Maria Mvati na Bw James Kanuri (wahariri), Mutwiri alichangia mashairi 10 ya bahari ya kikwamba katika diwani hiyo.

Kitabu chake cha pili ni ‘Uchambuzi wa Mashairi na Maswali: Ladha ya Lugha’ alichojichapishia mnamo 2016. Baada ya Bookmark Publishers kumtolea kitabu ‘Tunu ya Lugha: Mitihani ya Karatasi ya Pili na Tatu’ mnamo 2017, Mutwiri alichapisha kitabu ‘Utamu wa Ushairi’ ambacho kina jumla ya tungo 60 za mashairi yake.

Ametunga idadi kubwa ya hadithi fupi na mashairi ambayo yamewahi kuchapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo na kufana sana katika tamasha za kitaifa za muziki mnamo 2017.

Kitabu chake ‘Mwanga wa Fasihi’ kinachorejelea mashairi yake yote yaliyowahi kutumiwa katika tamasha za muziki kote nchini mnamo 2017 kinatazamiwa kutolewa na Micharazo Publishers hivi karibuni.

Kwa kushirikiana na walimu wengine wanaofundisha katika shule mbalimbali za upili kutoka humu nchini, Mutwiri kwa sasa anaandaa diwani ‘Utenzi wa Bara’ kwa matarajio kwamba itachapishwa hivi karibuni.

Fahari

Mutwiri anajivunia kuchangia na kushiriki uendeshaji wa vipindi vya lugha katika takriban runinga na redio zote za humu nchini. Kila wikendi, angejumuika na wanafunzi wake kusikiliza vilivyokuwa vipindi ‘Kamusi ya Changamka’ (Qfm na Qtv),) na ‘Bahari ya Lugha’ (Radio Citizen).

Nyakati za vipindi hivyo vya lugha, Mutwiri angewahimiza wanafunzi wake kuwasikiliza kwa makini mikota wa lugha walioaminiwa kudadavua masuala mbalimbali yahusuyo Kiswahili kwa weledi mkubwa ajabu.

Mbali na kuchangia kwa ujasiri uendeshaji wa vipindi ‘Ramani ya Lugha’ (KBC Idhaa ya Taifa) na ‘Nuru ya Lugha’ (Radio Maisha), Mutwiri anajivunia pia kuchangia pakubwa mafundisho ya Kiswahili kupitia tovuti ya swahilihub.com.

Kwa pamoja na mkewe Bi Cecilia Muthoni ambaye ni mwanamitindo na mfanyabiashara, Bw Mutwiri amejaliwa watoto wawili – Nashlya Makena na Vivian Mutugi ambao wamepania kuzifuata nyayo za baba yao kwa kasi ya duma.