• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
GWIJI WA WIKI: John Muli

GWIJI WA WIKI: John Muli

Na CHRIS ADUNGO

HATUA ya kwanza katika safari yoyote ya ufanisi ni kufahamu kile unachokitaka; kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda.

Katika dunia hii, kuna binadamu wasio na maono. Jiepushe na kundi la watu wa aina hiyo!

Jifunze sana kutosheka na hicho kidogo ambacho Mungu amekubariki nacho. Pania kutenda yaliyo mema na ukipende kwa dhati chochote unachokifanya.

Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Ruhusu mawazo yako yatawaliwe na fikira za ushindi.

Fanya maamuzi sahihi na pangia vyema matumizi ya muda wako.

Weka Mungu mbele, vumilia, amini na ujitahidi!

Huu ndio ushauri wa Bw John Muli Munyithya – mwandishi chipukizi, mshairi stadi, mwimbaji shupavu, refa na kocha wa soka ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Charles Lwanga, Kitui.

Maisha ya awali

Muli alizaliwa mnamo Septemba 7, 1986 katika kijiji cha Ithookwe, eneo la Kitui ya Kati akiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita wa Bi Jeddidah Malombe na Bw Alex Munyithya.

Alipata elimu ya awali katika Shule ya Msingi ya Mbusyani, Kitui alikofanyia mtihani wa KCPE mnamo 2000 kisha kujiunga na Shule ya Upili ya St Charles Lwanga, Kitui mwanzoni mwa 2001.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) shuleni humo mwishoni mwa 2004 na kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea taaluma ya Ualimu (Kiswahili na Jiografia).

Aliyemchochea na kumshajiisha zaidi kutia bidii masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni aliyekuwa Naibu Mwalimu Mkuu katika Shule ya Mbusyani, Bw Titus Kamai.

Muli anatambua pia ukubwa na upekee wa mchango wa Bw Kilanga na Mwalimu Mulei katika kumhimiza kusoma kazi nyingi za Fasihi ya Kiswahili na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali wakati akiwa mwanafunzi wa sekondari shuleni St Charles Lwanga.

Bw Kilanga kwa sasa ni mkufunzi katika Chuo cha Walimu cha Kitui huku Mulei akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Wii.

Ni wakati akiwa mwanafunzi wa darasa la nne ambapo Muli aligundua utajiri wa kipaji chake katika mchezo wa kabumbu. Ingawa hivyo, mtihani mgumu zaidi aliokabiliana nao baada ya kukamilisha KCSE ni vita vya ndani ya nafsi vilivyompa msukumo wa kutaka kujitosa kikamilifu katika ulingo wa Kiswahili na kuwa ama mwanahabari maarufu, mwalimu mashuhuri au mwandishi shupavu wa Sarufi ya Lugha.

Anakiri kwamba kariha na ilhamu ya kukipenda Kiswahili zaidi akiwa chuoni ni zao la kutangamana kwa karibu sana na wahadhiri wake, hasa Dkt Joseph Nyehita Maitaria, Dkt Richard Wafula, Dkt Karanja na Dkt Mwihaki waliomtanguliza vyema zaidi katika taaluma ya Lugha na Isimu. Mbali na kupanda kisha kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya mwanafunzi wao huyu, wahadhiri hawa walimpokeza Muli malezi bora ya kiakademia anayojivunia hadi kufikia sasa.

Wengine waliomchochea pakubwa kwa imani kwamba Kiswahili kina uwezo wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Profesa Ireri Mbaabu na Profesa Kitula King’ei.

Ualimu

Muli alijitosa katika ulingo wa ualimu pindi alipohitimisha masomo yake ya sekondari. Alifundisha katika Shule ya Upili ya AIC Wii, Kitui kwa kipindi kifupi kati 2004 na 2005 kabla ya kujiunga na chuo kikuu.

Akiwa mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 2008-09, tayari alikuwa akifundisha katika Shule ya Upili ya St Peter’s The Rock, eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Nairobi.

Akisubiri kufuzu mnamo 2010, alielekea mjini Garissa kufundisha Kiswahili na Jiografia katika Shule ya Upili ya Bulla-Istin Girls. Alihudumu huko kwa kipindi cha muhula mmoja pekee kabla ya kurejea St Charles Lwanga, Kitui.

Akiwa huko, aliwahimiza wanafunzi wengi kushiriki mashindano mbalimbali ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki. Hili ni jambo ambalo anakiri kwamba lilibadilisha pakubwa sura ya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili katika shule hiyo.

Alihudumu St Charles Lwanga kati ya 2010 na 2012 kabla ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kumwajiri na kumtuma katika Shule ya Upili ya Wii alikoamsha upya ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake. Zaidi ya kuwashirikisha wanafunzi wake katika tamasha za kitaifa za muziki na drama, pia aliwakuza vilivyo katika utunzi wa mashairi na michezo ya kuigiza.

Ilikuwa hadi Januari 2019 ambapo alipata uhamisho hadi St Charles Lwanga, Kitui na kuaminiwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Zaidi ya kupiga ngoma na kucheza kayamba katika Makanisa ya Kikatoliki ya St Charles Lwanga na Kitu Cathedral, Muli pia ni kocha mkuu wa soka, kinara wa YCS na mlezi wa Chama cha Kiswahili shuleni St Charles Lwanga. .(CHAKINGA). Isitoshe, yeye ni refa wa daraja la pili la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na katibu wa marefa wote wa soka katika tawi dogo la Kaunti ya Kitui.

Anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo husika na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa yenyewe darasani. Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni St Charles Lwanga kwa sasa ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaotazamia kuvuna matokeo ya KCSE 2019 yatakapotolewa.

Uandishi

Muli anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mbali na utunzi wake kumpandisha katika majukwaa mbalimbali ya makuzi ya Kiswahili, nyingi za insha bora alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Mashairi mengi aliyoyatunga chini ya uelekezi wa baadhi ya walimu wake yalimzolea sifa sufufu na kumfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Kwa sasa anaandaa kitabu cha Marudio ya Sarufi na Matumizi ya Lugha anachotarajia kichapishwe kufikia mwisho wa mwaka huu.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu, Muli anajivunia kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili.

Uzoefu alionao katika ufundishaji wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule mbalimbali kwa maazimio ya kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu ibuka na mwafaka zaidi katika kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Muli anamstahi sana mkewe Bi Dalphine Mueni ambaye licha ya kuwa mwalimu wa Bayolojia na Zaraa katika Shule ya Upili ya Katutu Girls, Kitui Magharibi, amekuwa mstari wa mbele kumhimiza akichangamkie Kiswahili alaa kulihali. Kwa pamoja, wamejaliwa watoto wawili: Jayden John na Jaysean John.

You can share this post!

Starlets kuvaana na Ethiopia kirafiki kabla ya mechi za...

WASIA: Zingatia kigezo cha uadilifu unapoteua rafiki,...

adminleo