Makala

GWIJI WA WIKI: Justus Kyalo Muusya

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

JITIHADA za mja na neema za Maulana ni pande mbili za sarafu moja. Ni vigumu sana kwa binadamu kujitolea kwa jambo lolote lile maishani kisha Mola akose kabisa kumneemesha kwalo.

Mwenyezi Mungu hawezi kumbariki mtu pasipo na juhudi zozote kutoka kwa aliye katika uhitaji wa msaada wake. Ukijitolea kwa udi na uvumba kulimakinikia jambo lolote liwalo, hapana shaka kwamba utapokea baraka kubwa na tele kutoka kwa Muumba.

Huu ndiyo ushauri wa Bw Justus Kyalo Muusya – mwandishi shupavu, mhariri na mwalimu stadi wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Lawrence Kaluva, Kaunti ya Kitui.

Maisha ya awali

Muusya alizaliwa katika kijiji cha Kangii, kata ya Kakeani, Kitui yapata miaka 36 iliyopita. Wazazi wake ni Tabitha Muyali na mwendazake Muusya Mukuli. Ni mwana wa tatu katika familia ya watoto saba, wavulana watano na wasichana wawili.

Alisomea katika shule ya msingi ya Kangii. Baada ya kuufanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mnamo 1998, jahazi lake la masomo lilikuwa linayumba si haba, na nusura liende mrama. Hata hivyo, aliweza kujiunga na Shule ya Upili ya Kakeani.

Walimu wake wa darasa, Bw Moses Wambua (kwa sasa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Kangii) alitambua uwezo na talanta ya mwanafunzi wake huyu na akawa radhi kujitolea kwa jino na ukucha kumfaa.

Bw Wambua alimsaidia kupata ufadhili wa masomo katika shule ya kibinafsi ya Likii Hill School viungani mwa mji wa Nanyuki, Kaunti ya Laikipia. Wakati huu, Bw Wambua alikuwa amekwishampulizia Muusya mapenzi ya dhati kwa lugha ya Kiswahili.

Aliupasi vyema mtihani wake wa Kidato cha Nne.

Usomi na taaluma

Japo watu wengi, akiwamo mwalimu Wambua walimshauri kujitosa katika taaluma tofauti, aliazimia kusomea Shahada ya Ualimu (Kiswahili na Historia) ili kufuata nyayo za mwalimu na mwandani wake huyo.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, Bewa la Laikipia mnamo 2005 na kuhitimu mwishoni mwa 2008.

Huko, alipata fursa ya kutangamana kwa karibu na wahadhiri waliochochea ari yake ya kubobea zaidi katika taaluma ya Kiswahili.

Waliompa msukumo, kariha na ilhamu zaidi ya kukichangamkia Kiswahili ni Maprofesa Onyango Ogolla na Nabea Wendo, kwa sasa wa Chuo Kikuu cha Laikipia.

Muusya alipata ajira ya muda ya kufundisha Kiswahili na somo la Historia katika Shule ya Wasichana ya Mua Hills katika Kaunti ya Machakos mnamo 2008.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma baadaye kufundisha katika Shule ya Upili ya Kaluva mnamo 2010.

Mwaka uliofuata, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Masomo na Mitihani shuleni humo.

Mbinu zake za kipekee na juhudi chungu nzima zimebadilisha mtazamo wa wanafunzi kuhusu somo la Kiswahili na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa lugha hiyo miongoni mwa mwalimu shuleni Kaluva.

Jambo hili lilichangia matokeo ya Kiswahili kuimarika mno kwa kipindi kifupi. Wanafunzi wake wamekuwa wakichukulia somo hili kuwa taaluma. Wengi wao wamejiunga na vyuo vikuu mbalimbali kusomea Kiswahili.

Wengine wamejiunga na taaluma ya Uanahabari kama vile Erastus Joseph ambaye kwa sasa anahudumu katika runinga ya Kyeni.

Muusya amekuwa mhakiki shupavu wa miswada ya vitabu. Tangu 2013, amekuwa akihakiki miswada ya kazi za katika kampuni ya East African Educational Publishers (EAEP).

Hii ni baada ya Meneja wa Uhariri na Mhariri Mkuu wa Kiswahili, Bw Job Mokaya kutambua umahiri wake katika jambo hili.

Ni katika kipindi hiki ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa masomo ya kiwango cha umahiri ambapo alifuzu mnamo 2012 baada ya kuwasilisha tasnifu, “Mandhari katika Hadithi Fupi za Kisasa: Mtazamo Linganishi” chini ya usimamizi na uelekezi wa Profesa Kitula King’ei na Mwalimu Kamunde.

Chuoni humu, alitagusana na magwiji wengine kama vile Madaktari Richard Wafula, Pamela Ngugi, Edwin Masinde na Miriam Osore. Kutoka kwao, aliweza kunoa makali ya usomi na kupata na ujuzi wa kuhakiki kazi mbalimbali za Fasihi Pendwa.

Tangu ahitimu kwa shahada ya uzamili, amekuwa Mhadhiri wa muda katika South Eastern Kenya University (SEKU), Kitui akifundisha kozi za Isimu na Fasihi. Mnamo 2015, alirejea katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa shahada ya Uzamifu (PhD).

Tayari amewasilisha tasnifu yake kwa ajili ya utahini yenye mada, “Amali za Kisiasa katika Riwaya za Kiswahili za Kisasa za Mohamed na Walibora” chini ya usimamizi wa Profesa King’ei na Dkt Wafula.

Uandishi

Muusya amechapisha vitabu kadhaa. Vingine vingi vitachapishwa hivi karibuni. Kazi yake ya awali kuchapishwa ni riwaya ya Sinema Bila Malipo aliyoiandika akiwa mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika chuo kikuu mnamo 2005.

Riwaya hii ilichapishwa mwaka wa 2010.

Mwaka wa 2012, akishirikiana na Profesa King’ei na Bi Leah Mwangi (wa Chuo Kikuu cha Karatina), walichapisha Mwongozo wa Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine (JKF) na Mwongozo wa Mstahiki Meya (Target Publishers, siku hizi ni Spotlight Publishers). Mwaka uliofuata, walishirikiana tena kuandaa Mwongozo wa Kidagaa Kimemwozea (EAEP).

Mnamo 2015, Kyalo alichapisha Mwongozo wa Msururu wa Usaliti (EAEP) na kushirikiana na King’ei kuandika Mwongozo wa Mwakilishi wa Watu (EAEP).Miongozo hii imekuwa ikitumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita kwa minajili ya mafunzo ya Uchambuzi wa Fasihi nchini Uganda.

Mwongozo wa Kigogo aliouandika kwa ushirikiano na Evans Makhulo ulichapishwa na Phoenix Publishers mnamo 2018.

Zaidi, Muusya ameshirikiana na Bw Simon Ngige (Shule ya Wavulana ya Alliance) kuandika kitabu Magwiji wa Kiswahili – Miigo ya KCSE kilichochapishwa na EAEP.

Aidha, ameshirikiana na Leah na King’ei kuandaa mswada kuhusu mashairi wenye mada, Sanaa ya Ushairi: Historia na Uchambuzi. Kazi hii iko katika hatua za mwisho za kuchapishwa na shirika la Kenya Literature Bureau (KLB).

Muusya amechangia hadithi ‘Kusisimua Misuli’ katika diwani ya ‘Tutaonana Tena na Hadithi Nyingine’ iliyohaririwa na Stella Were na Edison Wanga.

Vilevile, diwani ya hadithi fupi ambayo ameshirikiana na Profesa King’ei kuihariri yenye kichwa, Kusukuma Kitu na Hadithi Nyingine itachapishwa na phoenix hivi karibuni. Kwa sasa anashughulikia mswada wa riwaya wenye anwani Mbio za Sakafuni.

Familia

Muusya ana familia. Mkewe Ann Kavuu Kyalo ni tabibu katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Machakos. Wawili hao wamebarikiwa na wavulana wawili, Moses Mumo na Ken King’oo.

Jivunio

Muusya ameasisi nadharia mpya ya uhakiki wa fasihi iitwayo Daindamano. Daindamano ni istilahi iliyotokana na mawazo ya wanafalsafa ya daintolojia (Deontology) na umaandamano (Consequentialism). Daintolojia na umaandamano ni falsafa za Immanuel Kant na Stuart Mill mtawalia.

Mhimili wake mkuu ni kuwa kiongozi yeyote haruhusiwi kutenda kitendo kisichokubaliwa na wanajamii anaowaongoza, isipokuwa ikiwa kwa kutenda kitendo hicho matokeo yake yatanufaisha wengi, hata kama kitawaumiza wachache. Mawazo haya aliyawasilisha katika Chuo Kikuu cha Kenyatta katika usomi wa uzamifu na kukubaliwa na wataalamu wa fasihi chuoni humu.

Aidha, aliwasilisha mawazo haya ya kinadharia katika kongamano la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (CUEA) jijini Nairobi mnamo Disemba 2016. Ana imani kubwa kuwa atakapochapisha na kusambaza mawazo haya kuanzia mwaka huu, yatapata wafuasi na wachangiaji wengi kote ulimwenguni.

Maazimio

Anaazimia kuwa mwandishi wa kazi za kubuni hasa za kinathari zitakazopata wasomaji wengi.